
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Machi 14, 2025 kutoa uamuzi wa ama kumuondolea mashitaka na kumfutia kesi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya(33) au kuendelea na kesi hiyo.
Uamuzi huo umetolewa leo, Machi 11, 2025 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini baada ya kusikiliza hoja za upande wa mashitaka na wa utetezi zilizowasilishwa mahakamani hapo kuhusiana na kesi hiyo.
Gasaya anakabiliwa na mashitaka mawili ambayo ni kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha kiasi hicho cha fedha.
Kesi hiyo iliitwa leo, Machi 11, 2025 kwa ajili ya upande wa mashitaka kujibu hoja zilizotolewa na upande wa utetezi za kutaka mshtakiwa katika kesi hiyo afutiwe mashitaka yake na kuachiwa huru.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema akisaidiana na Roida Mwakamele, waliiomba mahakama hiyo itupilie mbali hoja za upande wa mashitaka kwa kuwa Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali cha DPP.
Awali, Gasaya aliomba mahakama hiyo, imfutie kesi inayomkabili na kumuachia huru kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika tangu mwaka 2022, aliposhtakiwa.
Gasaya kupitia wakili wake, Nafikile Mwamboma aliwasilisha ombi hilo, Machi 6, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geoffrey Mhini, wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Mwamboma amefikia hatua hiyo, baada ya upande wa mashitaka kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
“Mheshimiwa hakimu, napinga ombi la upande wa mashitaka la kutaka kuahirisha kwa kesi hii, kwa sababu mshtakiwa alishafutiwa na kukamatwa tena na kufunguliwa kesi nyingine yenye mashitaka kama ya mwanzo” alidai Mwamboma na kuongeza.
” Mheshimiwa hakimu, baada ya marekebisho ya sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kifungu cha 91(3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kinaleta takwa, kama mshtakiwa ameachiwa kwa kosa lilelile, hawezi kukamatwa kwa kosa lilelile na hoja zilezile” alidai Mwamboma.
Aliongeza kuwa sheria hiyo iliweka takwa moja kwa upande wa mashitaka wawe na ushahidi wa kutosha ndipo mshtakiwa akamatwe tena.
“Kukamatwa kwake tena kwa mara ya pili, kunamaanisha upande wa mashitaka wana ushahidi wa kutosha na kesi inapaswa kusikilizwa, hivyo hii sababu ya upelelezi kutokamilika inashangaza” alidai wakili na kuongeza
Mwamboma aliendelea kudai kuwa, pia mwongozo wa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ( DPP) wa Septemba 20, 2022 kuhusu ufunguaji wa mashitaka na ukamilishaji upelelezi kwa makosa ya jinai unaeleza kuwa mshtakiwa hatakamatwa kama upelelezi haujakamilika.
“Na kesi hii iliitakiwa ikamilike upelelezi wake ndani ya siku 90 na kama haujakamilika, Mwendesha mashitaka wa Mkoa anatakiwa kuomba kibali kwa DPP ili kukamilisha upelelezi lakini hawajafanya hivyo” aliendelea kudai wakili Mwamboma.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa, kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5,139,865,733 kutoka Saccos ya Jatu kwa kujipambanua fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua kuwa sio kweli.
Shtaka la pili ni kutakatisha fedha hizo, tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es salaam.