Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ushiriki wa viongozi wa dini katika mipango ya maendeleo ya jamii unasaidia kwa kiasi kikubwa kusonga mbele.
Alisema mahubiri wanayotoa yanayokanya na kukemea maovu yanasaidia kuleta mahusiano mazuri na kuhamasisha uwepo wa amani katika jamii.

Baadhi ya wananchi wakiwa katika maombi ya kitaifa viwanja wa Leaders, Dar es Salaam.
Majaliwa amesema hayo katika maombi ya kitaifa yaliyofanyika Februari 28, 2025 kwenye viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Maombi hayo yamelenga kuwaunganisha waumini kutoka maeneo mbalimbali kuliombea Taifa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Alisema viongozi hao kupitia taasisi zao wamekuwa wakishirikiana na Serikali katika kuhakikisha huduma muhimu za kijamii zikiwemo shule, hospitali, maji na nyinginezo zinapatikana katika maeneo yote nchini.
Kupitia mahubiri amesema wamekuwa wakiwasisitiza waumini kuacha maovu, kufanya kazi kwa bidii na kuitunza amani ya nchi.

Baadhi ya ananchi wakiwa katika maombi ya kitaifa viwanja wa Leaders, Dar es Salaam.
“Ninatoa rai kwa viongozi wa dini na Watanzania wote msichoke kuiunga mkono Serikali yenu ili sote tuendelee kuishi pamoja kwa amani, upendo na mshikamano,” amesema.
Amesema Serikali inatambua wajibu mkubwa wa kiroho walionao ambao unaleta matokeo chanya katika maisha ya kila siku.
“Endeleeni kujitoa kwa ajili ya Taifa letu, viongozi na wananchi wake, hatuna shaka na imani yenu na mapenzi yenu kwa Serikali,” alisema.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa katika maombi ya kitaifa yanayofanyika Februari 28, 2025 kwenye viwanja vya Leaders Club Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema huwa anasikitishwa kuona kiongozi mmoja wa dini akimsema mwingine.
Alilifananisha tukio hilo na kitendo cha wazazi kutoleana lugha chafu mbele ya watoto wao.
“Mimi kama muumini nikiona vitendo hivyo huwa naiona roho ya shetani katikati na siyo ya Mungu,” amesema.
Amewasihi viongozi hao kuacha tabia hiyo na kuendelea kuhubiri upendo na amani kwa waumini.

Viongozi wa madhehebu mbalimbali wameshiriki kuliombea Taifa, uchaguzi uwe wa amani na kuwaombea Watanzania.
Baadhi ya viongozi hao ni Nabii na Mtume kutoka Kanisa la Inuka na Uangaze, Boniface Mwamposa, Nabii Clear Malisa, Mtumishi Allen Siso, Jacob Mwakibinga, Gidion Palapanda, Kuhani Mussa Mwacha, Padri Joseph Ngonyani na Askofu Emmanuel.
Waimbaji wa nyimbo za injili kadhaa walishiriki wakiwamo, Rose Muhando, Bella Kombo na Ambwene Mwasongwe.

Hali ilivyokuwa jioni katika viwanja vya Leaders kabla ya jua kuzama.
Akizungumza na Mwananchi Joseph John, mshiriki wa maombi hayo alisema yamefanyika muda muafaka ikizingatiwa mwaka huu ni wa uchaguzi.
“Mwaka huu ni wa uchaguzi tunatakiwa kumuomba Mungu uwe wa amani, tuweze kupata viongozi watakaotusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo,” alisema.
Justa Mwakangale, kwa upande wake alisema ni jambo la baraka kwa watumishi wa Mungu kutoka madhehebu mbalimbali kuungana na wananchi kuliombea Taifa.