Mahakama yatoa maagizo kesi ya Boni Yai, nyingine yakwama

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeitaka Serikali kukamilisha upelelezi kwa wakati, kesi ya kusambaza taarifa za uongo inayomkabili Meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo, Boniface Jacob maarufu Boni Yai pekee yake.

Jacob ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, anakabiliwa na mashtaka mawili ya kuchapishaji taarifa za uwongo kwenye mtandao wake wa X (zamani Twitter) katika Mahakama mahakama hiyo.

Kesi hiyo ilipangwa leo Jumatano Februari 12, 2025 kwa ajili ya kutajwa na kuangaliwa iwapo upande wa mashtaka umekamilisha upelelezi au laa, lakini Wakili wa Serikali, Cathbert Mbilingi aliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea.

Wakili Mbilingi alitoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Geofrey Mhini.

“Mheshimiwa hakimu, kesi hii imeletwa mbele yako kwa ajili ya kutajwa na hakimu anayesikiliza kesi hii, Franco Kiswaga, ana majukumu mengine ya kikazi, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” alidai Wakili Mbilingi.

Mbilingi baada ya kueleza hayo, wakili wa utetezi Peter Kibatala amedai ana mambo mawili ya kuzungumza, moja ni kwamba upande wa mashtaka hauko makini na suala ya upelele.

“Mheshimiwa hakimu, wenzetu wa upande wa mashtaka hawapo serious (makini) kukamilisha upelelezi wa kesi hii, na tulipambana sana hadi mteja wetu akapata dhamana, sasa je mshtakiwa angekuwa hajapata dhamana angekuwa mpaka sasa yupo ndani,” ameidai Kibatala na kuongeza.

“Suala la hakimu kuwa na majukumu mengine ya kikazi hilo halina tatizo, sisi tunaomba upande wa mashtaka wajitahidi kukamilisha upelelezi wao kwa wakati,” amedai Kibatala.

Mshtakiwa Boniface Jacob ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani (katikati) akiwa na mshtakiwa mwenzake, Godlisten Malisa (kulia) na kushoto ni wakili wao, Hekima Mwasipu. Picha na Maktaba

Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili, alielekeza upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo kwa haraka ili iweze kuendelea na hatua nyingine.

Baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 11, 2025 kwa kutajwa na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Boni Yai anakabiliwa na mashtaka mawili, ya kuchapisha taarifa za uwongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandano namba 14 ya mwaka 2015.

Katika shtaka la kwanza, Boni anadaiwa Septemba 12 2024 jijini Dar alichapisha taarifa za uwongo zikimhusisha Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) ya Dar Es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP).

Taarifa hizo zinasomeka kuwa:

“Mafwele anatuhumiwa na familia nyingi kama mtu ambaye ameshiriki mauaji kwa moja katika kuwapoteza ndugu wa baadhi ya familia zao, kupotea kwa mfanyabiashara Mussa Mziba, kupotea kwa Deo Mugasa, kupotea kwa Adinani Hussein Mbezi, kupotea kwa vijana watano wa Aggrey.”

Katika shtaka la pili, mshtakiwa anadaiwa Septemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam alidaiwa kuchapisha taarifa za uwongo kuwa zinazowahusisha wakuu wa upelelezi wa mikoa na utekaji na mauaji ya watu na kutupa miili yao.

Ujumbe huo inasomeka kuwa:

“Mkawasifia Ma-RCO (Wakuu wa Upelelezi Mikoa) wanaozuia uhalifu kwa kutenda uhalifu …, bali Ma-RCO waliokuwa kuteka, kukamata, kupiga watuhumiwa risasi, kuwafunga tape, kuwafunga mifuko ya nailoni usoni na kisha kutupa miili ya watuhumiwa ndio wanaijua kazi ya upolisi.”

Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Septemba 19, 2024 kujibu mashtaka yanayomkabili.

Kesi ya msingi:

Washtakiwa hao wameshtakiwa makosa yao, chini ya kifungu cha 16 cha sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Jacob anadaiwa kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kinyume na kifungu cha 16 cha sheria ya mtandao.

Jacob anadaiwa kutenda kosa hilo April 22, 2024 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa lengo la kupotosha umma, mshtakiwa alichapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wa kijamii wa X (Twitter) wenye jina la Boniface Jocob@ExMayor Ubungo.

Shtaka la pili ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kwa lengo la kuipotosha jamii linalomkabili Jacob pekee yake.

Mshtakiwa hiyo anadaiwa kutenda kosa hilo Machi 19, 2024 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo mshtakiwa  alichapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa kijamii X ( Twitter) wenye jina la Boniface Jacob @ExMayor Ubungo kwa kuandika  kama ifuatavyo.

“MAUAJI ARUSHA, Mwananchi mwenzetu na aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, Omari Msamo ameuawa na askari wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

Shtaka la tatu ni kutoa taarifa za uongo, linalomkabili Malisa pekee yake, ambapo mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2024 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Malisa anadaiwa siku hiyo ya tukio, kwa nia ovu na kwa lengo la kuupotosha umma na jamii, alichapisha taarifa ya uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa Kijamii wa Instagram wenye jina la Malisa_gj, kwa kuandika ujumbe uliosomeka” tarehe 13 Aprili meya mstaafu wa Manispaa ya Ubungo @Exmyor_bonifacejacob alitoa taarifa ya kupotelewa na ndugu yake Bw. Robert Mushi maarufu kama Babu G, ambaye alipotea mwezi Aprili 2024.

Wakati huo huo, kesi ya kusambaza taarifa za uongo inayomkabili Meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo, Boniface Jacob pekee yake, itatajwa katika mahakama hiyo.

Mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka mawili ya kuchapishaji taarifa za uwongo kwenye mtandao wake wa X (zamani Twitter).

Kesi hiyo ya jinai inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Boni Yai anakabiliwa na mashtaka mawili, ya kuchapisha taarifa za uwongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya kimtandano namba 14 ya mwaka 2015.

Katika shtaka la kwanza, Boni anadaiwa Septemba 12, 2024 jijini Dar alichapisha taarifa za uwongo zikimhusisha Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP).