Magaidi wakufurishaji waua Waislamu 40 wa Kishia, wajeruhi 30 kaskazini magharibi mwa Pakistan

Kundi la magaidi wakufurishaji wameyafyatulia risasi magari ya abiria yaliyokuwa yamebeba raia Waislamu wa madhehebu ya Shia kaskazini-magharibi mwa Pakistan na kuua karibu watu 40 na kujeruhi wengine 30 katika moja ya mashambulizi mabaya zaidi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni kwenye eneo hilo lenye machafuko.

Maafisa wa serikali ya Pakistan katika eneo hilo wamesema shambulio hilo lilitokea jana Alkhamisi huko Kurram, wilaya iliyoko kaskazini magharibi mwa jimbo la Khyber Pakhtunkhwa.

Abiria hao walishambuliwa walipokuwa wakisafiri katika misafara miwili kutoka mji wa Parachinar kuelekea Peshawar.

Javed ullah Maehsud, afisa mkuu wa utawala wilayani Kurram amesema, misafara miwili tofauti ya Waislamu wa madhehebu ya Shia ililengwa na magaidi katika wilaya hiyo na akaongeza kuwa, washambuliaji wapatao 10 walihusika katika matukio yote mawili, wakifyatua risasi kiholela kutoka pande zote za barabara.

Wanawake wasiopungua sita na watoto kadhaa ni miongoni mwa waliouliwa katika shambulio hilo la kigaidi, huku ripoti zikisema, majeruhi 10 waliokimbizwa hospitalini hali zao ni mahututi.

Ambulansi katika eneo la tukio ikibeba majeruhi wa shambulio la kigaidi

Katibu mkuu wa jimbo la Khyber Pakhtunkhwa, Nadeem Aslam Chaudhry, amesema, “ni janga kubwa na idadi ya vifo huenda ikaongezeka.”

Wimbi la hivi punde la mashambulio ya kigaidi limejiri wiki moja baada ya mamlaka kufungua tena barabara kuu katika eneo hilo baada ya kuifungia kwa wiki kadhaa kufuatia mapigano makali.

Rais wa Pakistan Asif Ali Zardari amelaani vikali hujuma ya kigaidi ya hapo jana na kuamuru pia vyombo husika kuchukua hatua dhidi ya wale waliopanga shambulio hilo.

Mnamo Novemba 7, maelfu ya watu kutoka mji wa mpakani wa Parachinar wa Pakistan walifanya maandamano ya amani kwa lengo la kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo lililoathiriwa na machafuko…/