Madaktari watoa taarifa mpya hali ya Papa Francis

Rome, Vatican. Hali ya kiafya ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis, imeendelea kuwa ya wasiwasi baada ya kushindwa kupumua kutokana na makohozi kuziba njia za hewa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Vatican, madaktari walilazimika kutumia mashine kuondoa makohozi hayo na kumuweka tena kwenye mashine ya kumsaidia kupumua. Hata hivyo, licha ya hali hiyo, Papa Francis bado anajitambua na yuko katika fahamu zake, huku madaktari wakiendelea kumfanyia uchunguzi zaidi.

Hali hiyo ni mwendelezo wa changamoto za kiafya zinazomkumba kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 88 tangu alipopelekwa na kulazwa katika Hospitali ya Gemelli, Roma, mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa Vatican, tatizo hilo lilitokana na makohozi kujikusanya kwenye mirija ya hewa na kusababisha kubana.

Jana mchana, Papa Francis aliwekewa mashine ya oksijeni kupitia barakoa ili kumsaidia kupumua. Pamoja na changamoto hiyo, Vatican ilisema kiongozi huyo wa kiroho ameendelea kuwa macho na kushirikiana na madaktari.

Taarifa za Vatican zilisema hali hiyo ilidhibitiwa na  kwa sasa Papa Francis anapumzika. “Ilikuwa alasiri ngumu,” vyanzo vya Vatican viliripoti, vikieleza kuwa tatizo la upungufu wa hewa lilidumu kwa muda mchache kabla ya kudhibitiwa.

Kwa mujibu wa madaktari, mkusanyiko wa makohozi umetokana na nimonia hali inayosababisha kukohoa na kubana kwa mirija ya hewa. Profesa wa tiba ya magonjwa ya mapafu na huduma ya wagonjwa mahututi kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, Dk Theodore Iwashyna, aliiambia CNN kuwa kifaa cha Bronchoscopy kinatumiwa kwa nadra kusaidia kuondoa makohozi yaliyoziba njia ya hewa.

“Kama mgonjwa ni mahututi na anahitaji msaada wa kupumua, lazima kuwe na sababu madhubuti ya kufanya hivyo,” alisema Iwashyna, akibainisha kuwa mkusanyiko wa makohozi si ishara nzuri kwa mgonjwa mwenye nimonia.

Vipimo vya damu vyabaki vilevile

Vatican ilibainisha kuwa vipimo vya damu vya Papa Francis bado vipo sawa, lakini hali yake inahitaji uangalizi wa karibu. Daktari wa Dharura kutoka Boston, Marekani, Dk Jeremy Faust, alisema matumizi ya Bronchoscopy yana lengo la kusaidia utoaji wa oksijeni kwa kiwango cha wastani.

Matibabu haya, kwa mujibu wa Dk Faust, hutumika ikiwa mgonjwa hajafikia kiwango cha kuhitaji msaada wa upumuaji wa moja kwa moja au ameamua kuepuka matumizi ya mashine za kupumulia.

“Siku chache zijazo ni muhimu kwa afya ya Papa Francis,” alisema Dk Panagis Galiatsatos, mtaalamu wa magonjwa ya mapafu kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, akiongeza kuwa wagonjwa wa umri na hali kama yake huhitaji angalau mwezi mmoja hospitalini na mwezi wa kupumzika kwa kila wiki aliyolazwa.

Papa Francis amelazwa katika Hospitali ya Gemelli tangu katikati ya Februari, akipambana na nimonia kwenye mapafu yote. Hili ni jaribio lake la nne la kulazwa hospitalini tangu alipochaguliwa kuwa Papa mwaka 2013.

Familia na waumini waendelea kumuombea

Binamu yake, Carla Rabezzana, aliiambia CNN kuwa familia yao imejawa na hofu kuhusu mwenendo wa afya ya Papa Francis.

Alisema hawajawasiliana moja kwa moja naye bali hupata taarifa kupitia vyombo vya habari. Simu yao ya mwisho kuzungumza naye ilikuwa siku ya Krismasi.

“Kwa kumjua yeye, anakabiliana na kila jambo kwa ujasiri mkubwa na utulivu,” alisema Rabezzana.

Katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, mjini Vatican, maaskofu, masista na mamia ya waumini wameendelea kukusanyika kila jioni kumuombea kiongozi huyo wa kiroho. Jana usiku, Kardinali Robert Prevost aliongoza sala ya rozari kwa ajili ya Papa Francis.

Kutokana na hali yake, Papa Francis hatoongoza ibada ya Jumatano ya Majivu inayoashiria mwanzo wa kipindi cha Kwaresima. Hii ni mara ya pili tangu kuwa Papa ambapo hatashiriki ibada hiyo, na badala yake, Kardinali anatarajiwa kuiongoza kwa niaba yake.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.