
Arusha. Mahakama ya Rufani imebariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyohukumiwa mkazi wa Wilaya ya Senrengeti mkoani Mara, Musa Range baada ya kukutwa na hatia ya kumpiga hadi kumuua mtoto wake aliyekuwa na umri wa miaka miwili na nusu, Emmanuel Musa.
Mahakama hiyo imetoa hukumu hiyo Februari 28, 2025 baada ya kutupilia mbali rufaa iliyokuwa imekatwa na Musa akipinga adhabu hiyo aliyopewa na Mahakama Kuu Kanda ya Musoma Julai 12, 2021 katika kesi ya jinai.
Tukio hilo lilitokea Juni 17, 2017 katika Kijiji cha Nyamatare wilayani Serengeti ambapo mke wa Musa, Pendo Marwa ambaye ni mama mzazi wa marehemu, aliondoka nyumbani kwake na kwenda kwa baba mkwe wake Kijiji cha Mwigaye kwa ajili ya kulalamika kuhusu tabia ya mume wake kumpiga mtoto huyo.
Pendo ambaye katika kesi ya msingi alikuwa shahidi wa kwanza, alidai mahakamani kuwa siku ya tukio mumewe alimpiga sana marehemu, hivyo kwa kuhofia usalama wa mtoto alilazimika kwenda kushitaki kwa wakwe zake.
Alidai alipofika kijijii humo, baba mkwe wake alimuagiza mmoja wa ndugu wa Musa, Magoiga Range, kuongozana naye (Pendo) hadi kijijini kwao ili kujua sababu za vitendo vya ukatili kwa mtoto huyo.
Pendo alidai alipofika nyumbani alimkuta mrufani akiwa anafyatua matofali, lakini marehemu hakuwepo nyumbani na kuwa baada ya muda, mumewe alikiri kufanya kitendo kibaya cha kumuua mtoto wao.
Baada ya Pendo kupiga kelele na wananchi kukusanyika eneo hilo, walianza kuutafuta mwili wa marehemu ambapo mtoto wao mkubwa aliyekuwa na umri wa miaka tisa aliwaongoza hadi kwenye kichaka ambapo mwili wa marehemu ulikuwa umefichwa.
Hukumu hiyo ilitolewa na majaji watatu wa Mahakama ya Rufani ambao ni Barke Sehel, Lucia Kairo na Amour Khamis.
Jaji Sehel amesema wamefuatilia kwa makini mawasilisho ya mawakili wa pande zote na kinachojitokeza kwa uamuzi wetu ni kama mashahidi wa upande wa mashitaka walikuwa wa kuaminika na wa kweli.
Amesema wanaanza na kanuni ya sheria iliyowekwa juu ya uthibitisho wa shahidi kwamba, kila shahidi, pamoja na mshtakiwa, ana haki ya kuthibitishwa na lazima aaminiwe na ushuhuda wake kukubaliwa isipokuwa kama kuna sababu za kutosha za kutomwamini, huku wakinukuu mashauri kadhaa ya Mahakama ya Rufani.
Jaji Sehel amesema kuhusu kukiri kwa mdomo, ungamo hilo lilifanywa na mrufani kwa mkewe (shahidi wa kwanza) na wao wanaona ungamo lilifanywa kwa uhuru kwani hatukupata ushahidi wa kushawishiwa, vitisho au nguvu, kwa hiyo wanaridhika kwamba mrufani alikiri kwa mdomo akiwa huru.
“Kinachofuata cha kuzingatia kuhusu kukiri kwa mdomo ni kama kuna ubora wa kukiri. Maneno yaliyotamkwa na mrufani kwa shahidi wa kwanza yanaonyeshwa katika ukurasa wa 10 wa rekodi ya rufaa.
“Inasomeka: ‘Mshitakiwa, mume wangu aliniambia kuwa amemuua mtoto wetu. Musa Range aliniambia kuwa amefanya kitendo kibaya cha kumuua mtoto Emmanuel Musa’.”
Jaji Sehel amesema wanakubaliana na upande wa Jamhuri kuwa mrufani alikiri kosa kwa mdomo ambalo kwa mujibu wa kifungu cha 3 na 27 cha Sheria ya Ushahidi na kuwa mashahidi wanne wa Jamhuri walikuwa mashahidi wa kuaminika na walifikia uamuzi sahihi katika kumtia hatiani mrufani, kwa kuzingatia ushahidi wa kimazingira na ungamo la mdomo alilotoa mrufani.
Kutokana na sababu hizo, majaji hao walitupilia mbali rufaa hiyo kutokana na kukosa mashiko.
Ilivyokuwa
Usiku wa tukio hilo, Magoiga alimpigia simu Mwenyekiti wa kitongoji cha Mirengo, Thomas Nyahanga (shahidi wa pili) na kuripoti tukio hilo, kisha taarifa kutolewa Polisi.
Shahidi wa nne ambaye ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Mugumu, Albert Kasanga, ambaye aliufanyia uchunguzi mwili wa marehemu na kueleza kuona michubuko kwenye mwili wa marehemu, ambaye alikuwa na nguo zilizotapakaa damu.
Shahidi huyo alihitimisha kuwa chanzo cha kifo cha marehemu ni majeraha katika viungo vya ndani, ambavyo ni ini, wengu, kibofu unaosababishwa na kitu butu kilichowekwa kwa nguvu kwenye tumbo, na hivyo kusababisha mshtuko wa moyo.
Mwili wa marehemu uliagwa Juni 17, 2017 bila kuwepo mrufani ambapo kwa mujibu wa mkewe, alitoweka baada ya kutenda kosa hilo na kurejea baada ya siku tano.
Machi 3, 2019 mrufani huyo alidaiwa kuonekana nyakati za usiku ambapo alikamatwa Machi 4, mwaka huohuo nyumbani kwake na kufikishwa mbele ya Mahakama Kuu kwa kosa la mauaji.
Katika utetezi wake, mrufani alikana kutenda kosa hilo na kudai siku ya tukio alikuwa nyumbani na watoto wake wawili waliokuwa wakicheza nje, na mara alimsikia mtoto mkubwa akilia na alipotoka alimkuta marehemu akiwa na shambulio la kifafa huku akitokwa povu mdomoni.
Alidai kukimbilia duka la dawa la karibu kununua dawa lakini aliporudi, alimkuta mwanawe amefariki na kuwa chanzo cha kifo cha mtoto wake ni ugonjwa wa kifafa, hali ambayo alidai marehemu aliipata baada ya kunyonya huku akikana kutoroka kijijini.
Alidai alishiriki katika ibada ya maziko ya mtoto wake, na baada ya hapo aliendelea na shughuli zake kabla ya kukamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kumiliki silaha kinyume cha sheria.
Mahakama Kuu kupitia ushahidi wa kimazingira uliotolewa na upande wa mashitaka, ilieleza kumtia hatiani mrufani na kumuhukumu adhabu hiyo.
Baada ya kutoridhishwa na hukumu hiyo, Musa alikata rufaa Desemba 8,2021 akiwa na sababu nane kabla ya kuziongezea hadi kufika 12, Januari 2022.
Miongoni mwa sababu hizo ni Mahakama iliyosikiliza kesi ilikosea kisheria kushikilia kwamba, upande wa mashitaka ulithibitisha kesi yake bila shaka, mahakama ilikosea kutoa hatia dhidi ya mrufani licha ya kwamba, uaminifu wa mashahidi wa upande wa mashitaka ulikuwa na shaka kutegemewa kutiwa hatiani.
Katika rufaa hiyo Musa aliwakilishwa na Wakili Leonard Magwayega huku Jamhuri ikiwakilishwa na mawakili wa Serikali wawili wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Madikenya.