
Mshambuliaji wa Al Ahly Tripoli, Cristovao Paciencia Mabululu amezua kihoja kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa baada ya kuonekana akikagua nje kabisa ya eneo la kuchezea kwa kunyanyua nyavu na kuchomoa vibendera kuangalia kama kuna kitu kimewekwa.
Tukio hilo limetokea muda mchache kabla ya wachezaji kupasha misuli ikiwa ni utaratibu maalumu kwa wachezaji kutazama uwanja kabla ya kurejea kwenye vyumba vya kubadilisha nguo na kuwa tayari kwa maezoezi mepesi.
Hata hivyo, kitendo hicho ambacho ni kinyume na taratibu kiligundulika haraka na walinzi watatu wa uwanjani ambao walimkimbilia na kumuondoa.
Kitendo hicho, Mabululu aloneakana kukifanya upande ambao Simba iliutumia kupasha misuli na hata wakati akiondolewa alionekana mwenye kujiamini kabla ya ofisa wa timu yake kumkimbilia kwa ajili ya kumsapoti.
Wekundu wa Msimbazi, Simba wapo nyumbani kumalizana na Walibya hao kwenye Kombe la Shirikisho Afrika baada ya mchezo wa kwanza kutoka suluhu wakiwa ugenini wikiendi iliyopita.