Mabomu ya machozi yarindima tena Songea, Heche naye adakwa

Songea. Mkutano uliopangwa kufanyika leo saa tano asubuhi kati ya waandishi wa habari na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, umevurugika baada ya Polisi kuwatawanya wanachama na wafuasi wa chama hicho waliokusanyika katika ofisi za chama zilizopo eneo la soko la Mfaranyaki, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Hata hivyo, hii ni mara ya pili kwa wafuasi hao kutawanywa na mabomu ya machozi baada ya jana Aprili 9, 2025, pia kutawanywa kutokana na kugomea kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chadema, Taifa, Tundu Lissu.

Lissu alikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma muda mchache baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Mbinga mkoani humo.

Mpaka sasa bado haijafahamika chanzo cha Lissu na walinzi wake wawili, kada mmoja wa chama aliyefahamika wa jina la Shija Shebeshi kushikiliwa na Polisi.

Hivyo, wananchi waliokuwa kwenye mkutano huo, waligomea kukamatwa kwa Lissu huku wakisema mwenyekiti haendi popote, ndipo Polisi walipoamua kupiga mabomu ya machozi mfululizo ili kuwatawanya na kumchukua mwenyekiti huyo.

Leo Alhamisi, Aprili 10, 2025, Polisi walifika katika ofisi za Chadema saa nne asubuhi, kulikotangazwa kufanyika mkutano baina ya viongozi wa chama hicho na waandishi wa habari na kuanza kuwatawanya baadhi ya wanachama waliokuwa wakimsubiri pia Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa, John Heche aliyekuwa mzungumzaji katika mkutano huo.

Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya kuhusiana na tukio hilo, amesema anafuatilia tukio hilo sambamba na taarifa ya kukamatwa kwa Lissu amesema atatoa taarifa baadaye.

“Lakini nimesikia Chadema wana mkutano ofisini kwao, haturuhusu mikutano,” amesema kamanda huyo.

Licha ya polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya, baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema walirejea tena katika eneo hilo wakiendelea kusubiri ujio wa kiongozi wao, huku wakinawa nyuso kwa maji na kunywa wakisisitiza kuwa wanapigania haki na mkutano utafanyika kama ulivyopangwa, ingawa eneo hilo pamoja na viwanja vya Matalawe walikopanga kufanya mkutano wa hadhara tayari limezingirwa na Polisi.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Aden Mayala, alipohojiwa na Mwananchi juu ya kinachoendelea, alikataa kuzungumza huku akisema anamsubiri Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche awasili na kuzungumza kwanza kabla yeye hajatoa kauli nyingine.

Mkutano wakatishwa

Hata hivyo, wakati Heche akiendelea na mkutano huo, Polisi walizingira ofisi hiyo na kuingia katika chumba cha mkutano, wakimtaka kiongozi aache kuzungumza na wanahabari badala yake afuatane nao kuelekea kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia amesema, “mkutano wa Heche haukumalizika baada ya kutakiwa kwenda kwa RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa), jambo ambalo makamu mwenyekiti amelitii,”amesema Rupia.

Hadi sasa bado haijafahamika chanzo cha Lissu kushikiliwa na polisi, ingawa jana Kamanda Chilya aliliambia Mwananchi yupo katika ufuatiliaji kuthibitisha kuwepo kwa taarifa hizo, akiahidi leo kuuelezea umma kuhusiana na tukio hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *