Mapigano makali yaliripotiwa Jumanne ya wiki hii katika eneo la Nyangezi lililoko umbali wa kilometa 20 kaskazini mwa mji wa Bukavu mashariki mwa nchi ya DRC kati ya waasi wa M23 na wale wa Mai Mai Wazalendo.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Mashuhuda wanasema milio ya risasi ilisikika tangu mapema asubui wakiripoti kwamba ni wazalendo waliojaribu kushambulia ngome za M23 katika eneo hilo la wilaya ya Walungu. Milio ya risasi ilisikika kuanzia milima ya Kamina wilayani Walungu hadi vijiji vya Mumosho na Nyakabongola maeneo ya Mudusa katika wilaya ya Kabare, si mbali na jiji la Bukavu.
Vyanzo kadhaa vimebaini kuwa M23-AFC waliokuwa na silaha nzito wamefanya harakati kueleka upande wa mapambano hayo ambapo milio ya risasi na silaha nzitonzito imesikika eneo linaloitwa Toyota kwenye barabara ya taifa namba tano, bila kutoa ushahidi zaidi.
Mapambano hayo yalisitishwa majira ya saa tano ikiaminika kwamba wapiganaji wa Maimai Wazalendo wamerejea milimani.
Tukio hili limeongeza hofu miongoni mwa wakazi wa Nyangezi na Mumosho hata pia Nyantende. Wengi wao walikuwa tayari wamehama makazi yao wakijihifadhi msituni siku tatu zilizopita, na wengine wamebaki nyumbani.
Hadi hapo hakuna tangazo lolote lililotolewa na pande zote hasimu kuhusu mapigano haya. Imepita wiki mbili tangu mapambano mengine yaliyoripotiwa katika eneo hilo wakati wa shambulio lingine la Wazalendo dhidi ya ngome za M23 katika vijiji vya Nyangezi na Nyantende.
M23 imeongeza uwepo wake katika baadhi ya maeneo ya mji wa Bukavu yanayopakana na wilaya za Walungu na Kabare.
William Basimike, Mumosho, RFI Kiswahili