Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Saudi Arabia, Ghassan al-Nuwaimi, miongoni mwa mahujaji wanaotekeleza ibada yao mwaka huu, milioni moja na nusu wanatokea mataifa ya kigeni, idadi iliyo chini kidogo na ile ya 1, 611,310 walioshiriki ibada hiyo mwaka jana.
Safari ya kuelekea milima na viwanja vya Arafa ilianza jana Jumatano, kwa wengi wa mahujaji kutembea kwa miguu wakiwa wamebeba mizigo yao, huku hali ya hewa ikifikia nyuzijoto 40.
Soma zaidi: Mahujjaji wakusanyika Arafat katika kilele cha Hijja
Picha kwenye mitandao ya kijamii na vyombo rasmi vya habari zinawaonesha wengine wakiwa wamewabeba mahujaji wenzao wasiojiweza migongoni mwao wakielekea kwenye eneo hilo tukufu, ambalo zaidi ya miaka 1,400 iliyopita, kiongozi wa Waislamu, Mtume Muhammad (S.A.W) alitoa kile kiitwacho Hotuba ya Kuaga, iliyokuwa ya mwisho kwake na iliyoutangaza rasmi Uislamu kuwa dini ya ulimwengu mzima.
Umuhimu wa Siku ya Arafa
Kwa mahujaji, kufika kwenye eneo hilo ni sehemu muhimu sana ya ibada hiyo na takribani kilele cha imani, kwani kunawakumbusha siku ya makutano ya wanaadamu wote mbele ya Muumba wao, yaani Siku ya Kiama.
“Ni hisia zisizoweza kuelekeza. Utukufu ni wake Mwenyezi Mungu. Ni kama kwamba malaika wameufunika mwili wangu, na sihisi kitu chengine chochote. Nahisi moyo unatetemeka kwa furaha, matumaini na uhakika kwamba Mwenyezi Mungu atatusamehe makosa yetu na na kuzikubali dua zetu. Mtu akiiona madhari hii, utukufu wake Mungu, tupo kwenye Mlima wa Rehema, na ni kama rehema imetushukia.” Alisema Hassan Ali Salameh, hujaji kutokea Misri.
Soma zaidi: Mahujaji waelekea Arafat, wengine wajiandaa kwa Eid al-Adha
Kwa mujibu wa masimulizi ya Mtume Muhammad (S.A.W), Siku ya Arafa ni siku tukufu kabisa kwenye mwaka, kwani ni siku ambayo Mwenyezi Mungu mwenyewe hujikaribisha zaidi kwa waumini na kuwasemehe madhambi yao.
Mahujaji wanabakia kwenye Mlima na viwanja vya Arafa kwa ibada na dua kutoka jioni hadi asubuhi, na baada ya machweo ya watakwenda kwenye viwanja ya Muzdalifah kukusanya vijiwe vitakavyotumika kwenye sehemu ya ibada inayoitwa kumrushia mawe ibilisi.
Saudi Arabia yajipanga kwa Hijja
Saudi Arabia mwaka huu imetumia mabilioni ya dola kwenye hatua za kudhibiti usalama wa mahujaji, lakini kiwango kikubwa cha mahujaji kinaonekana kuzifanya hatua hizo kuwa na athari ndogo kwenye usalama wao. Mojawapo ya changamoto kubwa kabisa kwenye hija za miaka ya karibuni imekuwa ni kiwango kikubwa cha joto.
Mapema wiki hii, Waziri wa Afya wa Saudi Arabia, Fahad bin Abdulrahman Al-Jalajel, alisema kwamba miti 10,000 imepandwa kwenye eneo hilo ili kutowa kivuli kwa mahujaji, mbali ya vitanda vya hospitali na idadi ya wafanyakazi wa huduma za afya walioongezwa takribani mara tatu kuliko miaka mingine.