Machi imenikumbusha misiba ya wanamuziki

Dar es Salaam. Mwezi Machi umepita, lakini ni mwezi wenye kumbukumbu nyingi chungu kwa ndugu, marafiki na wapenzi wa muziki wa dansi Tanzania na Afrika. 
Wanamuziki wengi maarufu waliaga dunia Machi.

Kati ya wanaonijia kichwani ni wanamuziki gwiji,mtunzi muimbaji na mpiga gitaa Marijani Rajabu aliyefariki Machi 23, 1995,  mtunzi na muimbaji  TX Moshi William, naye alifariki Machi 29, 2006.

Nimemkumbuka pia Andrew Damas mpiga gitaa wa miaka mingi wa bendi ya Polisi, ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa TX Moshi William kiasi cha watu wengine kudhani ni ndugu. Andrew alifariki tarehe ileile aliyofariki rafiki yake Moshi William, Machi 14. Vifo vyao vilipishana miaka kumi na minne.

Mwanamuziki mwingine mkongwe, aliyekuwa muimbaji na mpigaji wa vyombo mbalimbali  Lazaro Bonzo alifariki Machi 19 huko Morogoro. Bonzo ambaye historia yake ya muziki ilimpitisha katika bendi maarufu kama Morogoro Jazz Band SuperVocano, Orchestra Lombe Lombe, Kurugenzi Jazz ya Arusha, hatimaye alirudi Morogorona kuendelea na muziki mpaka mauti yalipomkuta. Bonzo alizikwa kwao nje kidogo ya mji wa Morogoro.

Magwiji wengine watatu waliofariki Machi, ni  Aurlus Mabele aliyefahamika kwa uchezaji na uimbaji wake katika muziki wa soukus, Manu Dibango, mpiga saksafoni na muimbaji aliyefahamika kwa upigaji wa muziki aina ya  Makossa. 

Katika safari yake ya muziki Manu Dibango ambaye ni jina lake halisi ni Emanuel N’Djoke Dibango alikuwa raia wa Cameroon lakini alisafiri kwenda Congo na kujiunga na kundi la African Jazz na kurekodi nao nyimbo kadhaa.

Manu Dibango pia alishiriki na kupanga vyombo katika nyimbo za Franklin Boukaka kama vile Le Bucheron Africa na Nakoki. Aurlus Mabele na Manu Dibango wote walifia Ulaya kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa Corona. 

Hakika kumbukumbu hizi zinanikumbusha hata wanamuziki wengine ambao hawakufariki Machi. Wimbo  uitwao Ndaya ambao wanamuziki wengi wa kike huuimba katika maonyesho yao hata leo, ulirekodiwa na  Bi M’pongo Love. 

Mwanamuziki huyu aliyekuwa na sauti nzuri aliamua kurudi nchini Kongo Julai 1989 baada ya kuwa nje ya nchi kwa miaka minne. Aliporudi aliwaahidi wapenzi wa muziki wake kuwa amerudi na mambo mapya na nguvu mpya, akamtambulisha mwanaye mchanga kwa wapenzi wake na  akafanikiwa hata kutoa album na kuwaahidi wapenzi wa muziki wake kuwa angeanza maonyesho baada ya muda mfupi.

Wapenzi wake walisubiri kwa hamu, tena wakitegemea angeanza maonyesho akishirikiana na mpiga saksafone mashuhuri Empopo Loway ambaye ndiye alimfanya afahamike katika ulimwengu wa muziki, na ndiye aliyekuwa mtunzi na mpangaji wa vyombo wa wimbo Ndaya. 
Haikuwa hivyo, Mpongo Love aliaanza kuumwa na muda mwingi alikuwa hospitali hatimaye  Januari 15, 1990, Mpongo Love alifariki. 

Wakati wapenzi wa muziki wa mwanamama huyu wakishangaa, siku sita tu baadaye mwalimu wa Mpongo Love, Empopo Loway naye alifariki kutokana kile kilichodaiwa kuwa ni Kifua Kikuu kilichokuwa kikirudia rudia kutokana Loway kujali zaidi kazi kuliko matibabu.
 Empopo Loway aliyejulikana pia kwa jina la Deyesse alikuwa mmoja ya wanamuziki wa TP OK Jazz kuanzia mwaka 1974.
 
Wakati akiwa mwanamuziki wa TP OK Jazz, alimsaidia Mpongo Love kwa kumtungia nyimbo na kisha kumuingiza studio. Saksafon yake na sauti ya Mpongo Love zinasikika vizuri katika wimbo maarufu wa Ndaya.

Wiki chache baada ya misiba hii miwili, vigogo wawili waliokuwa kati ya wanamuziki wa awali kabisa katika OK Jazz  nao walifariki.

Isaac Musekiwa mpiga saksafon, huyu alikuwa Mzimbabwe aliyezaliwa Bulawayo akahamia Kongo. Alijiunga na OK Jazz mwaka 1957 na alikuja kuwa rafiki wa karibu sana wa Franco, mwishoni mwaka 1989 alipata ajali akaumia mguu, huo ukaja kuwa sababu ya kifo chake.

Nicholaus Bosuma maarufu kwa jina la Dessoin, huyu alikuwa mpiga conga wa OK Jazz alifariki siku chache baada ya kifo cha Musekiwa kifo kilichosababishwa  na kansa ya koo. 

Mungu awalaze pema wahenga hawa.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *