
Katika kijiji cha Koono, Kaunti ya Turkana nchini Kenya, kijana wa miaka 12 amekaa kwenye kiti huku akiwatazama vijana wenzake wakicheza kandanda.
Anauguza mguu wake uliofanyiwa upasuaji kurekebisha tatizo lililosababishwa na jeraha alilopata alipokuwa akicheza.
“Ilikuwa Januari mwaka jana ambapo alikuwa akicheza na wenzake, kwa bahati mbaya akaanguka na mguu wake wa kulia ukavunjika,” anaeleza baba yake.
Kwa miezi kadhaa tokea wakati huo, baba huyo alikuwa akimbeba mwanawe kumpeleka katika kliniki moja iliyoko kilomita chache kutoka kijijini mwao, lakini hakuwa akipokea matibabu.
“Alikuwa akipokea tu huduma za kupunguza maumivu na kufungwa au kubadilishwa bendeji. Hii ni kwa sababu kliniki hiyo haina uwezo wa kuendesha shughuli za upasuaji,” anasema.
Kwa hivyo, wazazi wake Lomong walilazimika kusafiri kwenda mjini Lodwar mara kadhaa kufuatilia ombi la kutaka mtoto wao afanyiwe upasuaji katika hospitali yenye uwezo wa kufanya utaratibu huo.
“Umbali wa kijiji chetu hadi katika hospitali hiyo ni takriban kilomita 70, na gharama ya usafiri ni ya juu. Aidha, kila tulipokuwa tukienda huko, tulikuwa tukipata foleni ndefu,” anaongeza.
Hospitali hiyo ilikuwa ikikumbwa na tatizo la uhaba wa wahudumu wa kutosha, huku idadi ya wagonjwa waliokuwa wakisubiri kufanyiwa upasuaji pia ikiwa kubwa.
Iliwalazimu kusubiri kwa muda huu wote kabla ya mwanawe kufanyiwa upasuaji huo ambapo kwa sasa anaendelea kupata nafuu.
Uhaba wa madaktari
Tatizo la uhaba wa madaktari wa upasuaji sambamba na vifaatiba vyake, halikumbi tu Kaunti ya Turkana au Kenya, ni shida ya bara la Afrika.
Takwimu zinaonyesha zaidi ya asilimia 90 ya raia wa mataifa ya Afrika yaliyo kusini mwa jangwa la Sahara, hawawezi kufikia huduma hata sahihi ya upasuaji.
Hii ndiyo ilikuwa mada kuu kwa madaktari, watafiti na wadau katika sekta ya matibabu ya upasuaji barani walipokutana Februari jijini Kigali, katika kongamano la kwanza la matibabu ya upasuaji barani Afrika.
Kulingana na wataalamu, hali ya huduma za upasuaji barani ni ya kutatanisha, kwani mbali na kuwa ni duni, bado haifadhiliwi vilivyo, huku mapengo katika miundombinu ya misingi yakizuia mamilioni ya watu wasiweze kufikia huduma hizi.
Ripoti ya Benki ya Dunia inaonyesha kwamba idadi ya madaktari wa upasuaji barani Afrika ni sawa na daktari mmoja kwa kila idadi ya watu 200,000. Idadi hii ni ya chini zaidi ikilinganishwa na viwango vinavyokubalika vya madaktari wa upasuaji 76 kwa kila watu 200,000.
Hata hivyo kwa Tanzania idadi madaktari ya madaktari hao ni 600 kwa mujibu wa Rais wa Chama cha Madaktari wa Upasuaji, Dk Amaani Malima.
Kwa mujibu wa Abebe Bekele, Profesa wa upasuaji na Naibu Chansela wa masuala ya akademia na utafiti katika Chuo Kikuu cha Global Health Equity, janga hilo linatokana na kutokuwepo kwa msingi wa kustawisha wataalamu katika sekta hiyo.
“Katika mataifa mengi hapa barani hakuna mfumo unaohakikisha mafunzo ya wataalamu hawa,” anasema.
Dk Charles Kabetu, mtaalamu wa nusukaputi na ofisa wa matibabu anayesimamia eneo la Afrika Mashariki, anasema upungufu huu hauathiri tu madaktari wa upasuaji, bali pia wahudumu wote wanaohusika. Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), mataifa ya Afrika yanaendelea kukumbwa na uhaba wa wahudumu wa upasuaji, huku baadhi ya nchi zikiwa na wahudumu 2.3 kwa kila watu 1,000.
“Uhaba huu unafanya hali kuwa mbaya zaidi, na hivyo, kuzuia hospitali zisitoe huduma ipasavyo,” anaongeza Dk Kabetu.
Hali ni mbaya zaidi katika maeneo ya vijijini, huku madaktari na wahudumu wengi wa upasuaji wakifanya kazi mijini, suala ambalo limeacha hospitali za maeneo ya vijijini bila wataalamu.
“Wengi hukimbilia hospitali za mijini, hasa ikizingatiwa zina vifaa na miundombinu bora zikilinganishwa na zile za vijijini,” anaeleza Profesa Bekele.
Nini kimechangia uhaba huo? Kulingana na Dk Bekele, tatizo kuu limekuwa uhamaji wa wataalamu.
“Wahudumu walio na ujuzi wa juu hapa Afrika wanaendelea kutafuta kazi ughaibuni, siyo tu kwa sababu ya pesa, bali pia, mazingira duni ya utendajikazi,” anaeleza Dk Stephen Okelo, mtaalamu wa nusu kaputi na mkufunzi katika shirika la Global Heart Association.
Kwa mfano, utafiti uliochapishwa Januari 2023 katika jarida la Global Public Health Journal, kati ya mwaka wa 2008 na 2021, takriban madaktari 35,000 waliondoka nchini Nigeria na kuhamia nchini Uingereza pekee.
Kwa wahudumu, idadi inasikitisha hata zaidi, kwani kati ya mwaka wa 2002 na 2021, zaidi ya wahudumu 60,000 kutoka nchini humo walihamia nchini Uingereza.
Madaktari na wataalamu wa kimatibabu wanasisitiza suala la miundo ya msingi na teknolojia liangaziwe kuondokana na uhaba.
“Lazima serikali za Afrika ziwekeze kiwango kikubwa cha pesa katika teknolojia, miundo ya misingi na mafunzo kwa wahudumu,” anaeleza Dk Okelo.
Kathy Magee, mwanzilishi mshirika wa shirika la Operation Smile, linalotoa huduma za upasuaji katika mataifa kadhaa barani, anasema sharti serikali za Afrika ziungane na mashirika ya kimataifa na jamii.
“Hili siyo tatizo linaloweza kutatuliwa na mtu mmoja,” anaongeza.
Makala haya ni kwa hisani ya Gazeti la Taifa Leo