Mahdi afichua siri Kiluvya United

KOCHA wa Kiluvya United, Zulkifri Iddi ‘Mahdi’ amesema moja ya malengo ya timu hiyo kwa sasa ni kuendelea kusalia msimu ujao wa Ligi ya Championship, baada ya kuona nafasi waliyopo ni finyu ya kupigania nafasi nne za juu kama walivyotaka.

Akizungumza na Mwanaspoti, ‘Mahdi’ alisema kwa sasa hawana njia nyingine ya kuipigania timu hiyo zaidi ya kuinusuru na janga la kushuka daraja, hivyo ameweka mikakati mipya ya kuhakikisha wanatimiza hilo kwa kupata matokeo chanya nyumbani.

“Kiukweli mwelekeo wetu ni mgumu lakini lazima tupambane hadi mwisho, hali ya timu siyo nzuri ila mashabiki waendelee tu kutupatia sapoti na sisi benchi la ufundi tunawaahidi tutapambana bila ya kuchoka ili kuinusuru tu isishuke,” alisema.

Kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Biashara United, timu hiyo iliyopanda Ligi ya Championship msimu huu, imeshinda michezo miwili, sare mmoja na kupoteza 13, ikifunga mabao tisa na kuruhusu 25, ikiwa nafasi ya 15 kwenye msimamo na pointi saba.

‘Mahdi’ aliyewahi kufundisha timu mbalimbali zikiwemo za Namungo FC, Cosmopolitan na Singida United, amejiunga na kikosi hicho akichukua nafasi ya Twaha Beimbaya aliyeanza nacho msimu, kisha kutimuliwa kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo.