
Sean ‘Diddy’ Combs (54) ndiyo jina alilopewa na wazazi wake, lakini jina la kutafutia ugali anajulikana kama P Diddy ama Diddy.
P Diddy ambaye ni msanii maarufu wa miondoko ya hip hop nchini Marekani amezuiwa katika gereza linaloitwa ‘The Metropolitan Detention Center (MDC)’ akikabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kingono.
Uamuzi wa kushikiliwa mahabusu kwa gwiji huyo wa muziki nchini humo ulitolewa na Hakimu wa Mahakama ya New York Robyn Tarnofsky baada ya kesi yake kusomwa Jumanne Septemba 17, mwaka huu na kukataa pendekezo la dhamana lililotolewa na mawakili wa Diddy.
Mwanamuziki huyo alishtakiwa kwa ulaghai wa kingono na usafirishaji wa binadamu ili kujihusisha na biashara hiyo ya ngono.
Mbali na hilo, waendesha mashtaka wanadai walikuta dawa za kulevya katika chumba cha hoteli alikokamatwa P Diddy Septemba 16, mwaka huu.
Akiwa mahakamani P Diddy alikana mashtaka yanayomkabili na ombi la dhamana yake kugonga mwamba kisha kupelekwa mahabusu katika gereza hilo maarufu kama ‘The Metropolitan Detention Center (MDC)’.
Kwa mujibu wa Michael Cohen ambaye ni Mwanasheria wa zamani wa Mgombea Urais wa Republican, Donald Trump, gereza la ‘The Metropolitan Detention Center (MDC)’ siyo tu sehemu ya ajabu, pia inatisha kwa msanii huyo aliyezoea kuishi kwenye majumba ya kifahari yaliyopo katikati ya Jiji la Miami na Los Angeles nchini humo.
Cohen akizungumza na CNN amenukuliwa akisema; “Kila anapoamka anatazamana na kuta ngumu zilizonakshiwa rangi nyeupe zinazokinzana na aina ya ujenzi wa majumba yake ya kifahari,”
Akielezea sifa nyingine ya gereza hilo Cohen, alisema kwamba P Diddy anapaswa kufahamu kuwa amezuiwa katika moja ya magereza hatari zaidi ndani ya Jiji la New York, ndani ya gereza hilo ndipo mwanamuziki R. Kelly anapotumikia kifungo chake.
Mbali na Diddy na R. Kelly, wasanii wengine walioishia ndani ya gereza hilo ni pamoja na “Pharma Bro” Martin Shkreli, Mwanamitandao, Ghislaine Maxwell, mtaalamu wa biashara ya safari ya mtandaoni maarufu kama Cryptocurrency’ Sam Bankman-Fried na rapa Fetty Wap.
Hata mtuhumiwa ambaye anatajwa kama kinara wa uuzaji na usambazaji wa dawa za kulevya duniani, Ismael ‘El Mayo’ Zambada Garcia naye amezuiwa katika gereza hilo akisubiria hatma ya kesi inayomkabili.
Gereza hilo siyo tu linasifika kwa kuwa na huduma mbovu ya malazi kwa wafungwa na mahabusu, pia linasifika kwa usalama mdogo dhidi ya wafungwa na kukatika katika kwa umeme mara kwa mara na ndiyo gereza ambalo linahudumia sehemu kubwa ya taifa hilo.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusiana na hali ya usalama katika gereza hilo, msemaji wa jeshi la magereza nchini humo, aliieleza CNN kuwa wanachukulia kwa uzito suala la ulinzi na usalama wa wafungwa na mahabusu kwa kufuatilia kwa karibu na kuhakikisha hakuna ukiukwaji wa hatua za kiusalama dhidi ya mahabusu.
“Ni sehemu ambayo ni ngumu mtu kuhimili kufungwa” ni kauli iliyotolewa na mwanasheria wa P Diddy, Marc Agnifilo alipomweleza hakimu kuwa itakuwa ngumu kwa mteja wake kuhimili kushtakiwa huku akiishi katika gereza hilo.
Gereza hilo lililojengwa mwaka 1990 ili kupunguza msongamano wa wafungwa katika magereza yaliyopo New York, linatumika kuhifadhia mahabusu wanaoshtakiwa katika mahakama mbalimbali zilizoko eneo la Manhattan na Brooklyn nchini humo.
“Asubuhi anaamkia kwenye kitanda cha chuma chenye godoro lenye ujazo wa nchi moja, hakuna mito kwenye selo yenye ukubwa wa hatua 10 tu, naweza kuwahikikisha hili siyo jambo la kufurahisha hata kidogo,” alisema Cohen, ambaye pia amewahi kufungwa katika gereza hilo mwaka 2020.
“Kwenye gereza hilo hakuna hata vitabu vya kusoma naamini atakuwa anapitia wakati mgumu sana sasahivi,” alieleza mwanasheria huyo.
Ni jehanamu ya duniani
The Metropolitan Detention Center ni gereza ambalo linafahamika kama jehanamu ya duniani. Hiyo ni kutokana na historia ya matukio yake, mwezi Juni mwaka huu, mahabusu, Uriel Whyte aliyekuwa akisubiria hukumu ya kesi ya matumizi ya bunduki aliuwawa kwa kuchomwa na kisu akiwa ndani ya gereza hilo.
Mwezi mmoja baadaye, mahabusu mwingine, Edwin Cordero alifariki baada ya kuzuka mapigano ndani ya gereza hilo. Taarifa ya kuuwawa kwa Cordero ilitolewa na mwanasheria wake kuwa mteja wake alifariki baada ya mapigano yaliyoibuka ndani ya gereza hilo aliloliita jehanamu ya duniani.
Mwaka 2019, visa vya kukatika umeme vilitawala ndani ya gereza hilo jambo lililosababisha wafungwa kukaa gizani hadi zaidi ya wiki moja na kuwasababisha kuteswa na baridi kali. Kutokana na changamoto hiyo gereza lililazimika kuwalipa fidia wafungwa 1,600 zaidi ya dola za Marekani milioni 10 kutokana na madhara yaliyosababishwa na baridi hiyo.