Dar es Salaam. Wakati wengi wakikata tamaa kutokana na maumivu mbalimbali ikiwemo ya mapenzi, maisha na mengine, lakini kwa upande wa mtengeneza maudhui na mwigizaji Collins Frank ‘Best King’ yamempa maisha.
Staa huyo wa TikTok anaipokea Mwananchi nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam maeneo ya Mbezi Kimara na kuliambia gazeti hili, safari nzima mpaka kupata umaarufu uliomfanya kufanya kazi na mastaa wakubwa ndani na nje ya nchi.
Ilivyoanza
Anasema, alipofika elimu ya Sekondari aligundua kuwa anavipaji vingi, kwani alikuwa akicheza michezo yote, huku akiwa Kiongozi wa Michezo shuleni.
“Nilikuwa nacheza mpira wa miguu namba 5, kikapu, volebo, muigizaji, muandaaji maudhui na kukaa nyuma ya kamera, nje ya uongozi niliokuwa nao.

Jina la Best King ndipo lilianza kwani mmoja kati ya marafiki zangu aliona uwezo wangu mkubwa wa kufanya vitu vingi kwa uzuri ndio maana akaniita hivyo.
“Napenda sana mpira wa miguu kuliko michezo yote, lakini sikuwa na mpango wa kuwa mchezaji ila nimekuwa shabiki wa Simba kwa kipindi kirefu sana,” anasema.
Mahusiano yalivyomfungulia dunia
Anasema kama ilivyo kawaida ya mapenzi, ukipenda lazima uone wivu, na hutaki kabisa kumpoteza au achukuliwe na mwingine kwa sababu ya kitu ambacho wewe huna ndivyo ilivyokuwa pia kwake.
“Nilikuwa na mpenzi wangu niliyempenda sana lakini baadaye aliamua kuwa na staa wa TikTok kwa wakati huo, iliniumiza sana na nikaona anachoweza kufanya mwanaume mwenzangu hata mimi nakiweza pia.
“Hivyo kwa kuanza nilikuwa nachukua video na kuzitengeneza lakini sio kwa kuzirusha TikTok, lakini watu wengi walikuwa wananishauri nifungue akaunti ya mtandao huo na hapo ndio nilianza.
“Kwa hiyo nilianza kwa kuangalia wenzangu wanafanya nini na siku moja nikajirekodi video moja ikielezea mambo ya mapenzi ambayo ilipata watazamaji laki saba ndani ya siku moja na afuatiliaji waliongezeka pia,” anasema.
Alivyokutana na Kizz Daniel
Collins aliyejulikana zaidi baada ya kupostiwa na staa wa Nigeria Kizz Daniel, akifanya challenge ya wimbo wa msanii huyo ‘Marahba’ amesema siyo tu video yake kupostiwa na staa huyo bali alipewa na mchongo.
“Mimi ndio Tiktoker pekee niliyepostiwa na staa huyo katika shindano la wimbo wake mpya, alinitafuta akaniunganisha na kijana mwingine ili niweze kupaisha moja kati ya wimbo wake uliokuwepo katika albamu yake.

“Alinipa pesa nyingi kidogo kama milioni mbili na laki tano hivi kwa video mbili, lakini kubwa ilikuwa uaminifu ambao aliuonesha kwangu. Kwa upande wa Afrika Mashariki kuona mimi ndiye nafaa kufanya kazi yake,” anasema.
Nyimbo za mastaa
Muda mwingi amekuwa akirekodi nyimbo za mastaa kama Diamond, Marioo na wengine lakini anasema siyo wote wanaomlipa ingawa wapo wanaompatia pesa kama shukrani.
“Kila ninachokituma kwenye mtandao wangu huwa nina sababu maalumu hasa hizi nyimbo ambazo ni za mastaa na ni mpya huwa zinasikilizwa sana na watu hivyo nikijirekodi naongeza watazamaji kwake na kwangu.
“Kuna muda wanakupa mkono wa Shukrani kwani sio malipo ambayo mnayapanga kutokana na matokeo wanayaona kupitia video yangu na hiyo kwake ni pesa,”anasema.
Diamond Kitambo
Collins anasema japokuwa amekulia Dodoma, alizaliwa na kuishi Tandale huku nyumba yao ikitazamana na ile ya staa wa Bongo Fleva Diamond.

