
Dar es Salaam. Katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabiliwa washtakiwa 13, wakiwemo waliokuwa watumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), umeieleza Mahakama kuwa bado wanaendelea na uchunguzi dhidi ya kesi hiyo.
Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Alhamisi Machi 20, 2025 wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matano, likiwemo kuharibu noti zenye thamani ya Sh4.6 milioni kwa kuzichanachana na hivyo kuisababishia benki hiyo hasara ya zaidi ya Sh4.6 bilioni.
Kasala ameieleza Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mhini alikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Aprili 17, 2025 itakapotajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mariagoreth Kunzugala, maarufu Bonge, Henry Mbowe, maarufu Mzee wa Vichwa, Asha Sekiboko, Cecilia Mpande, Agripina Komba, Zubeda Mjewa, Khadija Kassunsumo na Mwanaheri Omary wote walikuwa wafanyakazi wa BoT na wakazi wa jijini Dar es Salaam.
Wengine ambao sio watumishi wa BoT ni Alistides Genand, Musa Chengula, Zaituni Chihipo na Respicius Rutabilwa.
Katika hati ya mashitaka inadaiwa, kati ya Januari 2017 hadi Septemba 30, 2019, washtakiwa wakiwa watumishi wa BoT, kwa kuvunja majukumu yao ya kazi waliwezesha utendekaji wa kosa la kuongoza genge la uhalifu.
Pia inadaiwa, Genand, Mchegage, Chengula, Chihipo na Ishengoma wakiwa si watumishi wa BoT, kwa kushirikiana na watumishi hao wa BoT kwa makusudi, waliwezesha kutendeka kosa la uhalifu wa kupanga.
Katika shitaka la tatu, washtakiwa wote bila ya kuwa na kibali na kutokuwa wazalendo, waliharibu noti 460,000 za Sh10,000 kila moja kwa kuzikatakata zenye thamani ya Sh4.6 bilioni.
Katika shitaka la nne, siku na maeneo hayo, kwa mawasilisho ya kilaghai, kwa kujua na kwa mpango wa kitapeli washtakiwa wote walijipatia Sh1.5 bilioni kutoka BoT baada ya kuwasilisha noti hizo BoT.
Katika shitaka la tano washtakiwa wote wanadaiwa kuisababishia BoT hasara ya Sh4.6 bilioni.