Madereva wa Serikali watajwa vinara wa ‘ku-ovateki’, spidi

Dar es Salaam. Baraka Ludohela (32), ambaye amefungiwa leseni ya udereva kwa miezi mitatu, ni miongoni mwa madereva wa magari ya Serikali wanaotajwa kukaidi sheria za usalama barabarani.

Madereva hao wanalaumiwa kwa kuendesha kwa mwendo kasi, kuyapita magari mengine bila tahadhari na kutotii maagizo ya askari wa usalama barabarani.

Inadaiwa kuwa baadhi yao hukingiwa kifua na viongozi wakubwa, hali inayowafanya wakosekane na mkono wa sheria licha ya kufanya makosa.

Wakati mtazamo wa umma ukiwaona baadhi ya madereva wa magari ya Serikali kama wakorofi barabarani, wenyewe wanasema wanahukumiwa kwa misingi ya upendeleo.

Wanaeleza kuwa licha ya madereva wengi kuvunja sheria za usalama barabarani, wao huonekana zaidi kuwa wakosaji kwa sababu tu wanaendesha magari ya Serikali.

Mjadala kuhusu mwenendo wa madereva hao umeibuka kufuatia hatua ya Polisi Mkoa wa Dodoma kumfungia leseni ya udereva kwa miezi mitatu, Baraka Ludohela kwa kutofuata taratibu za usalama barabarani.

Dereva huyo amefungiwa leseni baada ya tukio la Aprili mosi, 2025 kuonyesha akirudisha gari nyuma na kisha kuendesha kwa kasi kwenda mbele, wakati askari akichukua taarifa za gari lake.

Akiwa katika eneo la Kihonda Darajani, mkoani Morogoro dereva huyo alisimamishwa na trafiki na kuelezwa kosa alilotenda la kuyapita magari mengine sehemu isiyoruhusiwa kisheria, ndipo akafanya tukio hilo.

Tukio hilo limefanyika miezi 18 tangu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipowataka madereva wa Serikali kuwa mfano wa kuigwa kwa wengine akiwasisitiza kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Akiwa mjini Morogoro Oktoba 24, 2023 alipofungua kongamano la Chama cha Madereva wa Serikali, likiwa na kaulimbiu: “Dereva wa Serikali bila ajali inawezekana” Majaliwa alisema kuendesha gari la Serikali haimaanishi umepewa rungu la kuvunja sheria au uko juu ya sheria.

Hali ilivyo mtaani

Lawama dhidi ya madereva hao ya madereva zinakolezwa na Joshua Vitalis, dereva wa magari binafsi anayedai trafiki ni miongoni mwa wanaowapa jeuri madereva wa Serikali kwa kutowachukulia hatua stahiki.

“Dereva wa Serikali anaweza ‘ku –ovateki’ sehemu isiyoruhusiwa, ukimuiga, wewe dereva binafsi utatozwa faini na yeye ataachwa kana kwamba hajakosea. Hiyo ni faini, lakini hata kumsimamisha tu ampe onyo, pia ni nadra kutokea,” amesema.

Amesema wapo wanaopita spidi zaidi ya inayotakiwa kwenye maeneo husika lakini hawachukuliwi hatua na trafiki.

“Hili kosa ufanye wewe dereva wa gari binafsi, ndugu yangu trafiki hawakuachi hivi hivi, hata kama hawatakuandikia faini, basi watakusimamisha na kukuonya, lakini haya magari ya Serikali yenyewe yanapepea tu,” amesema akimaanisha yanatembea kwa kasi.

Dereva mwingine Gaspar Masatu amesema faini nyingi za makosa ya barabarani ni nadra kutozwa kwa madereva wa Serikali, akidai kama wapo wanaotozwa basi ni wachache mno.

“Ule u-Serikali kama unawakingia kifua, ni mara chache sana kuona amefanya kosa na kusimamishwa kuandikiwa faini, na huwa hawaogopi lolote barabarani,” amesema.

Gaspar anaeleza kisa chake alipokamatwa na trafiki Kibaha, mkoani Pwani kwa kosa la kuyapita magari mengine bila tahadhari.

“Nilimuiga dereva wa STK (gari la Serikali) aliyekuwa mbele yangu, tukiwa tumeongozana, mimi nilipigwa mkono yeye akaachwa kana kwamba yupo sahihi, liniumiza. Nilipigwa faini peke yangu, nikamuuliza trafiki mbona tumetanua wawili, mwenzangu kaachwa, akanijibu nisimfundishe kazi,” amesema.

Baadhi ya trafiki waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti kwa sharti la kutokutajwa majina kwa kuwa si wasemaji, wameeleza madereva wa Serikali wengi hufanya makosa makusudi wakiamini hawezi kuchukuliwa hatua.

Kwa mujibu wa askari hao, wengi wa madereva wa Serikali wanaendesha kwa spidi kupitiliza, wanaongoza ku- ovateki na hawatii amri za askari wa usalama barabarani.

“Huwa na dharau wakiamini hawawezi kufanywa chochote,” amesema trafiki mmoja aliyekuwa kituo cha kazi mkoani Morogoro.

Trafiki mwingine katika eneo la Mbezi, Dar es Salaam amesema wengi wao huwa na dharau kwa askari na hawazingatii alama za usalama barabarani.

“Mfano wa kawaida tu, ajali nyingi zinatokea. Ukilinganisha zile za magari ya kawaida na za yale ya Serikali, nyingi za magari ya Serikali zinapotokea huwa ni ajali kweli-kweli, unafikiri ni kwa nini?” amehoji akibainisha namna wengi wa madereva hao wasivyozingatia alama za usalama barabarani.

Hata hivyo, dereva wa gari la Serikali aliyeomba kutotajwa jina amelitetea kundi hilo akisema kuna sababu kadhaa zinazochangia waonekane wanaongoza kuvunja sheria za usalama barabarani.

“Makosa makubwa yanayotukuta ni ‘ku-ovateki’ eneo lisiloruhusiwa na kutembea kwa spidi zaidi, mengine ni yale ya kawaida ambayo humkuta dereva mwingine yoyote.

“Huwa tunalazimika kutembea mwendo mkali nyakati zingine kwa ajili ya kuwahi kumfuata bosi au kumuwahisha, hivyo kulazimika ‘ku- ovateki’ na kutembea spidi kali, lakini kwa uangalifu na umakini,” amesema.

Amesema ni ngumu kwa madereva wengi wa Serikali kutembea spidi 50 kwenye eneo linalotaka hivyo kutokana na uwezo wa magari yao na haraka walizonazo, akidai wengi spidi ya kawaida kwao kama barabara ni nyeupe (haina magari) ni kuanzia 100 na kuendelea.

“Hakuna bosi anayekwambia uvunje sheria za barabarani, wengi tunavunja kwa ujeuri tu wa madereva, tukiamini ukikamatwa utapiga simu na kuachiwa na matrafiki wakiona ni gari la Serikali hawashughuliki na wewe,” amesema.

Dereva mwingine wa Serikali amesema wanatajwa zaidi kukiuka sheria za usalama barabarani kutokana na chuki iliyojengeka baina yao na trafiki.

“Siyo kwamba sisi tu ndio tunavunja sheria za usalama barabarani, hapana. Lakini shida inaonekana kubwa kwetu kwa sababu kuna chuki. Sisi tunaposimamishwa barabarani huwa hatutoi fedha zozote tofauti na wenzetu wa magari binafsi, ndiyo maana unaona kosa la mmoja linakuzwa,” amesema.

Kuhusu kutosimama wanaposimamishwa na trafiki amesema: “Kuna wakati unaweza kukamatwa na trafiki, ukapiga simu agizo likatoka uachiliwe, hiyo inatuwekea kisasi na trafiki, ikitokea askari akampata dereva ambaye hana uwezo wa kupiga simu huwa anamshughulikia kweli-kweli,” amesema.

Kauli ya Polisi, Serikali

Aprili 3, 2025 katika rambirambi baada ya ajali iliyotokea Mamba Msangeni, wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro iliyosababisha vifo vya watu wanane, Rais Samia Suluhu Hassan aliwasihi watumiaji wote wa barabara kuendelea kuwa waangalifu na kufuata sheria za usalama barabarani.

Alisema: “Nasisitiza vyombo vyetu ya usalama barabarani kuendelea kusimamia sheria kwa makini ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika, ikiwemo kufuta kabisa leseni kwa madereva wenye makosa yanayochukua uhai wa Watanzania wenzetu.”

Takwimu za Jeshi la Polisi za mwaka 2024, zinaonyesha ajali za barabarani zilizotokea kati ya Januari hadi Desemba zilikuwa 1,735 kati ya hizo ajali 1,198 zilisababisha vifo.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, William Mkonda alipotafutwa na Mwananchi leo Aprili 7 ili azungumzie mitazano kuhusu madereva hao, simu yake ilipokewa na msaidizi wake aliyejitambulisha Sajenti Noel akasema kamanda yuko msibani akielekeza atafutwe msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, ambaye hata hivyo simu yake iliita bila kupokewa.

Hata hivyo, alipoulizwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema taratibu za barabarani zinafahamika na madereva wote wanazifahamu.

“Kule barabarani kuna askari wa usalama barabarani na sheria zipo kwa ajili ya kusimamia usalama, hao wanaosema kuna wakubwa wapo nyuma yao (madereva), wamtaje ni mkubwa gani, kisha urudi kwangu,” amesema Msigwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *