Maeneo 9 ya udhamini mpya Simba

MKATABA wa miaka mitano wenye thamani ya Sh38.1 bilioni ilioingia Simba na mzabuni mpya, Kampuni ya Jayrutty Investment atakayehusika na zoezi la kubuni, kuzalisha na kusambaza jezi na bidhaa nyingine zenye nembo ya klabu hiyo, umegusa maeneo tisa tofauti ambayo yatanufaika moja kwa moja.

Mwenyekiti wa Kamati ya Tenda ya Simba, Dk Seif Muba, alisema ofa ya kampuni hiyo imeishawishi Simba kuwapa haki za matumizi ya nembo yao kwa vile mbali na fedha, inaenda sambamba na manufaa mengi kwa klabu hiyo.

Katika mkataba huo wa miaka mitano, umegusa soka la vijana na timu ya wakubwa kwa kujenga uwanja wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 10,000 hadi 12,000 sambamba na kununua basi jipya.

Mambo mengine ambayo yatainufaisha Simba ni bonasi kwa wachezaji kila mwaka, kumsajili mchezaji yeyote anayetakiwa kikosini hapo.

UDH 01

Pia ujenzi wa ofisi, kituo cha matibabu ya wachezaji, usambazaji wa jezi za viwango vya kimataifa, bila ya kusahau kutoa sapoti katika Simba Day.

Mwanzilishi na Mwenyekiti wa kampuni hiyo, CPA Joseph Rwegasira ametolea ufafanuzi ishu hiyo akisema: “Jambo la kwanza ambalo tunakwenda kutekeleza ni kujenga uwanja wa mpira, uwanja ambao utachukua mashabiki 10,000 hadi 12,000 na tumekubaliana Simba wana uwanja Bunju na tutakwenda kujenga uwanja Bunju lakini kama watakuja na mapendekezo mengine basi tutayafuata.”

Rwegasira aligusia ishu ya usajili na alisema kila mwaka watasajili mchezaji mmoja ambaye Wanasimba wanamtaka huku akibainisha kutokana na ukubwa wa klabu hiyo, hawana budi kununua basi jipya la Irizar kwa ajili ya safari zao.

“Tunajua Simba makao makuu yapo Msimbazi lakini tunakwenda kujenga ofisi za kisasa. Pia kila mwaka tutatoa Sh100 milioni kusaidia kukuza soka la vijana. Pia kila mwaka tutachangia Sh100 milioni kuchangia pre season. Pia tumeahidi kujenga kituo maalumu cha matibabu ya wachezaji.”

UDH 02

Mbali na hayo zile sherehe za Simba Day kila mwaka, kampuni hiyo imesema itaweka mchango wake wa Sh100 milioni.

“Kila mwaka tumekubali kutoa Sh470 milioni kwa wachezaji, uongozi utagawa kwa namna ambayo wataona inafaa na hii fedha itakuwa inaongezeka kila mwaka.

“Mwaka huu na miaka inayofuata mambo yatakuwa mazuri sana, tunakuja kuonyesha tofauti. Tutahakikisha Simba inapata thamani kubwa kulingana na ukubwa wake, ndiyo maana tumewekeza fedha nyingi sana kwenye hili. Kwa mara ya kwanza Simba Sports Club itakuwa klabu ya kwanza Tanzania kuvaa jezi ambayo ni international brand.

Katika ishu ya jezi, imeelezwa Simba itavaa jezi zenye chapa ya kampuni ya Kappa yenye maskani yake Italia. Kampuni hiyo inawadhamini vigogo kama Fiorentina ya Italia na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Katibu Mkuu wa zamani wa Simba Evodius Mtawala ambaye kitaaluma ni mwanasheria alisema mkataba huo unakwenda kuisaidia Simba kupitia nembo yake,ikitokana na uwekezaji wa Bilioni 20 ambao uliwekwa kupitia Mohammed Dewji.

UDH 03

“Kikubwa zabuni ya namna hii inaonyesha ukujai kupitia malengo ya uwekezaji, wakati tunasimamia ule mchakato malengo makubwa yalikuwa kuibadili Simba kuja huku ambako inapita sasa,” alisema Mtawala ambaye alikuwa mmoja wa waliosimamia mchakato wa mabadiliko ya uwekezaji ndani ya Simba.

“Mtu anapokuja kuwekeza kama hivi anakuwa amevutiwa na mambo mengi lakini na yeye analenga kupata faida, maana halisi hapa tunasema Simba inakuwa, wapo watu wanachanganya mambo baada ya mkataba huu kusainiwa wakifananisha na uwekezaji kufanyika kwa Sh20 bilioni wakati mkataba huu una thamani ya Sh38 bilioni.”

“Zile 20 Bilioni ndio sasa zinaleta matunda yake lakini pia kupitia mabadiliko yale yalizisaidia hata klabu zingine kukuwa baada ya kuanza kutamani mabadiliko na sasa wako kwenye safari iliyoanzishwa na Simba kupitia mchakato ule wa uwekezaji.”

Mfadhili wa zamani wa Simba Azim Dewji akizungumzia mkataba huo alisema;

“Kuna suala la kujengwa kwa viwanja kupitia zabuni hii, hili ni muhimu sana, huwezi kuwa klabu namba nne Afrika halafu huna uwanja wako, uwanja huo utakapojengwa Simba itaongeza hadhi yake, ikifanya vizuri itaitangaza zaidi Tanzania na Taifa litanufaika kupitia Simba.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *