
Madrid. Shirikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA) limeridhia ombi la Real Madrid kufunga paa la uwanja wao wa Santiago Bernabéu katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Arsenal.
Uamuzi huo unalenga kuongeza shamrashamra na msisimko kwa mashabiki wao baada ya kupoteza kwa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza.
Paa hilo linalofungika limekuwa sehemu ya maboresho ya kisasa yaliyogharimu takriban dola bilioni 1.27 (sawa na zaidi ya Sh3 trilioni), likiwa ni moja ya maboresho makubwa ya uwanja huo maarufu duniani.
Madrid tayari wamewahi kufunga paa hilo katika mechi kubwa dhidi ya Manchester City na RB Leipzig, wakilenga kuongeza sauti ya mashabiki na kuupa uzito wa kiushindani upande wa nyumbani.
Kwa mujibu wa kanuni za UEFA, uamuzi wa kufunga au kufungua paa la uwanja wakati wa mechi zake za mashindano unapaswa kuidhinishwa na mwamuzi wa mchezo kwa ushauri wa mwakilishi wa UEFA aliye kwenye uwanja.
Paa likifungwa kabla ya mchezo kuanza, halitaruhusiwa kufunguliwa tena isipokuwa pale hali ya hewa itakapolazimisha kufanya hivyo.
Katika mchezo huo wa marudiano utakaopigwa jijini Madrid, Real Madrid watakuwa na kazi ngumu ya kujaribu kufuta kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Arsenal, huku wakitumia kila mbinu kujaribu kugeuza matokeo hayo mbele ya mashabiki wao nyumbani.