
Dodoma. Waziri Mkuu na Mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya maandalizi ya fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (Chan) 2025 na fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2027, Kassim Majaliwa amesema Tanzania imejipanga kubakiza mataji hayo mawili nyumbani.
Majaliwa aliyasema hayo leo Jumamosi Februari 1,2025 jijini Dodoma katika bonanza la Azania Bunge Bonanza lililohusisha mashabiki wabunge wa Simba na Yanga.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya mashindano hiyo Majaliwa amesema yanaenda vizuri hasa katika miundombinu.
“Maandalizi yetu siyo kushiriki tu katika mashindano hayo bali tumejiandaa na inawezekana pasipo shaka kulibakiza kombe hilo nyumbani. Naomba Watanzania wafahamu hilo uwezo tunao kwa sababu hata ligi yetu imeendelea kuwa bora Afrika,” amesema Majaliwa
Majaliwa amesema wakaguzi wa viwanja wamefika nchini na wameridhika na maandalizi ya mashindano hiyo.
Wakati huohuo Waziri Mkuu amewahamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kutokomeza magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
“Mazoezi husaidia kuimarisha afya na kinga ya mwili hasa kwa watu ambao wanafanya kazi maofisini kwani wanatumia muda mwingi kukaa,” alisema Waziri Mkuu.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson amesema wataendelea kuongeza ubunifu katika mabonanza yanayokusanyisha wabunge na wananchi ili kuvutia watu wengi zaidi kushiriki kwa manufaa yao.
Muamko wa mabonanza yanayoandaliwa na Bunge unazidi kuwa mkubwa kila mwaka na mahudhurio yanaongezeka na mwaka huu kuna wananchi wametoka majimboni kuja kushiriki mashindano hayo.
“Ubunifu wa kuwaita mashabiki wa Yanga na Simba ni kwa mara ya kwanza tunafanya hivi lengo likiwa ni kuendelea kuongeza ubunifu ili kuvutia wananchi wengii zaidi kushiriki. Bonanza la mwaka huu limekuwa na mwamko mkubwa kwa sababu washiriki wengine wametoka majimboni kuja kushiriki,” amesema Dk Tulia
Ofisa Matekelezo Mwandamizi kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Ritha Nguruwe amesema mazoezi ni muhimu kwa watumishi ambao muda mwingi wanautumia wakiwa wamekaa kwani yanasaidia kuepusha na magonjwa yasiyo yakuambukiza.
“NSSF tumeshiriki katika bonanza la Azania Bunge Bonanza lengo ni kuendelea kuhamasisha watumishi kufanya mazoezi kwasbabu ni muhimu kwa afya hasa kwetu sisi watumishi ambao muda mwingi kazi zetu tunazifanya tukiwa tumekaa,” amesema