MAHUBIRI: Hitaji muhimu ni kumpa Mungu nafasi ya kwanza

Bwana Yesu asifiwe… Wakati fulani nimewahi kufundisha somo linaloitwa “Vipaumbele vya Mwamini.” Katika somo hilo nilipewa msukumo wa kuonesha jinsi ambavyo kuna mambo yanatakiwa kupewa nafasi ya kwanza kabla ya mengine katika maisha ya mwanadamu.

Watu wengi wamefanya kosa la kufanya mambo ya kwanza kuwa ya pili na ya pili kuwa ya kwanza katika maisha yao. Katika somo la leo nataka nikutie moyo ndugu msomaji wangu kuhusu kumpa Mungu nafasi ya kwanza kwenye maisha yako.

Mtu mmoja aliwahi kusema: “Unaweza kupata vitu na kumkosa Mungu, lakini kama ukimpata Mungu vitu vitakuja.” Ni maneno mazito sana haya. Yesu anasema, “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa” Mathayo 6:33. Hii ni hesabu bora sana ya Kiungu. Ukiutafuta kwanza Ufalme wa Mungu, mengine atakuzidishia mwenyewe.

Pia Neno la Mungu linasema, “Mtakeni Bwana na nguvu zake, Utafuteni uso wake siku zote” (Zaburi 105:4). Kupitia Andiko hili tunajifunza kuhusu kumtaka Bwana, kuzitaka nguvu zake, na kuutafuta uso wake (uwepo wake).

Kabla ya kutaka jambo lolote katika maisha yetu, Mungu anataka kwanza tumtake Yeye na kwa kufanya hivyo mambo mengine yatakuja kama matokeo ya kuwa na Mungu kwenye maisha yetu. Nimeshawaona watu wengi wanaotaka kumtumikia Mungu, lakini hawataki kujiunganisha na chanzo (Mungu) anayeweza kuwapa nguvu zake ili wamtumikie.

Pia, katika ulimwengu wa sasa watu wengi wanajivunia zaidi mambo ya kimwili na kutumia nguvu kubwa kuyafukuzia hayo, huku wamemuacha Mungu nyuma. Mambo hayatakiwi kuwa hivi, maana Neno linasema, “Ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni Bwana” (Yeremia 9:24).

Kama kuna jambo la thamani unaweza kufanya leo, basi ni kumchagua Mungu kuwa wa kwanza kwenye maisha yako na kama utajisifu basi ujisifu kwa kuwa umemjua Yeye. Sisemi kwamba hatuhitaji kuwa na vitu, la hasha! Lakini kuwa kwetu na vitu hakutakiwi kupoteza nafasi ya Mungu kwenye maisha yetu.

Ni muhimu pia kufahamu kwamba, unapochagua kuwa na mahusiano na Mungu lazima ukubali kujikana na kuacha vyote. Haiwezekani kuwa na Mungu na wakati huohuo ukaipenda dunia. Neno la Mungu linasema, “Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake” (1 Yoh. 2:15). Ndiyo maana Yesu anasema, “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate” (Luka 9:23). Kumbe ili Mungu apate nafasi ya kwanza kwenye maisha ya mwanadamu ni lazima kujikana na kutokubali kuzuiliwa na dunia kumpenda Mungu. Mungu anataka tumpende kwelikweli pasipo kujibakisha hata kidogo (Mathayo 22:37). Inahitaji maamuzi ya kila siku ili kuendelea kuwa na mahusiano na Mungu.

Katika hali ya kawaida, mtu ambaye amekupa nafasi ya kwanza kwenye maisha yake atajitoa kwa ajili yako. Atakuwa na muda na wewe, atakuwa mwenye kuwasiliana na wewe, atakujali na kuhakikisha unakuwa na furaha.

Hebu fikiria wanandoa wanaodai wanapendana lakini hawana muda wa kuwa pamoja (kila mtu yuko na mambo yake), hawawasiliani wala hakuna anayemjali mwenzake, kuna mahusiano hapo kweli? Jibu ni hapana.

Tunaposema kuhusu kumpa Mungu nafasi ya kwanza inahusisha kumpa muda wa kutosha na kila kitu kinachohusu maisha yetu yote. Unaweza kuuliza kumpa muda wa kutosha ndiyo nini hasa? Hii inahusisha kuwa na muda wa maombi, kusoma na kujifunza Neno lake, kuwa na muda wa ibada binafsi na za kukusanyika na wengine. Pia inahusisha kumtolea na kujitoa kumtumikia Yeye kwa vipawa na karama mbalimbali alizowekeza ndani yako. Yaani ni kujitoa mzima mzima (total surrender).

Kabla sijampokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yangu, nakumbuka nilikuwa nikitoa muda wangu na vipawa nilivyopewa na Mungu kwenye mambo yasiyo na maana.

Wakati fulani nilikuwa nimeanza kukitumia kipawa cha uimbaji kuimba nyimbo zisizo za kumtukuza Mungu na kwenda kwenye maeneo ya disco ambako nilishindana kucheza muziki ili nipate sifa na wakati mwingine nipewe fedha.

Nilipoamua kuyatoa maisha yangu kwa Mungu, mambo yalibadilika. Nilisalimu amri kila ambacho Mungu ameweka ndani yangu kwa ajili ya kumtumikia Yeye na kwa ajili ya kuujenga Ufalme wa Mungu. Ukimfanya Mungu kuwa wa kwanza kwenye maisha yako, basi utayatoa maisha yako yote kwa ajili ya kulitimiza kusudi la Mungu na kwa ajili ya utukufu wake.