
Dar es Salaam: Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu imemuonya mwanaharakati Godlisten Malisa, ambaye anashiriki katika kesi ya jinai pamoja na meya mstaafu, Boniface Jacob, maarufu Boni Yai.
Mahakama hiyo imesema kwamba, endapo Malisa hatohudhuria usikilizwaji wa kesi yao siku nyingine, atachukuliwa hatua ikiwamo kupelekewa mahabusu.
Katika kesi hiyo, wawili hao wanakabiliwa na mashitaka matatu ya uchochezi.
Wanadaiwa kuchapisha taarifa za uongo katika mitandao ya kijamii, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015, wakilihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya raia.
Kesi hiyo ya jinai inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, ilipangwa kuanza kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri leo, Jumanne, Machi 11, 2025, lakini imekwama kutokana na Malisa kutokuwepo mahakamani.
Baada ya kesi hiyo kuitwa, mwendesha mashitaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clemence Kato ameieleza Mahakama wako tayari kuendelea na usikilizwaji, lakini hamuoni mahakamani hapo mshtakiwa wa pili ambaye ni Malisa.
Wakili wao, Peter Kibatala alipoulizwa kuhusiana na mteja wake huyo kutokuwepo mahakamani, amesema mshtakiwa wa kwanza, mwenzake yaani Boni Yai anaweza kuwa na maelezo.
Boni Yai alipoulizwa, amesema amewasiliana naye (Malisa) muda mfupi kabla ya kuingia mahakamani, lakini akamjibu kuwa alikuwa amesahau tarehe kama ni leo na hana hakika kama anakuja.
Baada ya kusikiliza maelezo hayo ndipo Hakimu Swallo akatoka onyo la kumtahadharisha kumpeleka mahabusu siku hali hiyo ikijitokeza tena.
“Mwambie mwenzako nitafuta dhamana, haiwezekani yeye na wadhamini wake wote wasahau tarehe. Tarehe ijayo asipofika atatokea gerezani,” amesema Hakimu Swallo.
Hata hivyo, Wakili Kibatala ameiomba radhi Mahakama kwa niaba yake, kwa hilo lililojitokeza na akaomba wapangiwe tarehe nyingine ya kusikilizwa.
Hivyo Hakimu Swallo ameahirisha kesi hiyo mpaka Machi 17 na 18, 2025 kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka.
Mashtaka yao
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani hapo kwa mara ya kwanza Mei 6, 2024 na kusomewa jumla ya mashitaka matatu, mawili kati ya hayo yanamkabili Jacob pekee yake, huku Malisa akikabiliwa na shitaka moja.
Shitaka la kwanza linalomkabili Jacob pekee ni la kuchapisha taarifa za uwongo kinyume na sheria, akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2024 jijini Dar es Salaam.
Anadai huku akijua na kwa nia ovu ya kuipotosha jamii, alichapisha taarifa katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa kijamii X wenye jina la Boniface Jacob @ExMayor Ubungo, inayolihusisha Jeshi la Polisi kuhusika na mauaji ya Baba G.
Shitaka la pili, ambalo pia linamkabili Jacob pia ni la kuchapisha taarifa za uongo, akidaiwa kutenda kosa hilo Machi 19, 2024 katika jiji la Dar es Salaam.
Anadaiwa kuwa kwa nia ovu ya kuupotosha umma, alichapisha taarifa katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa kijamii X wenye jina la Boniface Jacob @ExMayor Ubungo.
Katika shitaka hilo anadaiwa kuandika ujumbe unaolihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, Omari Msamo akidai kuwa aliuawa na askari wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
Shitaka la tatu ambalo pia ni la kutoa taarifa za uongo, linamkabili Malisa pekee yake, akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2024 katika jiji la Dar es Salaam.
Malisa anadaiwa siku hiyo ya tukio, kwa nia ovu na kwa lengo la kuupotosha umma na jamii, alichapisha taarifa ya uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram wenye jina la Malisagj, kwa kuandika ujumbe uliosomeka:
“Tarehe 13 Aprili meya mstaafu wa Manispaa ya Ubungo @Exmyor_bonifacejacob alitoa taarifa ya kupotelewa na ndugu yake Bw. Robert Mushi maarufu kama Babu G, ambaye alipotea mapema mwezi April 2024.
Inadaiwa alikamatwa na watu waliojitambulisha kuwa Polisi maeneo ya Kariakoo na baada ya hapo hawakuonekana tena…leo wakaambiwa “nendeni Hospitali ya Polisi Kilwa Road, ndugu yenu amefichwa mochwari pale” wakaenda.
La haula! Wakamkuta Robert akiwa kwenye jokofu la baridi. Hakuwa Robert tena bali ni mwili wake ukiwa na majeraha ya kipigo.
Ni mauaji ya kikatili. Masikini Robert hajawahi kuwa na ugomvi na mtu kwa nini utendewe haya” mwisho wa maelezo hayo.
Hata hivyo washtakiwa wote walikana mashitaka hayo na wapo nje kwa dhamana