
Lushoto. Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Katarina Mteule amewasihi Mahakimu wakazi kutenda kazi zao kwa weledi, uwazi, haki na uadilifu ili uamuzi wao mahakamani uheshimiwe na wananchi wanaokwenda kwao kutafuta haki.
Jaji Katarina amezungumza hayo jana Jumatatu, Septemba 23, 2024 wakati akifungua mafunzo elekezi kwa Mahakimu wakazi 28 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) mkoani Tanga kwa niaba ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapher Siyani.
“Ni lazima tuwe na uwazi, weledi na uadilifu katika utendaji wetu wa kazi ili wananchi waweze kutuamini na kuheshimu maamuzi yetu. Wananchi watajenga imani na sisi na maamuzi yetu pale tu tutakapotenda haki kwa wakati na ambayo itaonekana kutendeka,” amesema Katarina.
Vilevile Jaji Katarina amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambao Mahakama inaimarisha mifumo ya utoaji haki, hivyo kuwasihi kutoa haki kwa wakati, kwa ufanisi na bila kujali hali ya mtu.
Aidha, Katarina amewadokeza washiriki hao kuwa katika utendaji wao wa kazi watarajie kukosolewa na kupongezwa, huku akiwakumbusha hotuba ya Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma aliyewahi kusema kuwa, kazi yao ni ya umma, hivyo hawapaswi kupiga kelele wanapokosolewa.
Mafunzo hayo yatakayofanyika mpaka Oktoba 4, 2024 yameandaliwa na kuendeshwa na IJA kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania na yanalenga kuwaandaa na kuwapatia ujuzi na maarifa muhimu yatakayowaongoza katika utendaji wao.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Eva Nkya amewasisitiza washiriki hao kwenda kuonesha utendaji wao kwa viwango vya juu na wazingatie maadili ya kazi yao.
Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama na Elimu Endelevu wa IJA ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mkuu, Dk Patricia Kisinda amewasihi washiriki kwenda kufanyia kazi mafunzo hayo ili iwe nyenzo muhimu ya utoaji haki.
Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo ni Hakimu Mkazi, Zuhura Hamza ambaye ametaja matarajio yake baada ya mafunzo hayo ni kwenda kutekeleza kazi yake kwa uadilifu na weledi ili kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama.
“Matarajio yangu ni kutenda kazi yangu kwa uadilifu, uweledi na uwajibikaji ili kuweza kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama, tufahamu hii kazi ni ya kijamii zaidi, hivyo tunapaswa kuitumikia jamii hiyo kwa haki na uadilifu mkubwa,” amesema Zuhura.
Hakimu Mkazi James Kapele amesifu mafunzo hayo kwa jinsi yalivyoandaliwa na kwamba ana imani atatoka akiwa ameiva na kwenda kutekeleza vema jukumu la kimsingi la utoaji haki.