‘Mahaba’ ya Alikiba ni moto wa kuotea mbali 

Dar es Salaam. Tangu amekuwepo katika tasnia kwa miaka zaidi ya 20 na hata kushika kasi kwa matumizi ya teknolojia ya kuweka muziki mtandaoni, hakuna wimbo wa Alikiba uliofanya maajabu kama Mahaba (2023) ingawa haukupewa nafasi hiyo.  

Mahaba ni wimbo uliotengenezwa na Yogo Beats ambaye alishiriki pakubwa katika albamu ya tatu ya Alikiba, Only One King (2021) iliyoshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Albamu  Bora ya Mwaka 2021.

Alikiba alichukua usikivu wa wengi katika Bongo Fleva baada ya kuachia albamu yake, Cinderella (2007) chini ya G Records, kisha zikafuata Ali K4Real (2009) na Only One King (2021) pamoja na EP moja, Starter (2024). 

                      

Baada ya kumalizika kwa mkataba wake na Sony Music, Alikiba aliamua kuwekeza rasmi katika rekodi lebo yake, Kings Music ambayo kwa sasa inawasimamia wasanii wanne, K2ga, Abdukiba, Tommy Flavour na Vanillah. 

Alikiba aliufungua mwaka 2023 kwa kuachia wimbo ‘Mahaba’ ambao ulivuma sana TikTok kutokana na ujumbe wake, huko YouTube hadi leo hajaweka video yake rasmi zaidi ile ya mashahiri, yaani lyric video. 

Hata hivyo, hilo halijauzuia wimbo huo kuandika rekodi zake kwani ndani ya miezi nane tu tayari ulishatazamwa (views) zaidi ya mara 18 milioni na kushika nafasi ya tatu katika orodha ya nyimbo za Alikiba zenye mafanikio katika mtandao huo. 

Kwa mwaka 2024 pekee, video ya Mahaba ilitazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 13 na hadi sasa imefika milioni 36, inatazamiwa kuja kuwa video ya Alikiba iliyotazamwa zaidi YouTube kwani inayongoza sasa ni Mwana (2014). 

                      

Video ya Mwana ambayo ilitoka miaka 10 iliyopita hadi sasa imetazamwa zaidi ya mara 38 milioni, hivyo ni wazi ndani ya muda mfupi ujayo itapitwa na Mahaba na kuwa namba moja kama video ya Alikiba iliyofanya vizuri zaidi YouTube kwa muda wote. 

Hata hivyo, bado Mahaba inashikilia rekodi kama video ya Alikiba aliyotazamwa zaidi YouTube kwa muda mfupi sana ukizipita video za nyimbo kama, Seduce Me (2017) na Utu (2022) ambayo inashika nafasi ya tatu. 

Ikumbukwe Mahaba ni wimbo ulioshinda tuzo ya TMA kama Wimbo Bora wa Bongo Fleva 2023 ukizibwaga nyimbo nyingine kali kama Yatapita (Diamond Platnumz), Baridi (Jay Melody), Honey (Zuchu) na Single Again (Harmonize). 

Ni Alikiba ambaye video ya wimbo wake, Seduce Me (2017) ilitazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 1 ndani saa 37 ikiivunja rekodi ya wimbo wake Diamond Platnumz, Salome (2016) uliofikisha milioni 1 kwa saa 48. 

                      

Mwaka 2017, Alikiba aliandika rekodi kama msanii wa kwanza aliyesainiwa Sony Music Africa kwa video ya wimbo wake (Aje) kutazamwa mara milioni 5 YouTube kitu kilichopelekea lebo hiyo kubwa duniani kumpatia tuzo (plaque). 

Utakumbuka Alikiba aliingia Sony Music baada kuanza kufanya kazi na Seven Mosha ambaye walikutana katika mradi wa One8 uliotoa wimbo, Hands Across The World (2010) ulioandikwa na kutengenezwa na R. Kelly kutokea Marekani ambaye alisikika pia. 

Ni mradi uliokusanya wasanii wengi wa Afrika kwa wakati mmoja, ukimtoa Alikiba, pia walikuwepo Amani (Kenya), Navio (Uganda), 2Face (Nigeria), 4×4 (Ghana), Fally Ipupa (DR Congo), JK (Msumbiji)  na Movaizhaleine (Gabon). 

Chini ya Sony Music, Alikiba alishinda tuzo za kimatifa kama All Africa Music Awards (AFRIMA) 2017 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana Afrika (Aje) ft. M.I (Mr. Incredible), pia alishinda MTV Europe Music Awards  (EMAs) 2016 kama Msanii Bora Afrika.