Madaktari wawili Pemba wasimamishwa kwa kutumia lugha chafu kwa wagonjwa

Pemba. Wizara ya Afya Zanzibar, imewasimamisha kazi kwa muda wa mwezi mmoja madaktari wawili katika Hospitali ya Abdalla Mzee Kisiwani Pemba kwa tuhuma za kutoa lugha isiyofaa kwa wagonjwa.

Waliosimamishwa kazi ni Daktari Muuguzi Msaidizi daraja la tatu, Fatma Ali Makame na Muuguzi Msaidizi na Daktari wa Binadamu, Saleh Khalfan.

Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Afya Pemba, Khamis Bilali Ali, ametoa taarifa hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Chakechake, kufuatia tukio la kijana aliyepata ajali ya bodaboda, Said Amour Hassan, na kulazwa katika hospitali hiyo lakini alikumbana na kauli za kejeli.

Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia Januari 18, 2025. Awali, kijana huyo alianza kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Chakechake Vitongoji na baadaye kufikishwa Hospitali ya Rufaa Mkoani kwa matibabu zaidi.

“Baada ya kufikishwa katika hospitali hiyo, alianza kupatiwa matibabu vizuri lakini baada ya kuzimika kwa umeme, mama wa kijana huyo alilalamika kuhusu kauli za wafanyakazi hao,” amesema Bilali.

Cha kusikitisha, madaktari hao wa zamu waliokuwa wakimuhudumia walionyesha dharau na kutoa lugha isiyokubalika, jambo lililoifanya wizara kuchukua hatua ya kuwasimamisha kazi watumishi hao,” ameongeza.

Aidha, amesema watumishi hao walikiuka sheria za utumishi wakati walipaswa kutoa huduma zinazokubalika na sio kuwatolea maneno watu waliokwenda kufuata huduma.

“Kutokana na kadhia hiyo, Wizara ya Afya imelazimika kuchukua hatua za kisheria kwa watumishi hao kwa kuwa wasimamie kazi kwa mwezi mmoja ili kuwa ni fundisho kwa watumishi wengine,” amesema Bilali.

Amesema hatua nyingine ni kuwapeleka kwenye Baraza la Wakunga na Mabara ya Madaktari kwa hatua za kinidhamu. “Wizara haikuridhishwa na kitendo hicho kwani sio kitendo cha kiungwana kutoa lugha isiyoridhisha kwa mama wa kijana huyo ambaye sasa ni marehemu,” ameasema Bilali.

Hata hivyo, wizara imetoa onyo kali kwa watumishi wanaotoa lugha chafu wakati wa utoaji wa huduma na itaendelea kuchukua hatua kwa wale watakaobainika, huku ikiwataka wananchi kutoa ushirikiano katika kukomesha kadhia hiyo.