
Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan atazindua jengo la makao makuu ya Mahakama ya Tanzania, lililojengwa kwa mithili ya nyota huku likiwa na eneo la kutua helikopta.
Mbali na hilo, baada ya kujengwa kwa vituo jumuishi, majengo yaliyokuwa yakitumika kwa shughuli za mahakama sasa yatatumika kwa mahakama zinazoshughulika na kesi za familia, kama vile migogoro ya ndoa na mirathi, ambayo imekuwa changamoto kubwa.
Jengo hilo, ambalo atalizindua Aprili 5, 2025, litakuwa la kwanza kwa ukubwa barani Afrika kati ya majengo ya makao makuu ya mahakama huku likiwa la sita duniani.
Akizungumza leo Aprili 3, 2025, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mahakama Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel amesema jengo hilo litatumika kwa ajili ya Mahakama Kuu, ya Rufani na ya upeo.
Amesema gharama za ujenzi wa jengo hilo ni Sh129.7 bilioni, kati ya hizo za ujenzi bila kodi ya ongezeko la thamani ni Sh110 bilioni huku Sh19.7 bilioni ikitumika kulipa kodi hiyo.
Amesema fikra za ujenzi wa jengo hilo zilianza mwaka 2012, ambapo lilikuwa lijengwe jijini Dar es Salaam, lakini baada ya Serikali kuhamia Dodoma mwaka 2017, ujenzi ulihamishwa.
“Usanifu wa jengo hili ni alama ya nyota ulio na mabawa matatu, bawa la kwanza mahakama kuu, la pili ni mahakama ya rufani na bawa la tatu ni mahakama ya upeo (supreme court). Mahakama ya upeo bado kwenye Katiba haipo,”amesema.
Amesema kwa historia aliyoipata aliyekuwa Mtendaji wa Mahakama Tanzania, Balozi Hussein Katanga alielekeza makandarasi waweke eneo kwa ajili ya mahakama ya upeo ili uamuzi ukija kufikiwa wa kuianzisha jengo na samani ziwepo.
Profesa Gabriel amesema kuwa mbawa hizo tatu zimeunganishwa na katikati kuna jengo la utawala, lina miundombinu ya kisasa ya Tehama na eneo kwa ajili ya helikopta kutua.
Amesema sasa kuna ‘mobile court’ (mahakama inayotembea), lakini baadaye wanaweza kuamua kuwa na mahakama inayoruka (flying court) ambapo helikopta itakwenda na majaji kwenye eneo lolote na kufanya mahakama na kisha kurejea.
Amesema jengo hilo lenye sakafu tisa ambalo linakuwa la kwanza nchini kwa mahakama Tanzania kuwa na jengo tangu uhuru, limejengwa kwa fedha za ndani.
Profesa Gabriel amesema jengo hilo pia lina eneo la kunyonyeshea kwa wanawake wenye watoto wachanga, lina vyumba kwa ajili ya viongozi wa dini, mawakili, wanasaikolojia, mahabusu ya watoto, wanawake na wanaume.
Pia, Profesa Gabriel amesema Rais Samia atazindua jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama ambalo limegharimu Sh14.3 bilioni na kuwa Serikali imetoa Sh562 milioni kwa ajili ya kugharamia uhamisho kwa watumishi.
Aidha, amesema Rais Samia atazindua nyumba za majaji 48, zilizojengwa kwa thamani ya Sh42.3 bilioni.
“Sasa changamoto ya makazi kwa majaji kwa Mkoa wa Dodoma, imeisha kabisa, tunafikiria kujenga majengo mengine Dar es Salaam kwa sababu pale tuna kiwanja chetu ambacho kipo mjini kabisa,” amesema.
Akielezea mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita, Profesa Gabriel amesema bajeti ya mahakama Tanzania imeongezeka kutoka Sh160 bilioni kwa mwaka 2021/22 hadi kufikia Sh321 bilioni kwa mwaka 2025/26.
Amesema pia Sh416.46 bilioni zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya mahakama nchini huku Sh67.5 bilioni zikitumika kwa ujenzi wa mahakama za mwanzo na Sh29.7 bilioni kujenga mahakama za wilaya.
Kwa upande wa vituo jumuishi vya mahakama, Profesa Gabriel amesema vituo sita vimejengwa katika mikoa ya Dar es Salaam (2), Dodoma, Morogoro, Mwanza na Arusha.
Amesema gharama ya ujenzi wa vituo vyote sita jumuishi ni Sh51.45 bilioni, fedha ambazo ni mkopo nafuu wa Benki ya Dunia (WB).
Profesa Gabriel amesema kutokana na kufanya vizuri WB wamewapatia mkopo mwingine wa Dola za Marekani milioni 90 (sawa na Sh203 bilioni) ambao utakwenda kujenga vituo jumuishi tisa nchini.
Ametaja mikoa ambavyo vinajengwa Songea (Ruvuma), Lindi, Njombe, Songwe, Katavi, Singida, Geita na Simiyu huku Chakechake, Pemba, Zanzibar kikijengwa kituo kimoja.
Kwa upande wa ukarabati, Profesa Gabriel amesema Sh3.2 bilioni zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya mahakama mkoani Tabora na Dodoma ambayo sasa yatatumika kwa ajili ya mahakama ya familia.
Mkazi wa Nkhungu, Helena Mshana amesema jengo hilo litaondoa taswira ya majengo ya mahakama kuwa machakavu na yasiyovutia.