Majaliwa ataka jamii za kifugaji kutotumikisha watoto

Mwanga. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amezitaka jamii za kifugaji kuhakikisha zinawapeleka watoto shule na kuacha tabia ya kuwatumikisha kuchunga mifugo.

Amesema Serikali imeweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa elimu nchini ili kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora.

Majaliwa ameyasema hayo leo Jumanne Machi 25, 2025 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Usangi Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.

“Tumejenga shule za msingi na sekondari na sasa tunajenga vyuo vya ufundi na vyuo vikuu, tunapeleka walimu wa kutosha, vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Rais Samia (Samia Suluhu Hassan) amesema kuanzia chekechea hadi kidato cha sita hakuna ada wala michango ya ovyoovyo.

“Hivyo nitoe wito kwenu, pelekeni watoto shule hakuna sababu ya kutompeleka mtoto shule ambapo hakuna ada, hiyo pesa tuliyonayo sasa mnunulie sare, avae viatu vizuri, mwandalie chakula aende shule akasome arudi.

“Nataka niwaambie kwenda shule ni lazima na nataka nizungumze tena leo, najua jamii nyingi huku ni za kifugaji, watoto huku ndio wanaochunga ng’ombe,” amesema Majaliwa.

Naye mbunge wa Mwanga, Joseph Thadayo ameishukuru Serikali kwa kujenga chuo kikuu kimoja na kuboresha miundombinu ya majengo ya sekondari katika shule tano wilayani humo.

Katika hatua nyingine, Majaliwa amemtaka Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Dk Serijo Kusekwa kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya vinakuwa na dawa za kutosha ili kuepusha wananchi kuelekezwa kununua dawa kwenye maduka binafsi.

“Sitarajii hapa Mwanga, mwananchi kwenda hospitali, kituo cha afya na zahanati anaandikiwa kikaratasi akanunue dawa nje kwenye maduka ya dawa ya binafsi. Mganga Mkuu simamia dawa zipatikane kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, acheni kununua dawa ambazo kwa ‘nature’ (asili) ya eneo hili hakuna magonjwa yake”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *