
Arusha. ‘Mgeni njoo, mwenyeji apone.’ msemo huu unaelezea hali ilivyo jijini Arusha ambapo wageni kutoka maeneo mbalimbali wameanza kufurika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayofanyika hapa kitaifa, huku wenyeji wakinufaika na fursa hiyo.
Maadhimisho hayo yatafanyika Jumamosi Machi 8, 2025 huku Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Miongoni mwa fursa ambazo wakazi wa Arusha wanazitumia vyema ni biashara ya nyumba za kulala wageni ambapo mpaka asubuhi ya leo, nyingi zilikuwa zimejaa huku wageni wakiaswa kufanya ‘booking;’ mapema.
Pareso Pastor ambaye ni Meneja wa miongoni mwa hoteli jijini hapa akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Machi 6, 2025 amesema kabla hujafika jijini humo kuhusu suala la malazi ni vyema utafute eneo mapema (booking) kutokana na maeneo mengi kujaa.
“Kipindi cha mikutano hapa Arusha kunakuwa na wageni wengi na biashara inachangamka, kama sasa hivi kuelekea siku ya wanawake biashara imechangamka ‘booking’ zimefanywa kabla hata ya tarehe husika.
“Kipindi hiki mtu anatakiwa afanye ‘booking’ mapema kabla hajafika ili asikose eneo la kulala, mfano kama hapa kwangu mimi vyumba vyote vimejaa na kuna ambavyo wageni watatoka, booking zimeshafanywa hadi tarehe 12,” amesema.
Pastor ameongeza ongezeko hilo la idadi ya watu linafanya mzunguko wa biashara pia uongezeke na kunufaisha mtu mmoja mmoja.
“Biashara zinaongezeka na kipato cha mtu mmoja mmoja na kwa mkoa kwa ujumla kama hivi sasa kinaongezeka, kwa sababu mamantilie anauza, sisi watu wa malazi wageni wakija watakula, watahitaji usafiri na bodaboda nao wataingiza pesa,” amesema Pastor.
Kuhusu kujaa kwa nyumba za kulala wageni jijini Arusha katika kipindi hiki, ikiwa imebaki siku moja maadhimisho haya yafanyike, Scola Daniel ambaye pia ni meneja wa hoteli jijini hapa amesema wao tangu jana vyumba vyote vilishajaa.
“Katika kipindi hiki wageni wamefika, mpaka sasa hivi tumejaza vyumba vyote na vipo ambavyo vimeshafanyiwa booking tangu wiki iliyopita. Hapa kwetu tangu jana Machi 5, palikuwa pameshajaa na wageni wataanza kuachia vyumba Machi 9 na 10,”amesema Scola.
Mamantilie
Wakati hali ikiwa hivyo katika sekta ya malazi, mamantilie katika eneo la Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta ambapo maonyesho ya kuelekea siku ya wanawake yanafanyika wanasema biashara imekuwa nzuri tangu Machi Mosi 2025.
“Kwa sasa hivi wageni wameongezeka, tunauza sana tofauti na kipindi cha nyuma, hapa kwa siku nafunga na faida hadi ya Sh70,000 na chakula hakilali,” amesema Penina Lyimo ambaye anauza chakula jirani na eneo hilo.
Akizungumzia neema hiyo, Robison Ndareso ambaye anauza chipsi eneo hilo amesema, ongezeko la wageni na maonyesho hayo yamemfanya aongeze kipimo cha kukaanga viazi.
“Siku ya kwanza maonyesho yalivyoanza, kabla ya saa 11 jioni chipsi ziliisha na nilichukua viazi vichache, lakini baada ya kuona idadi ya wageni imeongezeka na mimi sasa hivi nimeongeza viazi ninavyonunua sokoni kutoka ndoo kubwa mbili hadi tatu,”amesema Ndareso.
Bodaboda waelezea fursa
Mbali ya tukio hilo la kitaifa litakalofanyika Arusha Machi 8 kuneemesha sekta ya malazi na chakula, Daniel Sima ambaye ni mwenyekiti wa kituo cha Bodaboda Kimahama jijini Arusha amesema wanapata wateja wengi wa kuwapeleka nyumba za wageni.
“Tumefurahia ujio wa sherehe hii, kwa sisi bodaboda tumepata fursa nyingi kwa sababu watu wamekuja Arusha kutoka maeneo mbalimbali na idadi ya watu imeongezeka, tumepata neema kwa sababu tunapeleka wateja wengi hotelini na gesti.
“Kwa sasa hivi sehemu nyingi za kulala wageni zimejaa, kama jana nilikuwa na mgeni hakufanya booking tulizunguka kwenye hoteli zaidi ya nne anakosa vyumba,”amesema Sima.
Johson Shirima ambaye naye ni dereva wa bodaboda katika stendi ndogo jijini hapa amesema: “Matukio kama haya yanaongeza mzunguko wa fedha na kwetu inakuwa fursa kwa sababu, wafanyabiashara nao wanauza sana, tofauti na wakati ambao unakuwa hauna tukio, na mtu ambaye hajafanya booking ya chumba, kwa sasa hivi atateseka sana.”
Watoa huduma za
kifedha nao waguswa
Martha Lucas ambaye ni wakala wa huduma za kifedha katika eneo la Makao mapya jijini Arusha amesema wageni wanapofika huduma hiyo inafanyika sana.
“Sio kipindi hichi tu, hata kukiwa na mikutano hapa Arusha wageni wanakuwa wengi na wakitaka kutuma fedha majumbani kwao wanatutumia sisi mawakala, kwa hiyo biashara inakuwa nzuri,”amesema Martha
Ongezeko la wageni katika Jiji la Arusha pia linaakisiwa na takwimu za Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) ambayo inaonyesha mwenendo wa wageni kuwasili nchini kwa ujumla, Arusha ikiwa miongoni mwa kitovu chake imezidi kuongezeka.
“Mwaka 2021 jumla ya watalii 922,692 waliwasili nchini, mwaka 2022 waliongezeka hadi kufikia 1,454,920 pia mwaka 2023 waliongezeka tena hadi watalii 1,806,359.
“Idadi hiyo iliongezeka tena mwaka 2024 hadi kufikia watalii 2,141,895, ambapo kutoka mwaka 2021 hadi 2024, idadi ya watalii imeongezeka kwa jumla ya 1,219,203,” zimeeleza takwimu.
Pia, kwa mujibu wa Ripoti ya Uchumi wa Kikanda ya Benki Kuu ya Taifa (BoT) Mkoa wa Arusha mchango wake katika Pato la Taifa umeongezeka mwaka 2023 ikilinganishwa na mwaka 2022.
“Mwaka 2022 mchango wa Pato la Taifa wa Mkoa wa Arusha ulikuwa Sh8.02 bilioni huku ukiongezeka hadi Sh8.87 mwaka 2023,”imeeleza ripoti hiyo,
Akizungumzia faida ya ongezeko hilo la watu, Mchumi, Mack Patrick amesema mzunguko wa fedha utaongezeka na biashara zitafanyika, pia Serikali itapata kodi.
“Ongezeko la wageni katika jiji la kitalii kama Arusha halinufaishi tu wamiliki wa hoteli na nyumba za wageni, naona hapo mnyororo wa thamani ukiongezeka.
“Mahitaji ya huduma mbalimbali kama malazi, chakula, usafiri, na burudani, hali inayochochea ukuaji wa biashara ndogo na za kati na Serikali nayo itapata kodi,”amesema Patrick.