Mahakama yatoa hati kumkamata Batweli aliyeruka dhamana

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu imetoa hati ya kumkamata mshtakiwa Ibrahim Batweli (21) baada ya kushindwa kufika mahakamani, bila kutoa taarifa.

Pia mahakama hiyo imetoa hati kwa wadhamini wa mshtakiwa huyo kufika mahakamani hapo kujieleza sababu ya kushindwa kumfikisha mshtakiwa mahakamani hapo.

Batweli ambaye ni mshtakiwa wa tatu  katika kesi ya kusafirisha vipande vinane vya meno ya tembo, ameshindwa kufika mahakamani hapo wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya  kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi wa upande mashitaka.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano, Aprili 9, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu baada ya mshtakiwa kushindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi yake bila kutoa taarifa.

Kabla ya kutoa uamuzi huo, wakili wa Serikali, Mosia Kaima akishirikiana na Winiwa Kasala amedai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji lakini mshtakiwa na wadhamini wake hawapo mahakamani hapo.

“Mheshimiwa hakimu hatuna taarifa za mshtakiwa yuko wapi wala mdhamini wake, na leo tuna shahidi ambaye anatakiwa kutoa ushahidi wake, hivyo kutokana na mshtakiwa huyu kushindwa kufika mahakamani bila kutoa taarifa tunaomba mahakama itoe hati ya kumkamata a kwa kuruka dhamana,” amedai Kaima na kuongeza.

“Na pia, tunaomba tarehe ijayo, mshtakiwa wa tatu, aje na uthibitisho wa kuonyesha kweli alikuwa mgonjwa maana isije kuwa ni taarifa za kutengezwa,” alisema wakili Mosia.

Wakili Mosia baada ya kueleza hayo, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo,  Stanley Michael alidai kuwa juzi Aprili 7, 2025 wakiwa katika Kituo Kikuu cha Mabasi wakitokea Morogoro mwenzake, Ibrahim Batweli alianza kuumwa ndio sababu ya kushindwa kufika mahakamani.

Hakimu Magutu aliikataa taarifa hiyo akisema haikuwa rasmi kwani haikufuata taratibu za mahakama.

“Hii ni mara ya pili mshtakiwa huyu hafiki mahakamani akidai anaumwa, kwani Aprili 8, 2025 tuliambiwa anaumwa na leo Aprili 9, 2025 hajafika mahakamani, lakini hakuna taarifa rasmi kutoka kwa wadhamini au mwakilishi wake, tutajuaje kama anatudanganya,” amehoji hakimu Magutu.

Hakimu Magutu, baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashitaka, alisema mahakama yake inatoa hati ya kumkamata mshtakiwa kwa sababu ameshindwa kufika mahakama bila kutoa taarifa.

Baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 22, 2025 itakapoendelea na usikilizwaji.

Mbali na Batweli, washtakiwa wengine ni Sadock Nathan (34) ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo na Stanley Michael (42).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *