
Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Janeth Mahawanga ameihoji Serikali ina mpango gani wa kuanzisha madarasa ya Elimu kwa Mlipa Kodi kupitia vikundi vya wanawake wajasiriamali.
Mbunge huyo amesema kutoa elimu kupitia makundi ya wanawake itasaidia elimu ya mlipakodi kuwafikia wahusika moja kwa moja na kutasaidia walipa kodi kutambua wajibu wao.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikitoa elimu ya kodi kwa njia mbalimbali kwa makundi yote ya walipakodi na vikundi vya wanawake wajasiriamali.
Naibu Waziri amesema, TRA imekuwa ikielimisha wanawake wajasiriamali kupitia vikundi vyao ikiwemo chemba ya wafanyabiashara wanawake “Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC)” na makundi mengine ya wajasiriamali wanawake.
Amesema katika kuhakikisha uendelevu katika kuwafikia wajasiriamali wanawake, TRA itaendelea kushirikiana kikamilifu na wizara husika kuimarisha mawasiliano na mtandao wa wanawake wajasiriamali ili kupitia taasisi au jumuiya zao tuweze kukidhi mahitaji ya elimu ya kodi na shughuli zao za kiuchumi.