Mahitaji mkojo wa sungura yaongezeka, lita yauzwa Sh19,000

Nairobi. Mahitaji ya mkojo wa sungura yameongezeka kwa kasi huku lita moja ikiuzwa kwa KSh1,000 (Sh19,885) hali inayowavutia wakulima zaidi kuwekeza katika ufugaji wa wanyama hao. 

Mbali na nyama ya sungura kuuzwa kwa kati ya KSh1,000 (Sh19,885 na KSh2,000 (Sh39,790) kwa kilo, wakulima sasa wanapata faida kutokana na mkojo wa mnyama huyo, ambao hutumika kama mbolea ya asili na dawa ya kuua wadudu wanaoshambulia mimea. 

Uvunaji wa mkojo wa sungura. Picha na Mtandao

Kwa sasa, nusu lita ya mkojo wa sungura huuzwa kwa zaidi ya KSh500 (Sh9,947) hali inayoufanya kuwa bidhaa yenye faida kubwa kwa wafugaji. 

Hata hivyo, licha ya mahitaji kuongezeka, changamoto ya upatikanaji wanyama hao kwa ajili ya kuchinjwa bado ni kubwa. Chama cha Wafugaji wa Sungura nchini (RABAK) kinasema kuwa uhaba wa sungura umesababisha machinjio kufanya kazi mara moja kwa wiki. 

Mwenyekiti wa RABAK, Peter Waiganjo amesema kuwa machinjio kwa wiki mara moja ambayo ni kila Jumatano na huchinja sungura 200 kiwango ambacho ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji ya soko. 

Mabanda ya sungura. Picha na mtandao

“Mahitaji ya nyama ya sungura yameongezeka kwa miaka mingi hadi kiwango ambacho wafanyabiashara hawawezi kukidhi,” amesema Waiganjo. 

Kutokana na hali hiyo, wakulima wametakiwa kuchangamkia fursa ya ufugaji wa sungura ili kunufaika na mauzo ya nyama na mkojo wake. 

Wadau wa sekta hiyo, wamezitaka serikali za kaunti kuweka mikakati ya kusambaza sungura kwa wakulima bila malipo kama motisha ya kuongeza uzalishaji na kukidhi mahitaji ya soko. 

Kwa mujibu wa RABAK, uwekezaji zaidi katika sekta ya sungura unaweza kusaidia kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa kilimo biashara nchini Kenya.

Mkojo wa sungura ukiwa kwenye chupa tayari kuuzwa. Picha na Mtandao

Nyama ya sungura inatajwa kuwa faida nyingi mwilini ikiwemo kiwango kidogo cha mafuta ukilinganisha na nyama nyekundu kama ya ng’ombe au mbuzi na husaidia kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.

Wataalamu wanashauri wagonjwa wa kisukari na shinikizo la damu kula nyama hiyo kwa sababu ya kuwa na mafuta machache na cholesterol ya chini.