Mahakama yajitenga kujadili uhalali ndoa ya Mrema, Doris

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani, imekataa kujadili uhalali wa ndoa kati ya aliyekuwa mwanasiasa mkongwe nchini, Augustino Mrema na Doris Mkandala kwa kuwa suala hilo halikuwahi kutolewa maamuzi na Mahakama Kuu.

Jopo la majaji watatu wa mahakama ya Rufani, Lugano Mwandambo, Abraham Mwampashi na Dk Eliezer Feleshi, limekosoa hukumu ya Mahakama Kuu iliyoenda mbali na kushughulikia nani waliostahili kuwa warithi wa mali za Mrema.

Hukumu ya majaji hao, imetolewa Aprili 16, 2025 na nakala yake kupatikana mtandaoni jana, kufuatia rufaa iliyowasilishwa na mtoto wa kiume wa Mrema, Peter ambaye ni msimamizi wa mirathi ya Mrema.

Doris maarufu kama Doreen Kimbi, alifunga ndoa na Mrema Machi 24, 2022 katika Parokia ya Uwomboni Jimbo Katoliki la Moshi, wakati huo Mrema akiwa na umri wa miaka 77 na Doreen akiwa na umri wa miaka 38.

Ndoa ya wawili hao ilipata umaarufu mkubwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kutokana na tofauti ya umri wa wawili hao, historia ya Mrema pamoja na umaarufu wake, lakini hata hivyo Mrema alifariki siku 150 tangu ndoa ifungwe.

Hadi umauti unamkuta, Mrema alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP) na alishawahi kushika wadhifa wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi  pia Waziri wa Kazi na Ajira na Mbunge wa Vunjo.

Kiini cha mvurugano

Baada ya kifo cha Mrema, mtoto wa kiume wa mwanasiasa huyo, Peter Mrema aliwasilisha ombi la kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu, lakini Doris akaweka pingamizi, akitaka ajumuishwe kuwa msimamizi mwenza.

Sababu za kuomba kuwa msimamizi mwenza ni kuwa Peter alikuwa amewabagua watoto watatu wa marehemu wa nje ya ndoa katika orodha ya wanufaika, kushindwa kuorodhesha mali zote na kukosa imani naye kwa sababu kuu mbili.

Moja ni kuwa muombaji huyo alikuwa amemtimua kwenye nyumba yao ya wanandoa iliyopo Salasala jijini Dar es Salaam pia kutokana na kitendo chake cha kumnyang’anya gari alilokuwa amepewa na mumewe ambaye ni Mrema.

Akipinga Doreen kuwa msimamizi mwenza, mtoto huyo wa marehemu (Peter) alisema Doreen siyo mtu wa kumwamini na aliolewa na baba yao wakati ndoa yake (Doreen) ya awali haijavunjwa na amekuwa akibadili majina yake mara kwa mara.

Doreen alipinga madai hayo akisema walishaachana kwa talaka na mume wake wa kwanza na hivyo ndoa kati yake na Mrema ilikuwa ni halali, hoja ambayo pia ilikubaliwa na Jaji, kwamba kulikuwa hakuna uthibitisho ana ndoa nyingine.

Katika hukumu yake aliyoitoa Oktoba 20, 2023, Jaji Augustine Rwizile wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam aliwajumuisha pia watoto watatu wa Mrema waliozaliwa nje ya ndoa kama wanufaika wa mali za mwanasiasa huyo.

Watoto hao wa nje ya ndoa ni Elizabeth Mrema (52), Elizabeth Mrema (43) na Goodlove Mrema (18) wakiungana na watoto wengine wa Mrema, Mary Mrema (48), Cresensia Mrema (45), Michael Mrema (40) na Edward Mrema (38).

Kuhusu nani wana uhalali wa kisheria wa kuwa wanufaika, Jaji Rwizile alisema mali hizo zinapaswa kugawanywa kwa mke na watoto wa marehemu akiwamo Peter Mrema kama sheria inavyoelekeza pale mtu anapokufa bila kuacha wosia.

Hata hivyo, Jaji Rwizile alilikataa ombi la Doris kuwa msimamizi mwenza.

Rufaa ya mtoto wa Mrema

Msimamizi huyo wa mirathi, Peter Mrema aliyewakilishwa mahakamani na mawakili Nazael Tenga, Hamis Albaraka na Grayson Laizer hakuridhishwa na hukumu ya Mahakama Kuu na alikata rufaa Mahakama ya Rufani akiegemea sababu tano.

Sababu ya kwanza ni kuwa Mahakama Kuu ilifanya makosa kwa kukubali kuwa ndoa ya marehemu Mrema na Doris ilikuwa halali bila kuwepo uthibitisho wowote kuwa ndoa yake ya awali na mwanamme mwingine ilikuwa imevunjwa kisheria.

Hoja ya pili ni kuwa mahakama ilikosea kwa kukubali kuwa sheria inayosimamia mgawanyo wa mali za marehemu ni ya India (Indian Succession Act) bila kuwepo kwa uthibitisho wa hali ya maisha (mode of life) aliyokuwa akiishi Mrema.

Mbali na hoja hiyo, katika hoja ya tatu, mrufani alidai mahakama ilifanya makosa ilipokubali kuwa watoto wanaodaiwa walizaliwa nje ya ndoa walikuwa ni wa watoto wa damu wa marehemu (biological children) bila uthibitisho wowote.

Mrufani alisema mahakama ilifanya makosa kuegemea ushahidi wa baadhi ya vyeti vya kuzaliwa ambavyo vilipatikana baada ya kifo cha marehemu na pia ilikosea kuegemea sheria ya mtoto kuwatambua watoto hao kama wanufaika.

Hukumu ya jopo la majaji

Majaji hao walianza kwa kunukuu mstari wa Biblia kitabu cha Marko 15:24 unayosema “Basi wakamsulubisha, wakagawana nguo zake kwa kuzipigia kura kuamua kila mtu achukue nini,” kuelezea kile kinachotokea katika familia hiyo.

Walisema huo ndio msimamo unajitokeza katika urithi pale ambapo marehemu hufariki bila kuacha wosia unaoelekeza jinsi mambo yake yatakavyosimamiwa baada ya kifo chake, kama ilivyotokea kwa mwanasiasa huyo wa upinzani.

“Katika masuala hayo kama ilivyo katika rufaa hii, masuala ya usimamizi wa mirathi yake yatategemea uamuzi wa warithi kupitia mkutano ambao unaweza usiakisi matakwa yake (Mrema) kama angeacha wosia,” wameeleza majaji hao.

“Mara nyingi zaidi, urithi wa mali za mtu ambaye hakuacha wosia huwa si mwepesi hasa katika hatua ya kuteua msimamizi wa mirathi au usimamizi wa mirathi ya marehemu baada ya msimamizi kuteuliwa,” walieleza majaji hao.

Uhalali ndoa ya Doris na Mrema

Katika hukumu yao, majaji hao watatu walisema sababu ya kwanza ya rufaa inayohusu uhalali (validity) wa ndoa kati ya marehemu na mjibu rufaa imejengwa katika msingi kuwa kulikuwa hakuna uthibitisho ndoa ya awali ya Doris ilivunjwa.

Kulingana na majaji hao, wakili Tenga alijenga hoja kuwa Mahakama Kuu iliyosikiliza suala hilo iliwajibika kumtaka mjibu rufaa kuthibitisha kuwa ndoa yake ilivunjwa au kuita watu wanaofahamu uhusiano huo waweze kutoa ushahidi.

Wakili huyo alisema ilikuwa ni makosa kwa mahakama iliyosikiliza shauri hilo kuegemea cheti cha ndoa pekee kuthibitisha uhalali wa ndoa bila kuzingatia kuwa vyeti vya ndoa kuna uwezo wa vyeti hivyo kugushiwa.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Frank Kilian aliyemwakilisha Doris, alisema suala la uhalali wa ndoa kati ya mteja wake na marehemu haikuwa hoja iliyokuwa mbele ya Mahakama Kuu wala siyo hoja inayoweza kuamuliwa na Mahakama ya Rufani.

Baada ya kusikiliza pande hizo mbili, majaji walirejea shauri la kuomba kuwa msimamizi wa mirathi ambapo walisema mrufani mwenyewe katika maombi yake hayo alikuwa akimtaja mjibu rufaa kama mjane wa marehemu.

Majaji hao walisema katika kikao cha ukoo, mjibu rufaa alitambuliwa kama mjane na mrithi halali wa mali ya marehemu na kwamba hata katika kiapo chake Peter, anamtaja Doris kama mjane na mrithi wa mali ya marehemu Mrema.

“Kwa maoni yetu, suala la uhalali wa ndoa kati ya mjibu rufaa na marehemu halikupaswa kuwa suala la kushughulikiwa na mahakama kuu wala halipaswi kuwa suala la kushughulikiwa na Mahakama ya Rufani kama alivyosema wakili Kiliani.”

“Kwa vile mahakama kuu haikufanya uamuzi wowote kuhusiana na uhalali wa ndoa, hapakupaswa kuwepo na sababu ya rufaa inayohusu jambo hilo. Hii ni kukiuka sheria inayotaka sababu za rufaa zitokane na uamuzi wa jambo lenyewe.”

Majaji hao walisema madai kuwa mjibu rufaa alikuwa na ndoa nyingine halali yaliibuliwa kwa mara ya kwanza na mrufani kupitia hati ya kiapo kinzani wakati akijibu kiapo kilichotokana na pingamizi la mrufani kuteuliwa kuwa msimamizi.

“Vyovyote iwavyo, wajibu wa kuthibitisha mjibu rufaa alikuwa na ndoa nyingine halali lilikuwa ni la mrufani. Angeweza kutafuta (search) kwa msajili wa ndoa kuthibitisha kama mjibu rufaa alikuwa na ndoa nyingine halali,” wamesema.

“Ni lini na kwa vipi mrufani alifahamu kutokuwepo kwa talaka ni jambo la kuhisi kwa kila mtu lakini kama hilo lingekuwa ni hoja basi mrufani angemwita mume huyo anayedai ndoa yake iko hai ili aweze kutoa ushahidi upande wake,” wamesema.

“Mwisho tumejiuliza kama mahakama iliyosikiliza suala la mirathi ingeweza kuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuamua kuhusu uhalali wa ndoa baina ya mjibu rufaa na marehemu Mrema. Jibu ni kwamba mahakama haina mamlaka hayo,” wamesema.

Majaji wamesema kama ilifanya maamuzi hayo, maamuzi hayo ni batili na kuongeza kuwa sababu ya kwanza ya rufaa haina mashiko kisheria.

Kuhusu hoja nyingine, majaji hao walisema Mahakama Kuu baada ya kusikiliza ombi la Peter Mrema kuwa msimamizi na kulikubali, huo ndio ulikuwa mwisho wa mahakama kwani msimamizi ndio aliwajibika kuorodhesha mali na wanufaika.

Katika hoja hiyo, Wakili Tenga alikosoa uamuzi wa Mahakama Kuu kuwatambua watoto watatu wa nje wa marehemu kwa kuegemea cheti za kuzaliwa pekee badala ya kusikiliza ushahidi kuthibitisha walikuwa ni watoto wa marehemu.

Majaji hao walisema pamoja na yote hayo, wajibu wao kama mahakama ya rufani ni kupima iwapo mahakama ilikuwa na uwezo wa kubaini nani ni mnufaika wa mali za marehemu wakati inaamua kuhusu uteuzi wa msimamizi wa mirathi.

Kwa mujibu wa majaji hao, mahakama imepewa tu nguvu ya kumteua msimamizi wa mirathi na suala la nani anastahili kuwa mnufaika wa mali za marehemu linaachiwa kwa msimamizi na kwamba mahakama ilipotea njia ilipolishughulikia.

Majaji hao katika hukumu yao wamesema baada ya mahakama kuu chini ya Jaji Rwizile kukataa ombi la Doris kuwa msimamizi mwenza, mahakama haikuwa na shughuli nyingine isipokuwa kumteua msimamizi wa miradhi ya Mrema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *