Mahakama yamwondoa Rais Yoon Ikulu, sasa kushtakiwa kwa uhalifu

Seoul. Mahakama ya Katiba ya Korea Kusini imemwondoa madarakani Rais Yoon Suk Yeol aliyekuwa amefutwa kazi kwa kura ya kutokuwa na imani naye, leo imehitimisha safari ya urais wake.

Uamuzi huo umefikiwa na mahakama leo Ijumaa Aprili 4, 2025, baada ya kutangaza kuwa Rais Yoon hapaswi kuendelea tena kuwepo katika Ikulu ya taifa hilo na kutoa fursa ya uchaguzi wa urais wa nchi hiyo kufanyika.

Rais Yoon ambaye ni mwanasheria wa zamani wa Serikali, aliingia kwenye siasa mwaka mmoja tu kabla ya kushinda urais mwaka 2022, amepitia misukosuko tangu alipotangaza kuiweka Korea Kusini chini ya Sheria ya Kijeshi (Martial Law) mwishoni mwa 2024.

Katika uamuzi uliosomwa mubashara kwenye televisheni, Kaimu Jaji Mkuu wa Mahakama hiyo, Moon Hyung-bae, amesema jopo la majaji wanane lilithibitisha kuondolewa kwa Yoon kwa sababu tangazo lake la sheria ya kijeshi lilikiuka katiba na sheria nyingine za nchi hiyo  kwa kiwango kikubwa.

“Mshtakiwa si tu kwamba alitangaza sheria ya kijeshi, bali pia alivunja katiba na sheria kwa kutumia vikosi vya jeshi na polisi kuzuia mamlaka ya kutunga sheria kufanya kazi yake.”

“Hatimaye, tangazo la sheria ya kijeshi katika kesi hii halikutimiza masharti halali ya hali ya dharura,” amesema Jaji Moon.

Shangwe kwa waandamanaji

Wakati uamuzi huo unasomwa mahakamani, umati wa watu ulifurika nje ya makazi yake na mahakamani wakisubiri kusikia hatma yake ambapo baada ya kutangazwa kuwa ameondolewa Ikulu, shangwe lililipuka huku wengine wakilia kwa furaha na kucheza.

Baadaye, umati huo ulianza kuandamana mitaani jijini Seoul. Wengine walivaa mavazi ya dubu wa buluu wenye sura ya kuvutia, nembo ya maandamano inayoakisi rangi za upinzani.

Uchaguzi kufanyika hivi

Kwa mujibu wa katiba ya Korea Kusini, uchaguzi wa kumpata mrithi wa Yoon, utafanyika ndani ya miezi miwili ijayo.

Hata hivyo, wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasema mgawanyiko wa kitaifa kuhusu kuondolewa kwake huenda ukaendelea na unaweza kuathiri juhudi za Korea Kusini kushughulikia sera za ‘Marekani Kwanza’ za Rais Donald Trump na uhusiano unaozidi kuimarika kati ya Korea Kaskazini na Russia.

Mmoja wa mawakili wa Yoon, Yoon Kap-keun, ameuita uamuzi huo kuwa haueleweki kabisa na wa kisiasa, lakini Rais huyo wa zamani hakutoa tamko mara moja.

Chama tawala cha Yoon, People Power Party (PPP), kilisema kitaheshimu uamuzi wa Mahakama hiyo.

Waziri Mkuu, Han Duck-soo, ambaye sasa ni kiongozi wa muda wa nchi hiyo, aliapa katika hotuba ya televisheni kuhakikisha anadumisha usalama wa umma, diplomasia na kuwapo kwa utulivu.

 Han, aliyeteuliwa na Yoon, alichukua uongozi kwa muda, Yoon aliposimamishwa madarakani kwa kufutwa kazi na Bunge la nchi hiyo.

“Kwa kuheshimu mapenzi ya wananchi wetu, nitafanya kila juhudi kusimamia uchaguzi wa rais ujao kwa mujibu wa katiba na sheria, kuhakikisha mpito laini wa uongozi,” amesema Han.

Utafiti wa maoni unaonyesha, Lee Jae-myung, ambaye ni kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Democratic Party, ndiyo mgombea anayepewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi wa kumrithi Yoon. Lee anakabiliwa na kesi za ufisadi na mashitaka mengine.

