
Arusha. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Masjala Ndogo ya Arusha, imetoa amri ya kutokutajwa majina ya mashahidi wala maelezo yao yanayoweza kuwatambulisha katika kesi ya ugaidi inayowakabili watuhumiwa tisa.
Watuhumiwa hao ni Zuberi Ngale, Abdul Seif, Jumaa Athumani, Juma Swalehe, Wally Aman, Said Abdallah, Jaluu Ismail na Yusuph Tambala.
Kutokana na sababu za kiusalama, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), amewasilisha ombi la kusikilizwa upande mmoja akiiomba Mahakama itoe amri ya kuzuia kutaja utambulisho wa mashahidi na mahali walipo.
Maombi hayo namba 6490 ya mwaka 2025, dhidi ya watuhumiwa hao tisa, yalisikilizwa na kutolewa uamuzi huo jana Machi 24, 2025 na Jaji Sedekia Kisanya na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
DPP aliwasilisha maombi hayo ya awali chini ya kifungu cha 34(3) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi na kifungu cha 188 (1) na (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), akiomba mashahidi watakaotoa ushahidi wao katika kesi ya jinai itakapopangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, itoe zuio hilo.
Pia, ameomba mashahidi waruhusiwe kutoa ushahidi kwa njia ya video, kutowekwa wazi utambulisho na nyaraka zinazoweza kuwatambulisha mashahidi wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo kwa lengo la usalama wao katika usikilizwaji wa awali na usikilizwaji kamili wa kesi hiyo ya jinai.
Aidha, DPP ameomba Mahakama itoe amri ya kusikilizwa faragha mwenendo wa kesi hiyo na hatua nyingine ambazo Mahakama itaona ni muhimu ili kuhakikisha usalama wa mashahidi hao.
Ombi hilo liliambatanishwa viapo viwili ikiwemo cha Wakili wa Serikali Mwandamizi, James Pallangyo.
Katika hoja za DPP zilizowasilishwa na Wakili Pallangyo, ameeleza kuwa wajibu maombi hao tisa wanakabiliwa na mashtaka mengi chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi na kuwa uchunguzi umebaini juhudi zinazoendelea kufanywa na baadhi ya wapambe wa wajibu maombi ambao bado hawajafahamika, wanawatisha mashahidi wa mashtaka ili kuwazuia kutoa ushahidi wao.
Kutokana na vitisho hivyo, Wakili Pallangyo ameitaka Mahakama hii kuridhia ombi hilo na hatua za kiulinzi kuchukuliwa akitolea mfano kesi ya DPP dhidi ya Yusuph Ally Huta na wengine watano, katika maombi namba 26/2022 ambapo hatua sawa za ulinzi wa mashahidi zilitolewa.
Uamuzi wa Jaji
Katika uamuzi huo Jaji Kisanya, amesema ni jukumu la Mahakama kupima kama ombi la DPP lina mashiko au la.
Amesema chini ya kifungu cha 188 (1) cha CPA, Mahakama inaweza kutoa hatua za ulinzi, ikiwa ni pamoja na kuruhusu ushahidi wa mashahidi kutolewa kwa njia ya video, kuamuru kutowekwa utambulisho wa shahidi na mahali alipo kwa sababu za kiusalama.
“Aidha kifungu cha 188(2) cha CPA kinaeleza kuwa mara baada ya amri hizo kutolewa, maelezo au nyaraka za mashahidi husika hazitatolewa kwa mshtakiwa wakati wa usikilizwaji.
Jaji Kisanya amesema katika kuamua uhalali wa ombi hili, Mahakama lazima itathmini ikiwa usalama wa mashahidi waliokusudiwa ungekuwa hatarini ikiwa utambulisho wao utafichuliwa.
Jaji Kisanya amesema kuwa taarifa za kiintelijensia zilizokusanywa wakati wa upelelezi zinaonyesha kuwa washtakiwa hao kwa kushirikiana na wapambe wao wamekuwa wakifanya jitihada za kubaini utambulisho wa mashahidi wa upande wa mashtaka kwa nia yakuwazuia kutoa ushahidi.
“Kutokana na mazingira hayo, naungana na Wakili Pallangyo kwamba usalama na ustawi wa mashahidi waliokusudiwa na familia zao utakuwa katika hatari kubwa endapo utambulisho wao utafichuliwa wakati wa usikilizwaji wa kesi, kwa hiyo hatua za kiulinzi zitafuatwa katika usikilizaji wa awali na usikilizaji wa kesi ili kuhakikisha usalama wa mashahidi,” amesema Jaji huyo.
Jaji Kisanya amesema kwa kuzingatia kifungu cha 188 (1) na (2) cha CPA, Mahakama inaamuru kuwa inapobidi baadhi ya mashahidi watatoa ushahidi wao kwa njia ya mtandao, kutotolewa utambulisho na mahali walipo mashahidi kutofichuliwa na usikilizwaji kufanyika faragha.