Mahakama yatupilia mbali pingamizi la Kanisa, yaruhusu Askofu Mokiwa kutoa ushahidi

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi imeruhusu aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Valentino Mokiwa na wenzake wanne waliokuwa wamewekewa pingamizi, kutoa ushahidi katika kesi ya ardhi iliyofunguliwa na Bernardo Sepeku dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania na Askofu Jackson Sostenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne, Septemba 24, 2024 na Jaji wa Mahakama hiyo, Arafa Msafiri baada ya kutupilia mbali pingamizi lililowekwa na Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania na Askofu Jackson Sostenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam la kupinga mashahidi hao wasitoe ushahidi kutokana na viapo vyao kuwa na kasoro za kisheria.

Bernado, ambaye ni mtoto wa marehemu John Sepeku aliyekuwa Askofu Mkuu wa kwanza wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Dar es Salaam, alifungua kesi hiyo ya ardhi namba 378/2023, akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978 na kanisa hilo.

Mtoto huyo alifungua kesi dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa Anglikana Tanzania, Askofu Jackson Sostenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam na pamoja na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.

Katika kesi hiyo, Bernardo anadai alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi katika kiwanja hicho.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Msafiri alisema mapingamizi yaliyowasilishwa na bodi hiyo pamoja na Askofu Sostenes hayana mashiko kwa kuwa yaliwasilishwa kabla muda ya kutolewa kwa ushahidi.

Jaji Msafiri amesema wakili Dennis Malamba anayetetea Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana  Tanzania na Askofu Jackson Sostenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam, aliwasilisha pingamizi lake kabla ya upande wa wadai kuanza kutoa ushahidi, hivyo pingamizi lake kuonekana halijakomaa.

Jaji Msafari amesema anatupilia mbali pingamizi hilo na kuruhusu mashahahidi hao kutoa ushahidi.

Endelea kufuatilia mitandao ya kijamii