WAKATI presha ya mechi ya watani Yanga na Simba ikizidi kupamba moto, staa wa zamani wa Moro United na Tukuyu Stars, Emmanuel Mwagamwaga amesema mchezo huo utakuwa na mabao ya kutosha yaani GG kwani kila mmoja ina watu wa kutupia nyavuni.
Mkongwe huyo amesema kutokana na ubora wa timu zote, lakini Simba ndio wenye uhitaji mkubwa wa pointi tatu ili kuondoa uteja waliouonesha kwa watani zao kwa kufungwa mechi nne mfululizo.
Timu hizo zinatarajia kukutana uwanjani Machi 8, ambapo hadi sasa Yanga ndio inayoongoza msimamo ikiwa na pointi 58, huku Simba akiwa nafasi ya pili na alama 54 zikitofautiana mechi ilizocheza, Yanga ikiwa na 22 na Simba 21.
Hata hivyo, watani hao wanakutana ikiwa Yanga anajivunia rekodi ya kuitambia Simba katika mechi nne mfululizo ziloizopita ikiwamo kipigo cha ‘aibu’ cha 5-1 kilichopatika msimu uliopita katika mechi iliyopigwa Novemba 5, 2023. Yanga ilishinda pia mechi ya marudiano ya msimu uliopita, ikafanya hivyo katika Ngao ya Jamii na katika mchezo wa kwanza wa msimu huu wa Ligi Kuu kila moja ikishinada 1-0.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwagamwaga alisema mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa timu zote kwa sasa na mchezaji mmoja mmoja ambao yeyote anaweza kuamua matokeo.
Alisema kwa kasi waliyoonesha timu zote kwenye mechi zao, haoni mpambano huo ukiisha bila bao, akieleza kuwa dakika 90 zitaamua japokuwa lazima wababe hao wafungane ‘GG’.
“Naona idadi kubwa ya mabao kwenye mechi hiyo, hakuna timu ya kupaki basi, japo Simba ndio yenye kuhitaji zaidi wa matokeo ili kuweka utulivu kikosini, wameteswa sana,” alimwa Mwangamwaga na kuongeza;
“Kwa ubora wa timu zote sina shaka, wachezaji kila mmoja anao uwezo wa kuamua matokeo na isitoshe mchezo huo unaweza kutoa muelekeo wa nani bingwa msimu huu.”
Kiraka huyo aliongeza kuwa, pointi walizotofautiana watani hao, inaweza kuwa vita nyingine kali, lakini makali ya Ellie Mpanzu, Steve Mukwala na Kibu Denis (Simba) na Clement Mzize, Aziz Ki wa Yanga wanaweza kuamua mchezo huo wa 114 katika ligi ya Bara tangu 1965.

Timu hizo zinaenda kukutana kila moja ikitoka kushinda mechi iliyopita ya Ligi Kuu ikiwa ugenini, Yanga ikiitambia Pamba Jiji kwa mabao 3-0 jijini Mwanza na Simba kuinyoosha Coastal Union kwa idadi kama hiyo mechi iliyopigwa jijini Arusha.
Lakini washambuliaji wa timu hizo, Jean Charles Ahoua, Leonel Atena na Steve Mukwala wakichuana na wenzao, Clement Mzize, Prince Dube, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz KI katika orodha ya wafungaji mabao kwa sasa katika ligi hiyo inayoingia raundi ya 23 kuanzia keshokutwa Jumatano.