
SIMBA kimerejea nchini jana kutoka Afrika Kusini ilikoenda kurudiana na Stellenbosch na kufuzu fainali za Kombe la Shirikisho Afrika, lakini kitendo cha Wekundu hao kutinga hatua hiyo kimeleta majanga baada ya mabosi wa Bodi ya Ligi kujifungia ili kuipangua ratiba tena.
Simba ilitoka suluhu na Stellenbosch katika mechi hiyo ya juzi, lakini ushindi wa bao 1-0 nyumbani ikiwa visiwani Zanzibar, umewavusha kwenda fainali na sasa itavaana na RS Berkane ya Morocco, lakini ikiwa na mechi nane mkononi, zikiwamo tano za viporo vya Ligi Kuu zilizopangwa kupigwa ndani ya Mei pamoja na kiporo dhidi ya Yanga katika Dabi ya Kariakoo iliyoahirishwa Machi 8 mwaka huu.
Ratiba ya awali ilikuwa inaonyesha Simba itacheza kuanzia Mei 2-11 dhidi ya Mashujaa, JKT Tanzania, Pamba Jiji na KMC kisha kurudi tena uwanjani sambamba na timu nyingine 15 za Ligi hiyo ili kumalizia raundi tatu za mwisho za kufungia msimu uliopangwa kuisha Mei 25.