
Marekani. Malkia wa Pop duniani kutokea Marekani, Madonna, 66, anaendelea kumuunga mkono mtoto wake wa pili, Rocco Ritchie, 24, katika kazi yake ya uchoraji baada ya kumtembelea katika maonyesho yake huko London, Uingereza.
Staa huyo aliyechukua usikivu wa wengi na kibao chake, La Isla Bonita (1986), katika mfululizo wa picha alizochapisha katika ukurasa wake wa Instagram amesifia kazi ya kijana wake huyo kwa kuiita dawa kamili ya huzuni.
Ikumbukwe Madonna alijaliwa mtoto wake wa kwanza, Lourdes hapo Oktoba 14, 1996 na aliyekuwa mpenzi wake, Carlos Leon, ilikuwa furaha kwake hadi kuandika wimbo ‘Little Star’ unaopakana kwenye albamu yake ya saba, Ray of Light (1998).
Na baada ya kutengana na Carlos mnamo Mei 1997, Madonna alianzisha uhusiano na Guy Ritchie mwaka 1998, ndipo akazaliwa Rocco hapo Agosti 11, 2000 na kubatizwa huko Scotland katika Kanisa Kuu la Dornoch.
Akiwa katika maonyesho ya mwanae Rocco ya Escape to Paris, Madonna amepiga picha nyingi akiwa na kazi alizochora kijana huyo na kuonyesha kuheshimu na kuunga mkono kile ambacho anafanya ingawa sio mara ya kwanza kufanya hivyo.
Hatua hiyo ni baada ya Aprili mwaka huu staa huyo wa kibao, Like A Prayer (1989) kutembelea maonyesho mengine ya Rocco yenye jina la Pack a Punch huko Miami, Marekani akiwa na watoto wake wengine David, 18, Mercy, 18 na mapacha Stella na Esther, 11,.
“Ninafuraha sana kuwa na usiku wa kupumzika ili kufurahia mkusanyiko wa picha za uchoraji wa mwanangu Rocco unaoitwa ‘Pack A Punch’ uliochochewa na wapiganaji wa Muay Thai,” Madonna aliandika katika Instagram.
Katika mahojiano yake na Jarida la W hapo Aprili, Madonna alifunguka kuhusu familia yake na kusema apoenda kwenye ziara, hakuna kitu kinachomletea furaha zaidi ya kujua kwamba wote wanafanya onyesho moja lenye nguvu za ajabu.
“Kwa kweli, mimi ni mama yao kwa hiyo wakati mwingine tunakasirishana. Sisi ni familia ya wasanii lakini pia ni familia, na ndivyo ilivyotokea,” alisema Madonna, mshindi wa tuzo saba za Grammy.
Ikumbukwe Lourdes na Rocco ndio watoto pekee wa kibaolojia wa Madonna, hao wengine wanne amewaasili kutoka nchini Malawi ambao ni David aliyemuwasilia mwaka 2006, Mercy 2009 na mapacha Esther na Stella 2017.
Akiongea na Jarida la People, Madonna alisema Stella na Esther ni kama walikuwa naye kwa wakati wote maana hawakuchukua muda mrefu kuzoea mazingira ya Marekani, na wamejifunza kwamba yeye ndiye mama yao na hakuna kitakachobadilisha hilo.
Madonna ambaye ameuza rekodi zaidi ya milioni 300 akiwa ndiye msanii wa kike aliyeuza zaidi dunani kwa wakati wote, ametoa misaada sehemu mbalimbali duniani baada ya kuanzisha mfuko wake wa hisani, Ray of Light Foundation 1998.