Mahakama za mwanzo Geita kuendeshwa kidijitali

Geita. Ili kupunguza gharama za uendeshaji na kutunza kumbukumbu Mahakama zote za mwanzo mkoani Geita zinatarajia kuanza rasmi kutumia mfumo wa Tehama) ifikapo Machi mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Geita,  Kelvin Mhina wakati wa ufunguzi wa wiki ya Sheria iliyofanyika katika viwanja vya EPZ Mjini Geita.

Amesema kufanya kazi kidijitali kutasaidia utunzaji wa kumbukumbu, kutapunguza gharama za uendeshaji, kurahisisha usikilizaji  na kutoa hukumu kwa wakati.

Akizungumzia mwaka mmoja wa uwepo wa Mahakama Kuu Geita, Jaji Mhina amesema tangu kuanza kwa mahakama hiyo  mwaka mmoja uliopita kesi 282 zilisajiliwa na kati ya hizo 261 zilimalizika.

Amesema mkoa huo wenye matukio mengi ya mauaji yaliyoripotiwa mahakamani chanzo ni imani za kishirikina na migogoro ya ardhi.

Kwa upande wake wakili kutoka Ofisi ya mwendesha Mashtaka wa Serikali mkoa wa Geita, Godfrey Odupoy amesema moja ya changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu ya kisheria ni mashahidi wa kesi za ukatili wa kijinsia kutojitokeza mahakamani.

Amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo, ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Geita imeanza kusikiliza ushahidi wa muathirika na wazazi wake, pindi kesi hiyo inapofikishwa  mahakamani ili kuondoa mwanya wa kumalizana kifamilia.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigella akizindua wiki ya amesema Mahakama ni eneo pekee ambalo mtu anapata haki hivyo kukitaka chombo hicho cha kisheria kutenda haki.

Hata hivyo, amewataka wananchi kutumia fursa ya wiki ya kisheria kutembelea viwanja vya EPZ ili kukutana na wanasheria ambao watawashauri masuala ya kisheria juu ya changamoto walizonazo.