Mahakama kuajiri watumishi wapya 522

Dar es Salaam. Wakati ajira mpya 522 za Mahakama zikitarajiwa kutolewa katika mwaka wa fedha 2025/26, kada sita zimetajwa kuwa ndizo zenye upungufu mkubwa katika mhimili huo.

Kada hizo ni za ofisa Tehama, ofisa hesabu, msaidizi wa hesabu, walinzi, wasaidizi wa ofisi na mahakimu.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 30, 2025 Bungeni jijini Dodoma wakati wa uwasilishaji taarifa ya Kamati ya Bunge ya Bajeti kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mfuko wa Mahakama-Fungu 40 kwa mwaka wa fedha 2024/25 pamoja na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Oran Njeza amesema bado uhitaji wa watumishi ni mkubwa kutokana na ongezeko la Mahakama mpya, kutokana na kupanuka kwa huduma kulingana na uhitaji uliopo.

Amesema kada hizo sita alizozitaja kwenye taarifa yake ndizo zina upungufu mkubwa.

Katika taarifa hiyo, amesema Mahakama imepanga kuajiri watumishi 522 katika mwaka wa fedha 2025/26 idadi aliyosema bado haikidhi mahitaji halisi ya watumishi 10,351 wanaohitajika.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25 Mahakama ilitarajia kuajiri watumishi 1,562, ingawa hadi Aprili 22, mwaka huu ilipata vibali vya kuajiri watumishi wapya 545 na watumishi wa ajira mbadala 216, hivyo kuwa na upungufu wa watumishi 1,071.

“Katika mwaka 2025/26 Mahakama imepanga kuajiri jumla ya watumishi 522, idadi hii bado haikidhi mahitaji halisi ya watumishi 10,351 wanaohitajika,” amesema Njeza alipokuwa akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo.

Hivi sasa mahakama ina watumishi 6070.

Amesema Mahakama pia imeshindwa kupandisha vyeo watumishi 2,464  na kuwabadilisha kada za watumishi wengine 64 katika mwaka wa fedha 2024/25.

“Mahakama ilitenga nafasi za kupandisha vyeo watumishi 2,464 na kuwabadilisha kada watumishi 64, hata hivyo imeshindwa kutekeleza suala hilo kutokana na kuchelewa kupata vibali kwa ajili ya utekelezaji,” amesema.

Amesema kwa kuwa upatikanaji wa nafasi za kuajiri unategemea idhini ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora (OR-MUUB), Kamati hiyo inaishauri Serikali itoe kipaumbele kwa mhimili huo muhimu kwa utolewaji wa haki.

“Ujenzi wa majengo ya Mahakama hatakuwa na maana endapo kuna uhaba wa rasilimali watu katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema. 

Akiwasilisha tathmini ya utekelezaji wa bajeti na majukumu ya Mfuko wa Mahakama kuanzia Julai, 2024 hadi Aprili 22, 2025, pamoja na vipaumbele na masuala muhimu yanayopendekezwa katika Mpango na Bajeti ya Mfuko wa Mahakama kwa mwaka wa Fedha 2025/26, amesema katika mwaka wa fedha 2024/25  Mfuko wa Mahakama uliidhinishiwa na Bunge zaidi ya Sh241.5 bilioni.

Kati ya fedha hizo, zaidi ya Sh71.9 bilioni ni mishahara ya Mahakama, Sh2.6 bilioni ni mishahara ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Sh78.6 bilioni ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.

Katika taarifa hiyo amesema, fedha za maendeleo zilizoidhinishwa ni zaidi ya Sh88.4 bilioni ambazo kati ya hizo zaidi ya Sh31 bilioni ni fedha za ndani na zaidi ya Sh57.4 bilioni ni fedha za nje.

Ada za mahakama ziwe chini

Akizungumzia ukusanyaji wa maduhuli ya mahakama, amesema katika mwaka wa fedha 2024/25  Mfuko wa Mahakama ulipanga kukusanya maduhuli yenye jumla ya zaidi ya Sh12.5 bilioni.

“Hadi Aprili 22,2025, ilikusanya zaidi ya Sh8.9 bilioni sawa na asilimia 71.22 ya lengo, kwa kuwa maduhuli ya Mahakama yanakusanywa kutoka kwenye vyanzo viwili vya msingi ambavyo ni faini na ada za mahakama.

“Kamati inaishauri Serikali kuhakikisha kuwa viwango hivyo hususan ada za mahakama  vinaendelea kuwa chini na rafiki ili wananchi wengi waweze kupata haki wanayostahili na sio kuwakwamisha,” amesema.

Mwenyekiti wa kamati hiyo aliomba Bunge lipokee, lijadili na kuidhinisha makadirio ya Mapato na Matumizi ya Mfuko wa Mahakama (Fungu 40) kwa Mwaka wa Fedha 2025/26 kama yalivyowasilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria uliotengewa zaidi ya Sh321 bilioni.

Katika fedha hizo, zaidi ya Sh82 bilioni ni kwa ajili ya mishahara ya mahakama, zaidi ya Sh2.6 bilioni ni mishahara ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), zaidi ya Sh143.3 bilioni ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na zaidi Sh93 bilioni ni  kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *