Madereva Moshi walia na mashimo eneo la reli

Moshi. Watumiaji wa barabara ya Tembo, Manispaa ya Moshi, wamelalamikia uwepo wa mashimo katika barabara hiyo eneo ambalo kuna kipande cha njia ya reli kinapita kuelekea katika matanki ya mafuta ya iliyokuwa kampuni ya BP.

Kipande hicho cha reli kilijengwa mahsusi na Serikali wakati huo Shirika la Reli Nchini (TRC), likisafirisha mafuta kwa kutumia mabehewa maalumu ya kusafirisha mafuta, lakini usafirishaji huo ulikoma safari za abiria zilipokoma mwaka 1994.

Kutokana na kusitishwa kwa usafirishaji huo wa mafuta, kipande hicho kilizibwa kabisa na lami mpya iliyojengwa baadaye, hadi mwaka 2017 ilipochimbuliwa, lakini eneo hilo halikurekebishwa vizuri kuruhusu vyombo vya moto kupita bila matatizo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi Februari 25, 2025 wananchi hao wamesema eneo hilo limekuwa korofi kutokana na mashimo na kusababisha magari, bajaji na pikipiki kupita kwa shida katika kipande hicho cha barabara.

Hata hivyo, akizungumzia malalamiko hayo, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (Tarura) Wilaya ya Moshi, Africano Orota amesema eneo hilo wanalifahamu na tayari upo mpango wa kulifanyia marekebisho.

“Tupo kazini, kazi ya kuziba mashimo inaendelea sasa hivi, tumeshafanya maeneo mengi ikiwemo barabara ya kwenda Uru na leo tupo barabara ya kuelekea KCMC, tukimaliza tutahamia kwenye eneo hilo.”

“Wananchi wawe na subira, hapo tunapafahamu hivyo ni lazima tutaziba mashimo hayo na barabara hiyo itapitika bila shida wala usumbufu,” amesema.

Kauli ya Tarura imepokelewa kwa furaha na madereva lakini kwa tahadhari.

Wakitoa malalamiko yao madereva wanaotumia barabara hiyo, wamesema kilio cha eneo hilo kimekuwa cha muda mrefu, kwani iliwahi kurekebishwa lakini kwa kulipuliwa na bila ubora na changamoto kubwa ikaendelea kubakia hasa kipindi cha mvua.

Mmoja wa wananchi hao, Rodrick Mushi amesema barabara hiyo inayounganisha kata za Bomambuzi, Pasua na Kaloleni imekuwa na changamoto ya mashimo katika eneo la reli inayoenda viwandani, ambapo tatizo hilo limedumu kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi.

“Hii barabara kama unavyoiona ni muhimu ambayo inaunganisha kata za Pasua, Bomambuzi, Kaloleni lakini pia kuelekea Mabogini nje ya Manispaa ya Moshi, lakini ukiangalia hapa kwenye hii reli pameharibika sana,” amesema.

“Hili tatizo sio la leo wala jana, hili limedumu kwa muda mrefu na madhara yake ni makubwa kwa vyombo vya usafiri. Baada ya mwezi tu ukipita na gari hapa au bajaji lazima uende gereji.”

“Magari yanaharibika na wakati mwingine magari makubwa ya mizigo yanaharibikia hapa kwa sababu ya ubovu wa hii miundombinu ya hapa, lakini pia kwa sasa tunaelekea kwenye kipindi cha mvua, mashimo yatakuwa makubwa zaidi na uharibifu utakuwa mkubwa kwani pamekuwa na mitaro mikubwa kutokana na kuachwa muda mrefu bila kurekebishwa,” amesema.

Aidha amesema, “tuombe mamlaka husika (Tarura) ilivalie njuga hili kwani ni eneo dogo na linaweza kufanyiwa marekebisho na barabara hii ikapitika vizuri kwani kutokana na uharibifu uliopo kwa sasa, vyombo vya moto vinalazimika kupita upande mmoja jambo ambalo pia ni hatari na linaweza kusababisha ajali.”

Deusdedit Kilian, amehoji inakuwaje eneo hilo linapitika kwa shida kutokana na reli kupita katikati wakati mita 10 tu kutoka hapo kuna reli nyingine inapita kutoka Moshi kwenda Arusha na Tarura walitengeneza vizuri kulinganisha na eneo hilo.

Kwa upande wake, Vicent Mkene mkazi wa Bomambuzi, amesema eneo hilo la reli ambako ni kwenye kona ni hatari na panaweza kusababisha madhara makubwa kama jitihada za kuparekebisha hazitachukuliwa mapema na Tarura.

“Hii barabara kwenye kona katika reli inayoingia viwandani imeharibika sana, tunashauri irekebishwe maeneo haya kwani kwa hali hiyo inahatarisha usalama wa watumiaji.”

“Lakini Tarura wasiishie tu hapa, waikague barabara yote ya Tembo kuelekea kule kwenye Hoteli ya Springlands kule kwa Zara. Pale karibu na tuta kubwa kuna mashimo yana zaidi ya miaka minne hayajawahi kuzibwa,” amesema.

Naye Ismail Ayubu amesema, “hiki kipande hapa kinatupa changamoto kubwa, kwa sababu hapa ni eneo la reli imepita lakini huwezi kujua ni reli au kalavati la maji kwani mvua ikinyesha tu kidogo maji yanajaa hapa kote. Tuombe waje watengeneze hili eneo.”