
Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imeelekeza rufaa dhidi ya Kocha Liston Katabazi aliyoikata dhidi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), akipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam, inayoketi Kisutu, isikilizwe kwa njia ya maandishi.
Rufaa hiyo ilikuwa imepangwa kusikilizwa na Jaji Phillip Butamo kwa mdomo juzi Alhamisi, Machi 20, 2025. Hata hivyo, Jaji Butamo alielekeza rufaa hiyo isikilizwe kwa njia ya maandishi.
Hivyo alielekeza mrufani, Katabazi anayewakilishwa na mawakili Peter Majanjara na Melchzedeck Joachim kuwasilisha hoja zao za maandishi Aprili 2, 2025, na wajibu rufani kuwasilisha majibu yao ya hoja za mrufani, Aprili 16, 2025.
Pia alielekeza kama mrufani atakuwa na majibu ya nyongeza dhidi ya majibu ya wajibu rufani yawasilishwe mahakamani Aprili 22, na rufaa hiyo itatajwa Aprili 23, 2025, saa 2:30 asubuhi kwa ajili ya kupanga tarehe ya hukumu.
Awali Katabazi ambaye anajitambulisha ni mwanamichezo na mdau wa mchezo wa soka na kocha wa mpira wa miguu mwenye leseni ya daraja C, iliyotolewa na TFF, alifungua kesi ya madai dhidi ya TFF na wadhamini wake.
Katika kesi hiyo ya madai namba 14708 ya mwaka 2024, alikuwa akipinga uamuzi wa TFF kumfungia maisha kujishusha na shughuli za soka.
Pamoja na mambo mengine alidai Kamati ya Maadili ya TFF haikuwa na mamlaka ya kutoa uamuzi huo dhidi yake kwa kuwa Kanuni za Maadili za TFF, Toleo la Mwaka 2021, zilizotumika kumfungia si halali.
Alidai kanuni hizo hazijasajiliwa na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kwa mujibu wa matakwa ya Sheria namba 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake na hivyo kuzifanya kuwa batili kutumika dhidi ya wanachama wake na mtu mwingine yeyote.
Katabazi alidai amri hiyo iliingilia haki yake ya kufanya kazi katika nyanja ya soka na hivyo kumkosesha fursa ya kupata mshahara na kipato kwa ajili ya kuendeleza maisha yake ya kila siku na familia yake na kumsababishia maumivu ya kisaikolojia.
Hivyo, aliiomba mahakama iiamuru TFF imlipe Sh600 milioni kama fidia ya madhara ya jumla aliyoyapata kutokana na uamuzi huo wa kumfungia maisha uliotolewa kwa makusudi, kimakosa na kwa nia ovu.
Pia aliomba alipwe Sh100 milioni kama fidia ya adhabu kwa kitendo cha wadaiwa kutoa na kuchapisha zuio la maisha katika soka wakijua hawana mamlaka ya kisheria kuchukua hatua hiyo dhidi ya mdai.
Katabazi pia aliiomba mahakama itoe zuio la matumizi ya Sheria (Katiba) na Kanuni za Maadili za TFF, kwa madai si vyombo halali kwa kutokusajiliwa kwa utaratibu na unaofaa.
Vilevile aliomba fidia ya madhara mengineyo kadiri mahakama itakavyotathmini, riba kwa tozo ambayo angepewa kwa kiwango cha mahakama kuanzia tarehe ya kufungua kesi mpaka tarehe ya hukumu na kuanzia tarehe ya hukumu mpaka tarehe ya kukamilisha malipo yote na gharama za kesi.
Hata hivyo, Mahakama ya Kisutu iliitupilia mbali kesi hiyo bila kusikiliza madai ya msingi, kutokana na pingamizi la awali lililoibuliwa na TFF.
Katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga ilikubaliana na sababu ya pingamizi la TFF kuwa haikuwa na mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo.
Hakimu Kiswaga alisema hakuna ubishi Katabazi ni mwanachama wa TFF, huku akikubaliana na wakili wa TFF, Rahim Shaban, TFF ina Sheria yake inayoitwa Katiba ya TFF ambayo inawafunga wanachama wake wote.
Pia alisema kwa mujibu wa Katiba hiyo ya TFF, mwanachama asiyeridhika na uamuzi wa Kamati ya Maadili anapaswa kukata rufaa katika Kamati ya Rufaa ya Maadili lakini yeye Katabazi hakufuata utaratibu, badala yake aliamua kufungua kesi hiyo mahakamani hapo.
Hakimu Kiswaga aliongeza, kwa Katiba ya TFF, shirikisho hilo litakuwa na mamlaka ya migogoro yote ya ndani ya soka.
Aliongeza mwanachama anaweza kupeleka shauri lake katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) baada ya kumaliza hatua zote ndani ya TFF, ambayo ndiyo itakuwa na uamuzi wa mwisho nje ya mahakama za kawaida.
Hivyo alisema kwa maelezo hayo, mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwani mlalamikaji, Katabazi alipaswa kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya Maadili na kama asingeridhika angekata rufaa CAS kama Katiba ya TFF inavyoelekeza.
Kwa sababu hizo, alisema anakubaliana na hoja ya pingamizi la awali na hivyo akafuta kesi hiyo.
Katabazi ambaye anadai kuwa si mwanchama wa TFF kama Mahakama ya Kisutu ilivyosema, licha ya kuwasilisha mahakamani barua ya BMT ya Juni 13, 2022, iliyothibitisha yeye si mwanachama wa TFF, hakukubaliana na uamuzi huo wa Mahakama ya Kisutu.
Hivyo alikata rufaa hii Mahakama Kuu kuupinga, akiwasilisha sababu nne, ambazo pamoja na nyingine anadai Mahakama ya Kisutu ilikosea kisheria kushughulikia pingamizi la wajibu rufani ambalo halikuwa na msingi wa kisheria na kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa wakati wa usikilizwaji wa pingamizi.
Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo, Katabazi alifungiwa na TFF kujishughulisha na masuala ya soka kwa maisha yake yote ndani na nje ya nchi, baada kuliandikia barua BMT akilishtaki TFF.
Katika barua hiyo ya Juni 15, 2021, Katabazi aliituhumu menejimenti ya shirikisho hilo kushindwa kusimamia mchezo wa soka kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo mingine ya shirikisho hilo.
Kutokana na barua hiyo, aliitwa katika Kamati ya Maadili, lakini hakuhudhuria badala yake alijibu yeye si mwanachama wa Chama cha Makocha Tanzania (TAFCA) ambacho kiko chini ya usimamizi wa TFF, hivyo yeye si mwanachama wa TFF.
Juni 24, 2021, TFF lilichapisha katika tovuti yao uamuzi wa kumfungia Katabazi maisha kujishughulisha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi, ndipo baadaye mwaka 2024 akafungua kesi hiyo mahakamani kupinga uamuzi huo wa TFF.