
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemkuta na kesi ya kujibu raia wa Burundi Ferdnand Ndikuriyo (27) maarufu Chuma cha Chuma, anayekabiliwa na shtaka la kuwepo nchini Tanzania bila kuwa na kibali.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu, Novemba 25, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa uamuzi.
Chuma ambaye ni msanii wa muziki na mkazi wa Mbezi Louis, alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 4, 2024 na kusomewa kesi ya jinai yenye shtaka hilo.
Awali, Wakili wa Serikali, Raphael Mpuya amedai kesi hiyo imeitwa kwa ajili mahakama kutoa uamuzi iwapo mshtakiwa ana kesi ya kujibu au laa na upande wa mashtaka upo tayari kusikiliza.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Ruboroga amesema amepitia ushahidi wa mashahidi wawili pamoja na vielelezo na hivyo Mahakama hiyo imemkuta na kesi ya kujibu.
“Mahakama imekukuta na kesi ya kujibu mshtakiwa Ndikuriyo, hivyo unatakiwa ujitete,” amesema hakimu Ruboroga.
Hata hivyo, mshtakiwa alidai kuwa atajitetea kwa njia ya kiapo na hatakuwa na shahidi wala kielelezo, bali atajitetea mwenyewe.
Baada ya kueleza hayo, Ndikuriyo alianza kutoa ushahidi wake ambapo amedai alikuwa na kesi kipindi cha nyuma aliyoshtakiwa Mahakama ya Mwanzo Kinondoni inayofanana na hiyo iliyopo Mahakama ya Kisutu ambayo alishahukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita.
Amedai baada ya kumaliza kifungo hicho, alirudi Polisi mara kadhaa lakini waligoma kumpatia hati yake ya kusafiria kwa sababu walikuwa wanaendelea kufanya uchunguzi wa kesi nyingine.
Amesema hata mashahidi wawili wa upande wa mashitaka walipotoa ushahidi wao mahakamani, walithibitisha kuwa hati yake ya kusafiria inashikiliwa Polisi.
“Hata, shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka alisema ni kweli hati yangu ya kusafiria ilikuwa inashikiliwa polisi,” amedai mshtakiwa.
Amebainisha kuwa kushikiliwa Polisi kwa hati yake ya kusafiria kulimfanya ashindwe kuhuisha taarifa zake pamoja na viza.
Ndikuriyo baada ya kutoa ushahidi wake, alihojiwa maswali na wakili wa upande wa mashitaka kuhusiana na ushahidi alioutoa na ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo.
Wakili: Una ushahidi gani kama uliwahi kwenda kuripoti kituo cha Polisi?
Mshtakiwa: Nilienda na wadhamini wangu.
Wakili: Na kama Polisi ulikuwa unaripoti, ilikuaje wakakukamata tena?
Mshtakiwa: Kimya.
Wakili: Ni sahihi umesema ulikuwa na wadhamini wako, ambao hapa Mahakama hujawaleta ili waje watoe ushahidi?
Mshtakiwa: Ni sahihi.
Wakili: Ni kweli masuala ya viza yanashughulikiwa na ofisi ya uhamiaji?
Mshtakiwa: Ni kweli.
Wakili: Kuna uthibitisho wowote umeuleta mahakamani hapa unaonyesha kuwa wewe ulienda ofisi ya uhamiaji kueleza hiyo changamoto kuwa hati yako ya kusafiria inashikiliwa?
Mshtakiwa: Sijaleta.
Wakili: Wakati wa unakamatwa mwaka huu, viza yako ilikuwa hai au ilikuwa imeisha?
Mshtakiwa: Ilikuwa imeisha
Wakili: Kwa kuwa ulijua viza yako imeisha muda wake na kwa kuwa wakili wako alikusaidia hadi umefikishwa mahakamani. Je, wakili wako ulimtuma ofisi za uhamiaji?
Mshtakiwa: Sikumtuma.
Mshtakiwa baada ya kumaliza kuhojiwa na upande wa mashitaka alifunga ushahidi wake.
Hakimu Ruboroga baada ha kusikiliza ushahidi huo, amepanga Desemba 5, 2024 kutoa hukumu dhidi ya mshtakiwa.
Ndikuriyo amerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Kesi ya msingi:
Chuma ambaye makazi yake ya muda ni Mbezi Lousi na makazi ya kudumu ni nchini Burundi, anadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 18, 2024 eneo la Upanga, Las Vegas Casino, Ilala, Dar es Salaam.
Inadaiwa kuwa, mshtakiwa akiwa eneo hilo, alibainika kuwepo nchini bila kuwa na kibali, wakati akijua kuwa ni kinyume cha sheria.