MAHUBIRI: Kila gumu unalolipitia Mungu akuinulie mtetezi

Bwana Yesu asifiwe, karibu katika tafakari ya neno la Mungu. Nitakayekulisha Neno ninaitwa Mwalimu Peace Rubagora kutoka Busega Simiyu.

Kipekee ninamshukuru Mungu kwa kunipa kibali cha kusema na wewe siku ya leo na ni maombi yangu kuwa unaposoma ujumbe huu Roho Mtakatifu akuhudumie, aguse hitaji la moyo wako na amani ya Kristo itawale ndani yako.

Leo tumepewa ujumbe unaosema “Katika kila unalolipitia Mungu akuinulie mtetezi.” Mpendwa tunaishi katika dunia ambayo tumezungukwa na watu wa kila aina, watu ambao wanatuwazia mabaya na wengine mazuri, pia ni vigumu sana kujua ni yupi aliye sahihi kwako.

Tunahitaji neema ya Mungu ili tuweze kupata watu sahihi wa kuambatana nao, watu ambao watakuwa upande wetu katika hali zote.

Maneno ya Mungu katika Kitabu cha Mathayo 10:36 yanasema “Na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake”. Hii inadhihirisha kuwa ni vigumu kujua nani anawaza nini kwa ajili yako. Hujui ni muda gani mtu wako wa karibu anaweza kukubadilikia na kukufanyia mambo ya hiana.

Tamari anatendewa vibaya na nduguye Amnoni (2Sam:13:11-15). Samsoni anasalitiwa na mkewe (Waamuzi:16:15-20), Yusufu anauzwa na ndugu zake (Mwaz: 37:15-36). Na mifano mingine mingi. Lakini ninachotamani ujue ni kuwa kwa habari ya Yusufu Mungu aliinua mtu miongoni mwa ndugu zake aliyekuwa upande wake kumtetea ili asiuawe.

Wakati wanasemezana na kukubaliana kumuua Bwana alimwinua Reubeni na akawaambia ndugu zake haifai kumwaga damu yake bali mtupeni katika birika iliyoko nyikani wala msimguse, lakibi Biblia inatujulisha kuwa alikusudia kumuokoa mikononi mwao na kumrudisha kwa baba yao. Lakini wakati Reubeni amejitenga na ndugu zake, Yuda akashauriana na wenzake na wakakubaliana kumuuza kwa Waishmaeli na wakamchukua Yusufu hadi Misri.

Mpendwa, watoto hao walirudi kwa baba yao na visingizio vya kila aina, hadi ushahidi wa kanzu! Watoto wanafanya hivyo kwa baba yao bila huruma! Pasipo msaada wa Mungu mpendwa, hatupo salama!

Katikati ya wanaokusudia mabaya juu yako Mungu akuinulie mtu! Usibaki peke yako. Miongoni mwa watumishi wenzako, wachungaji wenzako, wazee wa kanisa wenzako, waimbaji wenzako, wafanyakazi wenzako, wanafunzi wenzako au, ndugu zako wa karibu wapo wanaowaza mabaya juu yako. Mungu ainue mmoja miongoni mwao awe upande wako wa kukutetea!

Tunaona pia habari za Mtume Petro na wenzake wakiwa katika kueneza ufalme wa Mungu wanakutana na changamoto ya kutokukubalika kwa sababu ya kufundisha kweli ya Kristo, kuponya na kuwafungua waliokuwa wamefungwa na ibilisi. Lakini pamoja na mambo mazuri waliyokuwa wanafanya bado Mafarisayo walikusudia kuwauwa. (Mdo:5: 26-42 ).

Mitume hawa wanawekwa mbele ya baraza, lakini bado wako imara kutangaza habari za ufalme wa Mungu. Mstari wa 33 unasema “Wao (mafarisayo) waliposikia wakachomwa mioyo yao; wakafanya shauri kuwaua”. Mpendwa wangu siyo kwamba wanaofanya mambo mabaya tu ndio wanaohukumiwa, hapana, wako wanaofanya mambo mazuri sana, lakini bado wanaangukia mikononi mwa watu wabaya. Watu wasiofurahishwa na yale mazuri unayoyafanya hawatakuacha salama.

Mstari wa 34 unasema: “Lakini mtu mmoja Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza akaamuru mitume wawekwe nje kitambo”. Mungu akitaka kukuinulia mtu ainue mtu wa kawida, Biblia inasema Gamalieli alikuwa mtu mwenye kuheshimiwa na kila mtu. Akisema nyamaza, unanyamanza! Akisema kaa chini, unakaa! Akisema ondoka, unaondoka. Kila mtu alimheshimu na kumtii. Mtu huyo ndiye ambaye Mungu anamuinua ili awatetee kina Petro.

Gamalieli akawakumbusha walichokifanya kwa Theuda na Yuda, akawaambia watu hawa ni wa tofauti siyo kama wale mliowazoea, hawa wana kitu cha tofauti ndani yao. Akawaonya na kuwaambia jiepusheni na watu hawa, waacheni kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa inatoka kwa binadamu itavunjika, lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapingana na Mungu.

Mpendwa Mungu akuinulie Gamalieli wako, atakayesimama upande wako na kuwaonya wote walio kinyume na wewe kwa sababu yule uliyembeba ni mkuu kuliko wanavyodhani. Iwapo walizoea kufanya hivyo kwa wengine, kwako haitakuwa katika Jina la Yesu.

Miongoni mwa wanaokusudia mabaya juu yako, Yesu akuinulie mtetezi, miongoni mwa wachawi wanaokuloga Yesu ainue mchawi mwenye nguvu zaidi yao na awaambie kwa habari ya mtu huyu nawaonya msijaribu kumgusa yeye wala familia yake, kwa sababu atakayemgusa tu amekwisha!

Ni maombi yangu kwako, kuwa Mungu wangu hatakuacha, atakuandalia mtetezi katika nyakati ngumu unazopitia. Kikubwa nakusihi usimuache huyo Yesu uliyembeba. Uwe na moyo mkuu, uwe na imani thabiti. Mungu wangu atakuwa upande wako. Amina.