Majaliwa ataja sababu kutoanzishwa maeneo mapya ya utawala

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema watakapojiridhisha na utoaji huduma, miundombinu na rasilimali watu kwenye maeneo mapya ya utawala ndipo Serikali itatoa vibali vya uanzishwaji wa maeneo mapya, pamoja na kufafanua fursa ya mikopo ya asilimia 10 kwa wanaume.

Mwaka 2016 wakati wa kuhitimisha mjadala wa bajeti ya Waziri Mkuu, alitoa tamko la kusitishwa mamlaka mpya za utawala.

Kwa muda mrefu wabunge wamekuwa wakihoji kuhusu uanzishwaji wa maeneo mapya, ikiwemo Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi ambaye Juni 28, 2024 aliyehoji ni kwa jinsi gani tangazo hilo litafika mwisho ili mamlaka mpya za utawala ziweze kutangazwa.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange alisema kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika kukamilisha miundombinu katika mapenepo mapya ya utawala.

Leo Alhamis Februari 13, 2025, Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Priscus Tarimo naye ameibuka na swali hilo katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Tarimo amehoji ni nini mpango wa Serikali kwa kuzipandisha hadhi halmashauri za serikali za mitaa ambazo zimeshapitia hatua zote za wilaya, mikoa ilizipandishwa hadhi.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema ni kweli upo uhitaji wa maeneo mengi ya Serikali za Mitaa ya kupandishwa hadhi na hata yeye (Tarimo) ameshakwenda mara kadhaa kwake akiomba kupandishwa hadhi kwa halmashauri yake.

“Tunatambua zipo halmashauri zimeshapitia katika hatua zote za kupandisha hadhi na Serikali imekuwa ikifanya hivyo na mara ya mwisho tulisimama kidogo kutoa fursa maeneo mapya ya utawala ili, kuyawekea tunayawekea miundombinu maeneo mapya yaliyopo,” amesema.

Amesema kinachofanyika hivi sasa katika maeneo hayo mapya ni kuimarisha katika utoaji huduma kwa wananchi na kuwa pindi watakapojiridhisha kuwa utoaji huduma, miundombinu imekamilika, raslimali watu inatosha na hali ya fedha za kujiendesha ni nzuri wataendelea kutoa vibali kwa maeneo mapya ili maeneo yote yenye uhitaji wa mamlaka mpya iweze kupata.

Majaliwa amesema Tamisemi itashughulikia suala la hilo ikiwemo la kupandisha hadhi Halmashauri ya Moshi kulingana na wakati na kukamilika kwa mahitaji ya rasilimali watu, miundombinu na hali ya fedha za kujiendeshea kuwa nzuri.

Mbunge wa Hai (CCM) Saasisha Mafuwe amehoji Serikali iko tayari sasa kuruhusu wanaume nao kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa kuwa kundi hilo limeachwa nyuma.

“Kumekuwa na malalamiko makubwa ya akinababa ya kukosa fursa hiyo na wao ndio wakuu wa kaya na wa familia hizi. Serikali haioni ni wakati wa kufanya marekebisho ya kanuni za mikopo hiyo ili kundi hilo linufaike na mikopo hiyo bila kigezo cha umri,” amehoji.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema upatikanaji wa fursa za mikopo lilifanyiwa tathimini na kugundua kuna makundi yana fursa ndogo ya kupata mikopo inayotolewa.

“Makundi hayo ambayo baadaye tulianzishia mikopo maalumu kupitia halmashauri zetu nao ni wanawake, vijana na walemavu hivyo tuliamua kuanzishia makundi maalum,” amesema.

Majaliwa amesema wanaume walikuwa na nafasi nzuri ya kupata mikopo hata baada ya kubadilisha umri wa kupata mikopo hiyo (kutoka miaka 35 hadi miaka 45).

Amesema baada ya kufanya tathimini walibaini wengi waliokuwa wakipata mikopo katika taasisi za fedha walikuwa ni wanaume kuliko wanawake.

Majaliwa amesema hata kijana anapofika miaka 45, anaweza kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali na kuwa kwa kugawa katika mgawanyo huo wanajua sasa watu wote wanaweza kupata fursa ya mikopo.

“Tumeshazungumza na taasisi za fedha kufungua dirisha la mikopo kwa wajasiriamali wote kuhakikisha kila anayefika anapata mikopo hiyo ili kuwafanya Watanzania kubuni miradi na kupata mitaji,” amesema.

Amesema wataendelea kuboresha utoaji wa mikopo ili kila mtu aweze kupata mikopo hiyo.

Naye Mbunge wa Kinondoni (CCM), Abbas Tarimba amesema Serikali haioni kuwa mfumo unaotumika hivi sasa wa ukarabati wa barabara umefeli na haufanyi kazi.

Amehoji Serikali haioni ni wakati sasa wa kurejesha mfumo uliokuwepo mwanzo wa halmashauri kutumia karakana na mitambo au Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) badala ya kuwapa wakandarasi binafsi.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema awali barabara hizo zilikuwa zikikarabatiwa na halmashauri lakini kwa kuwa zinauwezo wa mapato tofauti na kwamba baada ya kusikia maoni ya wabunge na kufanya tathimini ya ukarabati wa barabara waliamua kuanzisha Tarura.

“Tunaendelea kufanya tathimini ya utendaji wa Tarura lakini hadi sasa imeendelea kufanya vizuri kwa sababu wameendelea kufanya ukarabati na kujenga na tunaona mafanikio yanayofanywa na sisi tunaongeza bajeti,” amesema.

Majaliwa amesema wataendelea wakandarasi kupitia Tarura ili wakandarasi wanaopatiwa kazi wajenge barabara zinazoweza kudumu kwa viwango wa vilivyowekwa ili ziweze kutumika kwa muda mrefu.

“Lakini tutaendelea kuipatia fedha Tarura kwa ajili ya matengenezo ya muda mfupi mfupi ili waweze kuziba mashimo pale yanapotokea badala ya kukaa muda mrefu,”amesema.

Majaliwa ameagiza Tarura kujikita katika kuhakikisha wakandarasi wanaopewa kazi wanakuwa na uwezo wa kujenga na watumie fedha wanayopewa ya matengenezo  kuziba mashimo yanayotokea.