Watafiti wa moja ya mashirika ya anga za juu ya Iran kwa kubuni na kutengeneza satelaiti mbili za Kowsar na Hod’hod wameweza kuziingiza kwa mafanikio satelaiti hizo mbili kwenye mzingo wa dunia wenye umbali wa kilomita 500 kwa kutumia roketi ya Soyuz kutokea kituo cha Vostochny nchini Russia, hapo siku ya Jumanne tarehe 5 Novemba.
Hassan Salarieh, Mkuu wa Shirika la Anga za Juu la Iran, amesema baada ya kurushwa kwa mafanikio satelaiti hizo mbili kuwa: “Mwaka huu, tutarusha angani satelaiti nyingine kati ya 5 hadi 7 ndani ya nchi na kimataifa, ambapo baadhi ya urushaji utafanyika kwa kutumia roketi za Simorgh na Qa’em.

Satelaiti ya Kowsar ni bidhaa ya kwanza ya anga za juu ya kampuni ya Omidfaza ya Iran, ambayo inafuata kiwango cha satelaiti za ujazo, ambayo inapunguza muda na gharama ya mchakato wa utengenezaji wake. Satelaiti hiyo ina umri wa kuzunguka kwenye obiti wa miaka 3.5 na inafaa kwa matumizi kama vile ya kilimo na uchoraji ramani. Kwa upande wa pili, Hodhod pia ni setilaiti iliyo na viwango vya satelaiti za ujazo na jukumu lake ni kuunda jukwaa maalum la kutoa huduma za kimataifa za msuala ya mtandaoni. Uzito wa satelaiti ya Hodhod ni kilo nne na urefu wake wa mzunguko wa obiti ni kilomita 500, na umri wake wa obiti ni miaka minne, ambapo imerushwa angani kwa malengo ya kilimo, uchukuaji ramani na masuala ya mazingira.
Sekta ya anga za juu inachukuliwa kuwa kati ya tasnia zenye teknolojia ya hali ya juu. Licha ya vikwazo vyote ilivyowekewa, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kufikia mzunguko wote wa teknolojia ya anga za juu na imepiga hatua kubwa za kimaendeleo katika uga wa teknolojia hiyo katika miongo minne iliyopita. Hivi sasa Iran ni miongoni mwa nchi 10 zenye ujuzi na teknolojia muhimu ya anga za juu duniani, teknolojia ambayo imefikiwa kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na wanasayansi na wataalamu wa Iran katika zaidi ya miongo minne iliyopita.
Ingawa maadui wamejaribu kuzuia maendeleo ya kiuchumi na kisayansi ya Iran, ikiwa ni pamoja na sekta ya anga, kwa kuweka kila aina ya vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran, lakini licha ya vikwazo na mashinikizo hayo yote, Iran imefanikiwa kufikia teknolojia mbalimbali za anga za juu. Kimsingi, tofauti kubwa iliyopo kuhusu mpango wa anga za juu wa Iran na nchi nyingine za eneo la Asia Magharibi ni kwamba Iran imepiga hatua hiyo muhimu ya kiteknolojia kwa kutegemea uwezo wake wa ndani. Kwa kuzingatia nafasi muhimu ya satelaiti katika zama za sasa katika nyanja zote, ikiwa ni pamoja na mawasiliano ya simu, uvumbuzi, ujasusi, mazingira na matumizi mengine mengi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeazimia kuendeleza miundombinu yake katika sekta ya makombora na anga za juu na tayari imekwishapata maendeleo makubwa katika uwanja huo.

Kubuni na kutengeneza roketi za kubeba satelaiti, utengenezaji satelaiti za ndani ya nchi, kuzirusha angani, kupokea data na mwishowe kunufaika na data zilizopokelewa huunda mzunguko kamili wa teknolojia hii. Hivi sasa, ujenzi wa vituo vya kurushia satelaiti unamilikiwa na nchi sita, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafuatia katika hatua ya kuimarisha vituo vya anga za mbali. Iran pia imepiga hatua kubwa katika uwanja wa kurusha satelaiti katika anga za mbali katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na hasa kuhusu suala zima la kutengeneza maroketi ya kubebea satelaiti. Hivi sasa wataalamu wa Iran wamefanikisha juhudi za kudhibiti mzunguko kamili wa teknolojia ya anga za juu, yaani ujuzi wa msingi wa kurusha satelaiti katika kituo cha kurusha na kudhibiti satelaiti na kituo cha kupokea data za satelaiti.
Maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyanja mbalimbali za teknolojia nyeti, ikiwa ni pamoja na teknolojia ya anga za juu, hayakubaliki kwa Wamagharibi, na kwa hiyo wamekuwa wakitoa mashinikizo nakubwa dhidi ya Iran ili isimamishe juhudi zake katika uwanja huo. Hata hivyo, kutokana na kuwa mpango wa anga za juu wa Iran ni wa ndani ya nchi na unaotegemea tejnolojia na wataalamu wa ndani, mpango huo unaendelea kuimarika siku baada ya nyingine licha ya mashinikizo na vikwazo vya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani.