
Mbeya. Katika kuendelea kuboresha mazingira bora kwa wananfunzi shuleni ni pamoja na kuwa na mazingira bora ya kujifunzia ikiwemo kupata utulivu utakaowasaidia kuona elimu ni sehemu ya maisha yao na sio jukumu.
Hayo yamedhiirishwa na Benki ya Stanbic Tanzania kwa kutoa madawati 100 na miche 200 ya miti kwa shule za mkoa wa Mbeya.
Madawati hayo yatagawanywa kati ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Tulia na Shule ya Sekondari ya Nsalaga, na sherehe ya makabidhiano imefanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Tulia.
Hatua hiyo inaonyesha dhamira ya Stanbic kusaidia elimu na kuhamasisha uelewa wa uhifadhi wa mazingira nchini Tanzania.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mjini, Beno Malisa ameongoza sherehe hizo, akiishukuru Stanbic kwa jitihada zake za kuinua jamii kupitia mipango ya Uwajibikaji wa Kijamii (CSR).
“Sisi kama serikali tunatambua mchango mkubwa wa Stanbic Bank kama mshirika muhimu katika kuunga mkono elimu. Pamoja na kutoa rasilimali muhimu kama madawati na miche ya miti, tunatambua pia uhitaji wa vifaa vya kidijitali kama vile kompyuta.
Vifaa hivi ni muhimu katika kuwawezesha walimu na wanafunzi kuunganishwa na dunia na kuendana na maendeleo ya teknolojia, hivyo kuwaandaa kwa mazingira ya kisasa na ushindani.”
Naye, Paul Mwambashi, Meneja wa Tawi la Benki ya Stanbic Mbeya, amesisitiza kujitolea kwa benki hiyo katika maendeleo ya jamii.
“Katika Stanbic Bank, tunaamini katika kusaidia jamii tunazozihudumia, na tunajivunia kutoa rasilimali zinazochangia mazingira bora ya kujifunza na ya kijani kibichi,” amesema.
“Msaada huu ni sehemu ya dhamira yetu ya kuleta athari chanya na yenye kugusa maisha.”
Msaada huo unajumuisha mchanganyiko wa miche ya matunda na miti ya kivuli, ikilenga kuunda utamaduni wa kuhifadhi mazingira miongoni mwa wanafunzi na jamii nzima. Hadi sasa, uwekezaji wa Stanbic katika miradi ya maendeleo ya jamii umefikia Sh312 milioni, ukigusa zaidi ya watu 104,660 nchini Tanzania.
Madawati yaliyotolewa yamezalishwa ndani ya mkoa wa Mbeya, ikionesha dhamira ya benki hiyo ya kusaidia biashara za ndani na kukuza uchumi wa ndani wa jamii.
Shughuli za CSI za benki hiyo zinajikita katika maeneo muhimu kama elimu, afya, uhifadhi wa mazingira, na maendeleo ya jamii.