Mahakama ya rufaa ya Mali yakataa ombi la kuwaachia huru baadhi ya wapinzani

Mahakama ya rufaa katika mji mkuu wa Mali, Bamako jana ilikataa ombi la kuwaachiwa huru mawaziri na wanasiasa 11 waliokuwa wakiukosoa uongozi wa kijeshi nchini humo ambao walitiwa nguvuni mwezi Juni kwa kile kilichotajwa kuwa kula njama dhidi ya utawala wa kijeshi.

Wakosoaji hao walioko mbaroni ni pamoja na mawaziri na wanasiasa kadhaa wa zamani waliosaini azimio lililochapishwa mwezi Machi mwaka huu wakitaka kurejeshwa utawala wa kiraia huko Mali. 

Watu hao 11 walitiwa nguvuni wakati wakifanya kikao cha faragha katika mji mkuu wa Mali, Bamako kipindi ambacho shughuli zote za vyama kisiasa zilikuwa zimepigwa marufuku na utawala wa kijeshi wa nchi hiyo. 

Mawakili wanaowatetea wapinzani hao  walioko mbaroni wamesema kuwa wateja wao bado wana fursa ya kukata rufaa katika mahakama nyingine. 

Mawaziri hao wa zamani na wanasiasa wa upinzani ambao walisaini tamko lao Machi 31 mwaka huu walikosoa ombwe la kisheria na kitaasisi lilioachwa baada ya kumalizika muhula ulioainishwa kwa uongozi wa kijeshi kuondoka madarakani huko Mali.