Lee aliupokea uamuzi huo na kuwapongeza wananchi wa Korea Kusini kwa kulinda Jamhuri ya Korea Kusini ya kidemokrasia.

“Ujasiri wa watu waliokabiliana na bunduki, mapanga na mizinga, pamoja na ujasiri wa wanajeshi waliokataa kutii amri zisizo za haki, umeleta mapinduzi haya makubwa ya mwanga,” amesema Lee.

Miezi minne ya moto

Sheria ya kijeshi ilidumu kwa saa sita pekee, lakini iliibua mgogoro mkubwa wa kisiasa, ikitikisa masoko ya fedha na kuwahangaisha washirika wa kidiplomasia wa Korea Kusini.

Januari 2025, Yoon alikamatwa na kushtakiwa kwa uasi kuhusiana na tangazo hilo, shitaka linaloweza kumfanya apate adhabu ya kifo ama kifungo cha maisha jela akikutwa na hatia.

Chini ya amri ya Yoon, ambayo ilikuwa ya kwanza na ya aina yake katika kipindi cha zaidi ya miaka 40, mamia ya wanajeshi walitumwa katika bunge, ofisi za uchaguzi na maeneo mengine.

Wanajeshi wa vikosi maalumu walivunja madirisha ya Bunge la taifa na kupambana na raia waliokusanyika kupinga, hali iliyowashangaza raia wa Korea Kusini na kuibua kumbukumbu za kutisha za utawala wa kijeshi.

Wabunge wakiwemo baadhi kutoka chama tawala, waliingia bungeni na kupiga kura kupinga amri hiyo kwa kauli moja.

Hakukuwa na ghasia kubwa wakati wa kipindi kifupi cha sheria ya kijeshi, lakini baadhi ya maofisa wa juu wa jeshi na polisi waliotumwa bungeni walitoa ushahidi kuwa Yoon aliwaamuru kuwatoa wabunge kwa nguvu, ili kuzuia kura dhidi ya amri yake ama kuwakamata wapinzani wake wa kisiasa.

Yoon alisema wanajeshi walitumwa bungeni ili kudumisha utulivu pekee.

Yoon, mwenye umri wa miaka 64, aliondolewa madarakani na Bunge lililodhibitiwa na upinzani wa kiliberali Desemba 14, 2024.

Katika ushahidi wake wa mwisho mahakamani, Yoon alisema amri yake ilikuwa jaribio la kukusanya uungwaji mkono wa umma dhidi ya kile alichokiita uovu wa chama cha Democratic Party, ambacho kilikuwa kimezuia ajenda yake, kuondoa maofisa wake wakuu, na kupunguza bajeti ya serikali.

Alitangaza awali kuwa bunge hilo u ni pango la wahalifu.

Yupo sana mahakamani

Baadhi ya wataalamu wanasema huenda Yoon alitangaza sheria ya kijeshi ili kuzuia uchunguzi huru juu ya kashfa zinazomuhusisha mke wake, Kim Keon Hee.

Bila kinga ya urais, Yoon anaweza kukabiliwa na mashitaka mengine ya jinai, kama vile matumizi mabaya ya madaraka. Yeye ndiye Rais wa kwanza wa Korea Kusini kukamatwa au kushtakiwa akiwa bado madarakani.

Yoon aliwahi kuwa mwendesha mashitaka mkuu chini ya mtangulizi wake, Rais wa kiliberali, Moon Jae-in, kabla ya kujiunga na chama tawala mwaka 2021 baada ya kutofautiana na washirika wa Moon.

Sifa yake ya mtu asiyeogopa na asiyetetereshwa, ilimsaidia kumshinda Lee katika uchaguzi wa mwaka 2022.

Katika sera za nje, Yoon alijitahidi kuimarisha ushirikiano wa kijeshi wa Korea Kusini na Marekani na kusuluhisha migogoro ya kihistoria na Japan.

Alisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu wa usalama kati ya Seoul, Washington na Tokyo ni muhimu kukabiliana na tishio la nyuklia la Korea Kaskazini.

Hata hivyo, wakosoaji wake walimshutumu kwa kuchochea uhasama na Korea Kaskazini na kupuuza uhusiano na China, mshirika mkubwa wa kibiashara wa Korea Kusini.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *