Dar es Salaam. Baada ya kusambaa taarifa zikidai kuwa Abiud Onesmo aliyekuwa mshiriki wa mashindano ya kusaka vipaji msimu wa 15 (BSS) , alijing’oa kwenye mashindano hayo kutokana na kutamkiwa maneno yasiyofaa. Hatimaye mwandaaji wa mashandano hayo Madame Rita amekanusha taarifa hizo.
Madame Rita akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, amesema Abiud aliondoka kwenye mashindano hayo kwa hiyari yake hakuna aliyemfukuza.

“Abiud aliamua kuondoka mwenyewe alipigiwa simu na mpenzi wake. Akisema anaumwa baada ya kufika kule mpenzi akamwambia alikuwa amemkumbuka tu. Akataka tena kurudi kwenye mashindano nikimwambia huo mchezo hautawezekana.
“Nilipigiwa sana simu na mmoja ya watu wake wa karibu akasema anahitaji arudishwe. Nikamwambia sio sawa, sababu haya ni mashindano na sio sehemu ya mchezo mchezo. Lakini aliondoka mwenyewe na aliongea mbele ya kamera, na mimi nilivyoambiwa na mkuu wa kambi nilimruhusu kwa sababu huwezi kumlazimisha mtu kitu hataki kufanya,” amesema Madame Rita.
Hata hivyo Rita ameongezea kuwa mwenendo wa Abiud ulikuwa mzuri kwenye mashindano hayo, hivyo angeweza kufika kumi bora ya BSS msimu huu.

“Yaani hizo komenti za BSS kupendelea zingekuwa hazipo ningejiuliza nakosea wapi. Ningejiuliza kuwa kuna kitu sifanyi sawa kwa hiyo nazipenda, bila hizo tusingefika hapa tulipo zinatujenga wala hazinibabaishi ukiona hazipo kama hizo basi ujue kuna kitu hakipo sawa,” amesema Madame Rita.

Taarifa za Abiud kujitoa kwenye mashindano ya BSS zilianza mapema Februari, 2025. Huku zikitolewa sababu tofauti tofauti ikiwemo ya kupewa maneno mabaya na waamuzi wa shindano hilo akiwemo S2kizzy, aliyemwambia kuwa ana wenge.