Mahakama Kuu ya India yabatilisha hukumu ya kuzifunga Madrasa 17,000 za Waislamu

Baada ya uhakiki na uchunguzi uliochukua muda wa miezi kadhaa, Mahakama Kuu ya India hatimaye imetoa uamuzi wa kubakishwa Madrasa 17,000 za Waislamu zilizotaka kufungwa katika jimbo kubwa zaidi la nchi hiyo la Uttar Pradesh.

Baada ya ufuatiliaji mkubwa uliofanywa na mawakili na wabunge Waislamu, hatimaye Mahakama Kuu ya India, na baada ya miezi kadhaa ya uhakiki imezuia kufungwa madrasa hizo katika jimbo la Uttar Pradesh.

Hukumu ya Mahakama Kuu ya India inayoamuru kuendelea kubaki Madrasa za Waislamu, imetolewa wakati miezi minane iliyopita, Mahakama ya Juu ya mji wa Allahabad katika jimbo la Uttar Pradesh ilitoa amri ya kufungwa skuli hizo za kidini za Kiislamu na kuagiza wanafunzi wa madrasa hizo wapelekwe skuli za serikali. Mbali na uamuzi huo wa Mahakama ya Juu ya Allahabad kuzitia wasiwasi familia za Waislamu, ulikuwa unahatarisha pia hatima ya wanafunzi milioni 1.7 wa madrasa hizo pamoja na walimu 10,000.

Mahakama Kuu ya India

Baadhi ya wachambuzi wa siasa za India wameutafsiri mpango wa kutaka kuzifunga madrasa za Waislamu katika jimbo la Uttar Pradesh kama utangulizi wa utekelezaji wa mpango wa kuzifunga madrasa kote nchini India, ambao hata hivyo umetibuliwa na kuzimwa na uamuzi wa Mahakama Kuu.

Uttar Pradesh ndilo jimbo lenye watu wengi zaidi nchini India likiwa na wakazi zaidi ya milioni 250. Waislamu, ambao idadi yao nchini humo inapindukia milioni 200, wanaunda khumsi, au moja ya tano ya wakazi wote wa jimbo hilo…/