“Sina ukaribu naye ila napenda kufanya video za muziki wake kwani kwangu naona fahari kumuunga mkono kaka niliyeishi naye mtaa mmoja.
“Lakini katika hali ya utoto hujui alishawahi kukusaidia nini kwa sababu tulikuwa karibu sana na ninachokumbuka aliwahi kunikodishia CD mtaani, hivyo namkubali sana.”
Video ngumu zaidi
Anasema moja kati ya kazi aliyoifanya kwa muda mrefu ni ile ya shindano nyimbo ya Marhaba ambayo ilimtaka kuvaa nguo nyingi.
“Nilirekodi masaa 15 na siku zote anayekuwa nyuma ya kamera ni mpenzi wangu kwani yeye ndiye ‘Director’ wangu, lakini kiukweli ilikuwa kazi ngumu na nilipomaliza nilikuwa naumwa kabisa mapumziko yalikuwa ni kula tu.
“Japokuwa watu wanaona ni kazi ya ajabu lakini video ile ilinipa faida kubwa ya matangazo na moja wapo ni Duka kubwa Kenya, mmiliki alinitafuta kutaka nifanye naye kazi na kwa rekodi moja alinilipa Elfu 50 ambayo kwa Tanzania ni milioni moja na kifurushi changu ni kuanzia mwezi.”
Muda anaotumia
Anasema huwa ana mikakati maalumu ya kuandaa maudhui, hivyo huwa anaandaa na kufanya kazi zingine binafsi.
“Kwa wiki natenga siku mbili za kurekodi maudhui yangu yote ya wiki nzima na huwa napata video zaidi ya 10 zikiwemo za matangazo ya wateja wangu na mashabiki pia, hivyo kila siku naachia mbili.
Kwa video moja natumia saa hadi mawili japo zinaonekana fupi lakini mambo huwa ni mengi ikiwemo marekebisho ili kufanya kazi itoke kwa uzuri na kuvutia zaidi,”anasema staa huyo.
TikTok inalipa
Anasema kwake mtandao huo unalipa, mtu akimuona anacheza anaona kama kazi rahisi na kila mtu anaiweza kumbe sivyo.
“TikTok ina namna mbili ya kulipa kwani ukiwa mubashara watazamaji wanaweza kukutumia zawadi ambayo zinahesabika kama pesa. Lakini kwa Nchi za wenzetu wanalipwa kutokana na wingi wa watazamaji.
“Mimi nina akaunti ambayo iko kwa mfumo huo wa nje ya nchi hivyo kila mwisho wa mwezi huwa wananitumia pesa ambayo sio chini ya dola 500 na namba za watazamaji wangu na hapo ni nje ya matangazo ambayo kila mteja huwa na bei yake.
“Zipo video zinawatazamaji hadi milioni kwa watazamaji 50 huwa nalipwa dola 10, hivyo ni rahisi kwangu kuendesha maisha na kuishi vizuri mjini,” anasema .
Kuigiza balaa
Anasema safari ya uigizaji ilitokea akiwa chuo katika harakati zake za kutengeneza maudhui ya kupandisha katika mitandao yake ya kijamii.
“Wanaosoma Mlimani kuna sehemu maarufu sana wanachuo wengi wanapenda kukaa na kupata chakula panaitwa ‘Cafe One’ kwa hiyo tuliamua kupita na sahani za mabati katikati yao huku tunacheza muziki.
“Hivyo kila mtu akainuka na kuanza kuturekodi katika umati ule tulipostiwa sana, jambo ambalo likafanya wengi watufahamu kuna kaka alimaliza chuoni pale akawa ameona hiyo video alikuwa na filamu yake, hivyo akanitafuta na kunipa dili hilo japokuwa alishaandaa watu tayari ila alimtoa mmoja wapo ili mimi niingie.
“Walinipitisha na sikujua kama filamu hivyo itafika DSTV na kunipa jina lililopelekea kupata Tuzo ya Mwigizaji Bora Chipukizi 2022 na mwanzo ndipo ulipoanzia.”
Uhusiano na shemeji yake
Moja kati ya jambo linalowapa maswali mashabiki wake ni ukaribu na shemeji yake anayejulikana kama Ms Mary, ambaye amekuwa akifanya naye maudhui mengi (video).
“Nilianza kufahamiana na dada yake ambaye ndiye mama wa mtoto wangu na kuanza kujirekodi naye video ilianza pale aliponiambia ukweli juu ya hofu yake ya kutumia mitandao. Sionekani na mpenzi wangu kwa sababu yeye hapendelei mambo hayo, ni muongozaji msaidizi wa filamu ya Jua Kali hivyo anafurahia zaidi kunirekodi.

“Tupo kwa ajili ya kufanya kazi nzuri mimi na Ms Mary ambaye ni shemeji yangu tunaendana sana katika sanaa, huku tukishirikiana na mpenzi wangu ambaye ni mbobezi wa kazi hiyo,” anasema.
Ukaribu wake na wachezaji
Staa huyo anasema anafahamiana na wachezaji wengi ambao ni marafiki na mashabiki wake, hivyo huwa wanamfuatilia kwenye kazi zake kila wanapopata muda ili kujua yanayoendelea.
“Marafiki zangu ni Mohamed Hussein ‘Zibwe (Simba), Aziz K, Dickson Job,Abutwalib Mshery na wengine, lakini Ki ni kama familia na nilikutana naye kupitia mpenzi wangu.

“Ukaribu wetu umekuwa mkubwa kawa kama familia na ni mtu mstaarabu sana anayeweza kujua ustaa wake wa uwanjani sio wa mtaani na huwa ananiuliza maswali ya muhimu kuhusu maisha, hivyo ni mtu anaejielewa.”
Watani noma
Anasema anaishabikia Simba na matokeo yaliyowahi kumpashida zaidi ni yale ya msimu uliopita baada ya timu hiyo kupigwa mabao 5-1 dhidi ya Yanga mechi iliyochezwa Novemba 5, 2023.
“Kufungwa kunaumiza zaidi ila wapinzani wetu wanachopitia kwa sasa kupoteza mechi mbili mfululizo ni hali ya kawaida sana ila tatizo lao wanajiamini sana japokuwa ni kweli wanatimu bora.
“Matokeo haya yanatupa amani sana mashabiki wa Simba na huwa nafanya video mubashara wanapokuwa na wakati mgumu huku nikiwa nimevaa jezi ya timu yetu, kwani na sisi walishatunyooshaga.”
Ushindani
Anaweka wazi kuhusu vijana kujiajiri na ushindani uliopo katika mitandao ya kijamii kwani wengi wameona fursa ambayo ndani yake inahitaji utulivu mkubwa.
“Hii Mitandao inahitaji heshima sana na umakini kwani watu wengi wanaona vijana wanaofanya video ni kama wahuni na hawana kazi ya kufanya.
“Hivyo ni lazima uwe na malengo na usimsikilize mtu yeyote kwani kila kitu kinawezekana hasa ukijua nini unachotaka kukifanya,”anasema.
Changamoto kubwa
Anasema moja kati ya shida kubwa inayojirudia kila wakati ni maoni mabaya kutoka kwa watu ambao hawajui uhalisia wake.
“Kila mtu anapitia mambo tofauti kwenye maisha yake na huwezi kumpangia maoni gani anatoa japokuwa wakati mwingine inaumiza.”